Monday, July 7, 2008

Mamlaka ya chakula na dawa iwezeshwe

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii ya Jamhuri ya Muungano Tanzania imetakiwa kuijengea uwezo Mamlaka ya Chakula na Dawa ili iweze kudhibiti ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba na kutoifanya Tanzania kuwa dampo la bidhaa zisizofaa.

Rais Karume aliihakikishia Mamlaka ya chakula na dawa kuwa serikali iko pamoja na Mamlaka hiyo katika jambo hilo na itaendelea kuiunga mkono Wizara kwa maslahi ya Watanzania.

Changamoto hiyo imetolewa leo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume katika sherehe ya maadhimisho ya miaka mitano ya Mamlaka ya Chakula na Dawa sambamba na uzinduzi wa jenfo jipya la ofisi na maabara, mjini Dar-es-Salaam.

Akitoa hutuba yake katika sherehe hizo Rais Karume alisisitiza kuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa ni lazima ihakikishe kuwa utekelezaji wa kazi za Mamlaka hiyo unafanyika kwa kuishirikisha jamii na washirika wengine wa maendeleo.

“Pamoja na kwamba Mamlaka ya Chakula na Dawa imeundwa kwa lengo la kulinda afya za watumiaji wa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba dhidi ya athari za kiafya zinazoweza kutokana na matumizi ya bidhaa hizo, nidhahiri kuwa kazi hii itafanywa kikamilifu iwapo wananchi watatoa ushirikiano wa karibu kwa Mamlaka”,alisema Rais Karume.

Aidha, Rais Karume alieleza kuwa iwapo Mamlaka itawatumia wananchi kama washirika wa kwanza katika kutekeleza kazi za mamlaka ikiwa ni pamoja na kuwa na uhusiano mzuri na vyombo vya habari na kuvitumia ipasavyo kazi ya kutoa elimu itafanikiwa zaidi

Pia, Rais Karume aliwaasa wananchi kwamba wanaponunua bidhaa za dawa, chakula na vipodozi kuwa waangalifu sana wa tarehe za matumizi yake na wakivitia shaka wawe wepesi kutoa taarifa kwa Mamlaka husika.

Rais Karume aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kutoa taarifa mara moja pale wanapopata madhara baada ya kutumia dawa, chakula, na vipodozi kwani kwa kufanya hivyo wataiwezesha Mamlaka kufuatilia na kufanya uchunguzi wa haraka ili kubaini msingi wa madhara.

Rais Karume aliitaka Mamlaka hiyo kuandaa programu mbali mbali za kuielimisha jamii mjini na vijijini ili Mamlaka hiyo iweze kufahamika na jamii nayo iweze kuona jukumu lake la kulinda afya zao kwa kuzitambua bidhaa bandia na zisizokidhi viwango ili hatimae waweze kutoa taarifa kwa mamlaka.

Katika maelezo yake pia, Rais Karume aliipongeza mikakati ya Mamlaka katika kuendeleza viwanda vya kutengeneza dawa na chakula vilivyopo hapa nchini jambo ambalo ni la kujivunia kufanywa na taasisi ya ndani hasa ikizingatiwa kuwa juhudi hizi zinaendana na malengo ya MKUKUTA na MKUKUZA.

Mamlaka hiyo pia ilitakiwa kuendeleza ushirikiano katika kufanikisha kazi zake katika sehemu zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na nchi jirani.

“Nashauri mtilie mkazo pia kuwepo kwenu katika miji ya mipaka yote ambako bidhaa nyingi za chakula na dawa hupitishwa. Aidha natilia mkazo ushirikiano wenu na wezenu wa Zanzibar katika shughuli hizi na pia kwa nchi jirani ili udhibiti uwe na mafanikio makubwa zaidi.

Rais Karume alitoa rai kwa Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara nyengine kuimarisha mazingira ya uwekezaji katika viwanda vya dawa na vyakula ili kukuza uchumi wa nchi na kurahisisha udhibiti sambamba na kuvisaidia viwanda vya mazao ya kilimo.

Pia, Rais Karume alieleza kufarajika kwake kwa kuanzishwa kwa Mpango wa Maduka ya Dawa muhimu kupitia sekta binafsi ambayo yatakuwa na mchango mkubwa katika kusaida sekta ya umma na kutoa wito kwa kwa mamlaka hiyo kuzidisha kasi katika uchunguzi wa madawa, hasa ikizingatiwa kuzidi kwa dawa feki ulimwenguni ambazo baadhi yake zinaletwa na nchini na watu wasiokuwa na mema kwa wenzao.

Rais Karume pia aliishauri Mamlaka hiyo kuimarisha ushirikiano na vyombo na taasisi nyengine za kiserikali na zisizo za kiserikali ambazo zinafanya kazi ya udhibiti kama vile Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wafanyabiashara wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba pamoja na Tume ya Ushirindani.

Mapema Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Profesa David Homeli Mwakyusa alieleza kuwa kwa kutambua kwamba usalama wa chakula ni muhimu katika kulinda afya ya walaji, Wizara anayoisimamia inaandaa sera ya chakula kwa ajili ya kutoa mwongozo bayana kuhusiana na masuala ya usalama wa chakula katika nchi.

Aidha, Waziri Mwakyusa alisema kuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa imeweka mikakati maalum ya kupambana na dawa bandia ambayo inalenga katika kutambua na kuziondoa dawa hizo pale zinapoingizwa nchini.

Nae Balozi wa Denmak nchini Tanzania, Bwana Bjarne Sorensen akitoa salamu kwa Niaba ya Washirika wa Maendeleo alitoa pongezi zake kwa Wizara ya Afya kwa kusimamia vyema Mamlaha ya Chakula na Dawa na kueleza kuwa nchi yake pamoja na washirika wote wa Maendeleo wataendelea kuiunga mkono Tanzania katika shukuli za kimaendeleo.

Katika Sherehe hizo Rais Karume pia alipokea maandamano ya Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo pamoja na wanafunzi na kutoa zawadi kwa wafanyakazi waliosaidia na kutoa mchango mkubwa katika kuendeleza juhudi za Mamlaka hiyo.
.
Rajab Mkasaba, Dar-es-Salaam

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu