Wednesday, October 14, 2015

LHRC YAWAFUNDA WAGOMBEA WANAWAKE

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHRC, kimetoa mafunzo kwa wagombea wanawake na wenye ulemavu wanaowania nafasi za ubunge na udiwani nchini. Mafunzo hayo ya siku mbili ambayo yamekuwa na lengo la kuwawezesha wagombea hao kuzijua sheria za msingi za uchaguzi, haki za binadamu na matendo yanayoweza kusababisha uvunjifu wa sheria hizo na haki za binadamu yamefanyika nchi nzima kuanzia Octoba 12, 2015 na kumalizika Octoba 13, 2015.
Mgombea ubunge jimbo la Ubungo kwa tiketi ya chama cha TLP Mama GODLIVA MANUMBA akisoma tamko la wagombea wanawake na walemavu kwa wanahabari, kushoto kwake ni  mgombea ubunge wa jimbo la Ubungo kwa tiketi ya ACT-wazalendo Mama NYANJURA NYARINDO .

Wakizungumza kwa niaba ya wagombea wanawake wa nchi nzima, wagombea ubunge na udiwani wanawake na walemavu wa jiji la Dar es Salaam wametaja changamoto ambazo zinawarudisha nyuma kuwa ni pamoja na Vyama vya Siasa na Serikali kushindwa kuamini wanawake wagombea na kuwasaidia kifedha ili waweze kushiriki na kuwakilisha jamii katika mchakato wa uchaguzi na matumizi ya lugha za kejeli, matusi na mfumo dume pamoja na mawazo mgando toka kwa jamii dhidi ya wagombea wanawake.


Washiriki wakifuatilia mafunzo kwa umakini

Naye Afisa Programu wa Dawati la Jinsia na Watoto la LHRC amesema kuwa mafunzo hayo yanayofadhiliwa na Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa/UN - Women yameandaliwa kwa kusudi la kuwajengea wagombea hao uwezo wa kuweza kuendana na vuguvugu la uchaguzi lililopo nchini kwa sasa ukitofautisha na chaguzi zilizopita.  Aidha Naemy ameongeza kuwa mafunzo hayo yamelenga pia kuwapa ujasiri na mbinu mbadala wagombea wanawake na wagombea wenye ulemavu ili waweze kuibuka kidedea katika kinyang'anyiro cha Uchaguzi Mkuu 2015.

Afisa Programu wa Dawati la Jinsia na Watoto LHRC - Naemy Silayo akizungumza na wanahabari wakati wa mafunzo kwa wagombea wanawake na walemavu wa jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo LHRC imetoa rai kwa vyama vya siasa na vyombo vingine vianavyohusika ikiwemo Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutoa nafasi sawa na kipaumbele sawa kwa wagombea wanawake na wagombea wenye ulemavu kama inavyofanyika kwa wagombea wanaume.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu