Jumla ya wanafunzi 567,567 wamefaulu mitihani ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2011na watafanyiwa mtihani wa majaribio kabla ya kuanza masomo yao rasmi katika shule walizochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.

Akitangaza matokeo hayo (leo), jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Philipo Mulugo (Mb.) amesema, utaratibu huo wa kufanyiwa majaribio utaanza mwakani 2012, ambapo wanafunzi waliofaulu watafanyiwa majaribio ya kupima stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.

Wakati huo huo, Baraza la Mtihani la Taifa limefuta matokeo yote ya watahiniwa 9,736 sawa na asilimia 1.0 waliobainika kufanya udanganyifu wakati wa mtihani huo.

“Mwanafunzi atakayebainika kuwa kajiunga na kidato cha kwanza bila kumudu stadi hizo, Mwalimu Mkuu wa shule alikotokea mwanafunzi huyo na Msimamizi wa Mtihani wakumaliza elimu ya msingi watachukuliwa hatua za kinidhamu,” amesema Waziri Mulugo.

Akizungumzia kuhusu kiwango cha ufaulu alisema kimeongezeka hadi kufikia asilimia 58.28 ukilinganisha na cha mwaka jana ambacho kilikuwa asimilia 53.52.

Aliongeza kuwa kiwango cha ufaulu wa masomo ya Kiingereza, Sayansi na Hesabu kimepanda . Somo la Kiingereza kutoka asilimia 36.47 mwaka jana hadi asilimia 46.70 kwa mwaka huu , wakati somo la Sayansi ni asilimia 61.33 mwaka huu toka asilimia 56.05mwaka jana na Hesabu asilimia 39.36 mwaka huu toka asilimia 24.70mwaka jana.

Jumla ya wanafunzi 983, 545 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwezi wa Septemba 2011 na kuonesha kuwa, kiwango cha ufaulu kimeongezeka kutoka asilimia 53.52 mwaka jana hadi 58.28. Jumla ya wasichana waliofaulu ni 27,377 na wavulana ni 289,190.

Wakati huo huo, Serikali imesema, kazi ya kuhakiki madai ya walimu imekamilika tangu Desemba 2, mwaka huu na kwamba madai hayo ni kiasi cha sh. bilioni 52.

Akijibu swali lililoulizwa na waandishi kuhusu madai ya walimu, Naibu Katibu Mkuu Bw. Selestine Gesimba amesema, kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 30 ni za mishahara na bilioni 22 ni za madai mengineyo.

Bw. Gesimba ameongeza kuwa, madai ya malipo mengine yataanza kulipwa mwezi huu (Desemba) na madai ya malipo ya mishahara yatalipwa ifikapo Januari 2012.

Hata hivyo alisema tayari Hazina wameshalipa bilioni 28 za madai ya mishahara kuanzia Julai mwaka jana hadi Novemba mwaka huu.

Na Gradys Sigera & Magreth Kinabo – MAELEZO
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

1 comments:

  1. TUNASHUKURU KWA TAARIFA ZENU ZIMEKAA VZR NINAOMBA KUTUMIWA MATOKEO YA S/M KASIGA YA KOROGWE TANGA YA 2011 TAFADHARI

    ReplyDelete