Wednesday, October 14, 2015

KWAHERI DKT. ABDALLAH OMARI KIGODA

Na Profesa Mark Mwandosya.

Imenichukua muda wa zaidi ya saa ishirini kuandika machache kuhusu Dr. Abdallah Omari Kigoda, aliyetutoka akiwa Hospitali ya Apollo, New Delhi, India baada ya kuugua kwa muda mfupi. 
Katika kipindi hicho nimekuwa nikitafakari maneno gani yanaweza kumwelezea Dr. Abdallah Omari Kigoda, maneno ambayo yanaweza kumtendea haki, kuonyesha masikitiko yangu na familia yangu, na kutoa pole kwa familia yake, mkewe, watoto na ukoo wote wa Kigoda, wakiwa Handeni na popote pengine.  
Sijaweza kuyapata maneno hayo.
Kwani yangekuwa maneno mengi, na yenye kubeba ujumbe mzito.  Nakiri sina umahiri wa lugha hasa katika kipindi cha majonzi.  Neno kubwa na zito la kiswahili ni POLE kwa wote, labda kuongezea uzito ni kusema POLE SANA.  Pole hizi pia ni kwa wana Handeni aliowatumikia kwa muda mrefu wa maisha ya kazi; Mkoa wa Tanga, na wana Tanga, mliompa heshima ya uongozi wa kisiasa na maendeleo ya jamii; jamii (fraternity) ya uchumi na wachumi; na Watanzania kwa ujumla wetu.
Abdallah Kigoda ni mmoja wa Watanzania wasomi na wenye uzoefu mkubwa na aliyetoa mchango mkubwa kitaifa na kimataifa.  Hakuwa mzungumzaji sana kama ambavyo sisi wanasiasa tunategemewa kuwa.  Alizungumza pale tu ilipohitajika azungumze.  
Kwa wale tuliokuwa karibu naye tulishangazwa na kufurahishwa pia kwa majibu yake mafupi, sahihi na ya kifalsafa, ya maswali magumu.  Hakuna mtu ambaye angaliweza kuuliza imekuwaje Kigoda amekuwa Waziri, imekuwaje Kigoda amekuwa Mwenyekiti wa Kamati muhimu ya Bunge, au imekuwaje amekuwa Mbunge wa Handeni kwa muda mrefu.  

Alikuwa anafaa, alikuwa na uwezo na alikuwa anamudu majukumu yake.  
Kati ya mambo ambayo yalimnyima raha ni tatizo la maji Handeni.  Nathibitisha hilo. 

 Kwani katika kipindi chote nikiwa Waziri mwenye dhamana ya maji, hakuna siku ambayo tukikutana Bungeni, au katika Baraza la Mawaziri, ambapo hakuniuliza, kunikumbusha, au kunisisitizia kuhusu maji Handeni.  

Naamini waliofuata katika Wizara hiyo baada ya mimi kuhamishwa, wamefuatilia suala hilo na ahadi zetu kwake na wanatekeleza mpango wa maendeleo ya maji kuhusu Handeni.  Kama bado basi njia bora ya kumuenzi ni kutekeleza yale ambayo angependa kuyafanikisha alipokuwa hai.
Kwa kumalizia niwakumbushe tukio lililotokea wiki iliyopita la mitandao ya kijamii kutangaza au kama watakavyosema leo kifo kutabiri kifo chake.  Miaka kumi iliyopita yeye na mimi tulikuwa katika “timu” ya watu kumi na moja tulioomba ridhaa ya wana CCM ili mmoja wetu ateuliwe kuwa mgombea wa Chama katika ngazi ya Urais.  Kwa msemo wa kichama “Kura Hazikutosha”!  
Katika kutafuta wadhamini tulikutana Mtwara, yeye akitokea Lindi.  Taarifa zisizo rasmi lakini zilizagaa siku moja kabla zilihusu Dr. Kigoda kupoteza maisha!  
Mithili ya kukutana kwa Dr. David Livingstone na Henry Morton Stanley,Ujiji, Kigoma, nikamuuliza  “Bila shaka ni Dr. Kigoda”.  "Naam", akanijibu kwa kutabasamu.
  
Baada ya mazungumzo mafupi akasema, “nawafahamu walionizushia kifo, nimewasamehe”.  Sio hilo tu alilokutana nalo katika mchakato ule, bali kama alivyoniambia alikuwa "mhanga wa siasa za maji taka!”  Na waliomtakia kifo miaka kumi iliyopita! Msihofu.  Kwani moyo wake ulikuwa mkubwa.  Alishawasamehe.
Kwaheri Abdallah.  Kama utumishi wa nchi ni vita,  basi kama askari umepigana vilivyo.  Wakati wa kupumzika umewasili.  

Mwenyezi Mungu Airehemu Roho Yako.  Inna Lillahi wa Inna Ilahi Raji’un.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu