Wednesday, October 7, 2015

KATIBU MKUU KIONGOZI BALOZI OMBENI SEFUE KUWA MGENI RASMI KATIKA MKUTANO WA WADAU WA TAKWIMU

unnamedvv
Afisa Habari wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Veronica Kazimoto akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 7, 2015 jijini Dar es Salaam kuhusu mkutano wa wadau wa takwimu wenye lengo la kujadili namna ya kushirikiana katika kuhakikisha takwimu za viashiria vya Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGs) zinapatikana kwa wakati unaotakiwa. Mkutano huo utafanyika kesho katika ukumbi wa hoteli ya Habour View iliyopo Dar es Salaam.
---
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

KATIBU Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue kesho anarajia kuwa Mgeni Rasmi katika mkutano wa wadau wa takwimu ulioandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa ajili ya kukubaliana jinsi ya kushirikiana katika kuhakikisha takwimu za viashiria vya Mpango wa Maendeleo Endelevu zinapatikana kwa wakati.

Akizungumza na wandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa ofisi hiyo, Veronica
Kazimoto amesema mkutano huo utafanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Habour View, Dar es Salaam ukiwa na lengo la kuelimishana juu ya kukamilika kwa utekelezaji wa Malengo ya Milenia (MDGs) na kuanza kwa Malengo mapya ya Maendeleo Endelevu – Sustainable Development Goals (SDGs).

“Kama mnavyofahamu utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia – MDGs ulikuwa ni wa miaka 15 kuanzia mwaka 2000 hadi 2015. Mpango huu wa MDGs unakamilika mwaka huu na kuanza kwa mpango mpya wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambao pia ni miaka 15 ijayo”, amesema Kazimoto.

Kazimoto amefafanua kuwa mkutano huo utahudhuriwa na wadau wa takwimu takribani 100 kutoka Wizara, Idara, Wakala na Taasisi za Serikali, Wadau wa Maendeleo, Wadau wa Sekta Binafsi pamoja na Wadau wa Taasisi za Elimu ya Juu.Aidha, Afisa Habari huyo amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeandaa mkutano huo kwa kuwa ndio yenye mamlaka nchini ya kutoa takwimu rasmi kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo na kufanya maamuzi sahihi.

Kazimoto ameongeza kuwa mwezi Septemba mwaka huu, viongozi wa nchi mbalimbali duniani akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, walikutana nchini Marekani kwa ajili ya kutathmini utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia – MDGs ambapo ilionekana kwamba kuna baadhi ya malengo yalikuwa yamefanikiwa na mengine hayakufanikiwa.Kutokana na hali hiyo, viongozi hao walikubaliana na kuridhia mpango mbadala wa MDG ambao unaitwa Mpango wa Maendeleo Endelevu ambao pia ni wa miaka 15 kuanzia 2015 hadi 2030.

Mkutano huo wa viongozi mbalimbali duniani uliidhinisha mpango huo mpya wenye malengo 17 na viashiria 169 ambavyo kila nchi kwa uratibu wa Kitengo cha Takwimu cha Umoja wa Mataifa inatakiwa kuvipitia na kuona kama kuna takwimu za kutosha kukidhi upimaji wa malengo kwa kutumia viashiria hivyo.

Malengo hayo 17 yaliyoidhinishwa na mkutano huo wa wakuu wa nchi mbalimbali duniani ni pamoja na Kuondoa Umaskini wa aina zote, kuondoa njaa, kuhakikisha kuna maisha yenye afya bora na kuhamasisha ustawi kwa wote, Kulinda uhai wa viumbe juu ya ardhi, elimu Bora na usawa wa kijinsia.

Malengo mengine ni kuhakikisha upatikanaji na matumizi endelevu ya maji na usafi wa mazingira kwa wote, kuhakikisha kuna upatikanaji wa huduma rahisi ya nishati endelevu na ya kisasa kwa wote, uwepo wa Ajira na ukuzaji wa uchumi, uwepo wa Viwanda na Miundombinu, kulinda Amani na Utawala wa Sheria na kupungunza tofauti ya kipato baina ya nchi na nchi na ndani ya nchi.

Ameyataja malelengo mengine kuwa ni pamoja na uwepo wa Miji na Jamii endelevu, kuwajibika katika Uzalishaji, kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na madhara yake, kutunza na kuwa na matumizi endelevu ya bahari pamoja rasilimali za baharini kwa ajili ya maendeleo endelevu na kushirikiana na wadau katika kufikia malengo ya SDGs.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu