Na. Andrew Chimesela - Morogoro.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe ameunda kamati ya wajumbe kumi kwa ajili ya kuchunguza wizi wa mafuta ambao umeota mizizi katika mradi wa ujenzi treni ya mwendo kasi hapa nchini (standard Gauge Railway - SGR) kipande cha Morogoro.

Dkt. Kebwe ametoa agizo la kuunda kamati hiyo Julai, 16 mwaka huu alipofanya ziara ya kushtukiza katika kambi ya Ngerengere akiongozana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kwa lengo la kujiridhisha kutokana na taarifa alizonazo za uwepo wa changamoto hiyo ya wizi wa mafuta katika mradai huo mkubwa.

Aidha, Dkt. Kebwe na Wajumbe wa KUU walitaka pia kujiridhisha jinsi kampuni hiyo inavyopokea mafuta, inavyotoa na jinsi inavyofuatilia matumizi ya mafuta hayo kwa waendesha mitambo mbalimbali katika eneo hilo la Ngerengere.

Baada ya kumaliza kikao cha ndani kati ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na uongozi wa Kamapuni inayoendesha mradi huo wa SGR, ndipo Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akatoa agizo kwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Lucas Mwaisaka kuunda Kamati ya Uchunguzi.

Kamati hiyo ya Wajumbe kumi imepewa siku saba na kuwasilisha taarifa yake Julai 24 mwaka huu, taarifa hiyo pamoja na hadidu nyingine za rejea ieleze mlolongo mzima wa upokeaji na utoaji wa mafuta, kuchunguza watu wanaojihusisha kwa ufisadi huo wa mafuta kama wako ndani au nje ya kampuni hiyo. 

Hata hivyo Dkt. Kebwe alimuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro kuanza mara moja oparesheni itakayofanyika usiku na mchana ya kuwasaka wahusika wa wizi wa mafuta hayo, huku akitaka meneja wa Kampuni ya ujenzi wa SGR kukaa pamoja na Kamanda huyo ili kukubaliana namna polisi watakavyoshiriki katika ulinzi wa mafuta na mali nyingine za mradi huo. 

Naye Meneja wa Earth Works Joao Sousa alisema kwao ni vigumu kujua kama mafuta hayo yanaibiwa wakati wa kazi ama wakati wa chakula cha mchana ambapo waendesha mitambo wengi wanapata chakula na mitambo inakuwa imezimwa na mitambo mingine inakuwa maeneo ya mbali na maeneo wanayopata chakula cha mchana.

Akijibu swali la Mkuu wa Mkoa juu ya upotevu wa mafuta, Msimamizi wa Walinzi katika Kampuni hiyo Evance Mwakitwange alitaja moja ya sababu za wizi huo kuwa ikiwa ni pamoja na uchache wa walinzi ukilinganisha na wingi wa mitambo na eneo kubwa linaloegeshwa mitambo hiyo. lakini pia alieleza kuwa usumbufu mkubwa katika kulinda mitambo hiyo wanaupata wakati waaendesha mitambo wanapokwenda kupata chakula cha mchana.

Alisema wamejitahidi kupambana sana na tatizo la wizi wa mafuta lakini suala la kutoegesha pamoja mitambo hiyo wakati wa chakula cha mchana ni changamoto pamoja na kuwa walishatoa ushauri kwa uongozi kuegesha pamoja mitambo hiyo lakini ushauri wao haujafanyiwa kazi.

Aidha, Mwakitwange ameyataja maeneo ambayo yanaongoza kwa wizi wa mafuta kuwa ni eneo la kilometa 157, 158 na kilometa 160 ambavyo viko eneo la Mikese huku akibainisha kuwa jitihada zao katika kuepusha wizi huo walitoa taarifa Kituo cha Polisi na kuomba msaada zaidi.

Wajumbe walioteuliwa kwenye kamati hiyo ni pamoja na mjumbe mmoja kutoka Ofisi ya RPC, RSO na TAKUKURU kwa ngazi ya Mkoa. Wajumbe wengine ni kama waliotajwa hapo juu lakini ni kwa ngazi ya Wilaya. Mjumbe mwingine atatoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na watatu watatoka upande wa Kampuni inayoendesha mradi wa SGR.

Kwa taarifa zilizomfikia mwandishi wa habari hizi, hadi msafara wa Mhe. Mkuu wa Mkoa unarejea Ofisini kwake tayari mtu mmoja kati ya wanaotuhumiwa kujihusisha na mtandao wa wizi wa mafuta katika kampuni hiyo alikuwa ametiwa nguvuuni na jeshi la polisi kwa mahojiano.
 Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye, akisalimiana na Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike, baada ya kuwasili Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji yaliyopo jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi barabara ya ohio jijini Dar es Salaam.
Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike, akisaini kitabu cha wageni alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji yaliyopo jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi barabara ya ohio jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara yake ya kujitambulisha na kukuza mahusiano katika vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, (Kushoto) ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye. Picha na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. IMEANDALIWA NA KITENGO CHA HABARI NA ELIMU KWA UMMA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF) Thobias Andengenye atembelewa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Phaustine Kasike mapema leo asubuhi katika Makao Makuu ya Jeshi hilo yaliyopo jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi barabara ya ohio jijini Dar es Salaam. Lengo ni kujitambulisha na kukuza mahusiano kati ya vyombo hivyo viwili vya Ulinzi na Usalama.

Katika ziara hiyo Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye, alitumia fursa hiyo kumpongeza kwa kuteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza na kumuahidi ushirikiano katika kulijenga Taifa. 

Vilevile Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike amepata fursa ya kujifunza jinsi gani Jeshi hilo linavyoendesha shughuli zake pamoja na kufanya mazungumzo ya kina na Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo.

“Nimejifunza mengi lakini pia nashukuru kwa kupata fursa ya kutembelea na kuona ni jinsi gani tunaweza kushirikiana” alisema Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Phaustine Kasike akipokea saluti kutoka kwa Kamishna wa Utawala wa Magereza, Gaston Sanga mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Ofisi ya Makao Makuu ya Jeshi la Magereza jijini, Dar es Salaam, leo Julai 16, 2018.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akipokea salamu ya heshima kutoka kwa Gwaride maalum lililoandaliwa kwa ajili ya mapokezi yake Makao Makuu ya Jeshi hilo.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akikagua gwaride maalum lililoandaliwa na Maofisa na askari wa Jeshi la Magereza.
Kamishna Jenerali mstaafu, Dkt. Juma Malewa(suti nyeusi) akimkaribisha Kamishna Jenerali mpya wa Magereza, Phaustine Kasike mara baada ya kumaliza kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa na maofisa na askari wa Jeshi la Magereza.
Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali nchini wakifanya mahojiano maalum na Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike mara baada ya mapokezi Makao Makuu ya Jeshi hilo.
Kamishna Jenerali mstaafu wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(suti nyeusi) akifurahia jambo pamoja na Kamishna Jenerali mpya wa Magereza Phaustine Kasike wakiongozana kuelekea katika mazungumzo maalum na Maofisa, askari na watumishi raia wa Jeshi hilo Makao Makuu ya Magereza.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na Maafisa, askari na watumishi raia wa Jeshi hilo.
Maafisa waandamizi wa Jeshi la Magereza, Maafisa, Askari na watumishi raia wa Makao Makuu ya Jeshi la Magereza wakifuatilia kwa makini hotuba ya Kamishna Jenerali mpya wa Jeshi hilo(Picha zote na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Makao Makuu ya Jeshi la Magereza).
Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia viongozi wa vyama vya Siasa kutoka nchi za mbalimbali za Afrika kabla ya kufungua mkutano kati ya viongozi wa vyama hivyo na Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) katika ukumbi wa Serena Hotel jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya kimataifa na Waziri wa Mahusiano wa Kimataifa wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) Song Tao akizungumza katika mkutano huo wa viongozi wa vyama vya Siasa kutoka nchi za mbalimbali za Afrika na Chama hicho cha CPC jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bashiru Ally akihutubia katika mkutano huo.
Washiriki wa Mkutano huo wakifatilia kwa makini hotuba mbalimbali zilizokuwa zikitolewa ukumbini hapo katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya kimataifa na Waziri wa Mahusiano wa Kimataifa wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) Song Tao mara baada ya kufungua mkutano huo jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akijibu kero mbalimbali za wananchi katika kijiji cha Mariwanda kata ya Hunyari wilaya ya Bunda mkoani Mara wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo jana. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Lydia Bupilipili na Mbunge wa Bunda Vijijini, Bonafasi Mwita Getere (kulia).

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisalimiana na uongozi wa wilaya ya Bunda alipowasili wilayani hapo jana kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja.Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza uongozi wa wilaya ya Bunda ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Lydia Bupilipili (kulia kwake) wakati wa ziara yake ya siku moja kwa ajili ya kutatua changamoto za uhifadhi wilayani humo jana.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wananchi wa kata Nyatwali wakati wa ziara yake ya siku moja kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali za uhifadhi katika wilaya ya Bunda mkoani Mara jana. Wengine pichani kutoka kushoto ni Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TANAPA, Martin Loibooki na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili (wa pili kulia).
Mwananchi wa kata Nyantwali akitoa maoni yake kwa Waziri Kigwangalla.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bukore wakati wa ziara yake ya siku moja kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali za uhifadhi katika wilaya ya Bunda mkoani Mara jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini, Bonifasi Mwita Getere muda mfupi baada ya kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Bukore wakati wa ziara yake ya siku moja kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali za uhifadhi katika wilaya ya Bunda mkoani Mara jana.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mariwanda wakati ziara ya Waziri Kigwangalla wilayani humo.
Baraka Abdul, mkazi wa kijiji cha Mariwanda akiwasilisha maoni yake kwa waziri Kigwangalla katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.
Dk. Kigwangalla akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mariwanda.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akijibu akifafanua jambo katika mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Mariwanda kata ya Hunyari wilaya ya Bunda mkoani Mara wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo jana.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Dk. James Wakibara akifafanua jambo kwenye mkutano huo.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mariwanda wakimasikiliza Waziri Kigwangalla (hayuko pichani) wakati wa mkutano wa hadhara kijijini hapo.

Na Hamza Temba-Bunda, Mara.

Kilio cha muda mrefu cha wananchi wa wilaya ya Bunda hususan katika ukanda unaopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuhusu wanyamapori waharibifu jamii ya Tembo kuvamia makazi yao na mashamba kinaelekea kupata ufumbuzi wa kudumu.

Hatua hiyo inakuja kufuatia agizo la Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla kwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuanzisha mradi wa ufugaji nyuki kwa vijiji kumi vinavyopakana na hifadhi hiyo ili watumike kama uzio wa kudhibiti wanyamapori hao.

Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo jana kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mariwanda, kata ya Hunyari wilaya ya Bunda mkoani Mara wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja wilayani humo. 

"TANAPA wakishirikiana na TFS waje waanzishe mradi wa ufugaji nyuki wa kisasa katika vijiji vyote 10 vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti, waje wahamasishe uundwaji wa vikundi, wafundishe namna ya kuweka mizinga ya kisasa na namna ya kufuga nyuki na kuvuna, na mwisho wa siku wananchi wapate faida ya kuzuia wanyamapori kuvamia mashamba na makazi yao pamoja na kuvuna asali itakayowatengenezea kipato mbadala" ameagiza Dk. Kigwangalla. 

Akielezea mbinu hiyo mpya inavyofanya kazi Dk. Kigwangalla amesema, wataalamu ndani ya wizara yake wameeleza kuwa mbinu hiyo ya kuweka mizinga ya nyuki kuzunguka maeneo ya mashamba na makazi ya wananchi itasaidia kudhibiti Tembo kwakuwa huogopa sana nyuki na endapo wakisikia tu harufu yake huwa vigumu kusogelea maeneo hayo.

Awali akiwasilisha malalamiko kwa niaba ya wananchi wa vijiji hivyo, Mbunge wa Bunda Vijijini, Bonifasi Mwita Getere alisema kwa muda mrefu sasa wananchi hao wamekuwa wakipata madhara ya kuvamiwa na Tembo ambao hula mazao yao mashambani na hata majumbani, kuwajeruhi wananchi na wengine kupoteza kabisa maisha.

Baraka Abdul ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mariwanda wilayni humo alisema, mbinu zinazotumika kufukuza Tembo hivi sasa ikiwemo kupiga makelele na madebe na kutumia tochi za mwanga mkali zimekua hazisaidii, hivyo ameiomba Serikali kuongeza idadi ya askari na vituo katika maeneo yanayoathirika zaidi na matukio hayo.

Wakati huo huo, Waziri Kigwangalla ametoa onyo kali kwa wananchi wanaofanya vitendo vya ujangili na uingizaji mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuwataka kuacha mara moja kwakuwa wakikamatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kutaifishwa mifugo yao kwa mijibu wa kifungu cha 111 Na. 5 cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2009.

Katika hatua nyingine, ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kupitia eneo la mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Bufer Zone) kuanzia Ghuba ya Speke hadi kwenye mpaka na nchi ya Kenya, wabaini mipaka halisi na ramani na kuainisha mahitaji ya wananchi na changamoto zilizopo na hatimaye kuwasilisha kwake mapendekezo ya kuondoa changamoto zilizopo.
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam.

Benki ya Credit Suisse ya nchini Uingereza imeonesha nia ya kuipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa zaidi ya Dola milioni 200 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo ikiwemo miradi mikubwa ya Nishati ya Umeme na miundombinu ya Reli.

Hayo yamebainishwa Jijini Dar es Salaam katika Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na Ujumbe wa Benki ya Credit Suisse ya Uingereza ulioongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Bw. Lawrence B. Fletcher, kuhusu ushirikiano katika miradi ya maendeleo.

Dkt. Mpango alisema kuwa tayari zipo hatua mbalimbalimbali zimefikiwa katika kufanikisha upatikanaji wa Mkopo kutoka Benki ya Suisse hivyo kuwa na tumaini la kupata kiasi cha Dola milioni 2000 katika mwaka wa fedha wa 2018/19 .

“Miradi ya Kipaumbele ambayo Serikali inaitekeleza ni pamoja na Ujenzi wa Reli kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), kufufua Shirika la Ndege Tanzania kwa kununua Ndege mpya na miradi ya umeme ambayo itachochea maendeleo ya watu na Taifa kwa ujumla”, alieleza Dkt. Mpango.

Aliitaja miradi mingine ambayo Serikali inampango wa kuitekeleza kuwa ni pamoja na Ujenzi wa Bwawa la Umeme la Rufiji (Rufiji Haydro Project) ambalo kukamilika kwake kutasaidia kuzalisha umeme wa Megawati 2100 ambao utatumika katika kuchochea uchumi wa viwanda unaohitaji umeme wakutosha.

Waziri Mpango amebainisha kuwa Serikali inatekeleza miradi ya kupanua Bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Kigoma pamoja na ujenzi wa miradi mbalimbali ya barabara ambazo zitahudumia nchi ya Tanzania na nchi jirani ya Rwanda na Burundi hivyo kuchochea maendeleo.

Ameishukuru Benki ya Suisse, kwa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya Maji, barabara na Umeme na kuahidi kuendelea kukuza ushirikiano na Benki hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Credit Suisse ya nchini Uingereza, Bw. Lawrence B. Fletcher, amesema kuwa Benki yake inaangalia uwezekano wa kufadhili miradi ya kipaumbele ya Serikali ili kuweza kufanikisha nia yake ya kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda.

Aidha amesema Benki yake itatoa mkopo wa Dola milioni 200 baada ya hatua za mkopo huo kukamilika katika mwaka huu wa fedha ili kuweza kufanikisha kutekeleza miradi mbalimbali lakini pia ikiwa ni sehemu ya kudumisha ushirikiano kati ya Benki yake na Tanzania.