Saturday, October 31, 2015

MATOKEO DARASA LA SABA HADHARANI

Na Mwandishi Wetu.

Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) leo limetangaza matokeo ya darasa la Saba iliyofanyika nchini kote kuanzia Septemba 2 hadi Septemba 10, mwaka huu ambapo watahiniwa 518, 034 kati ya 763, 602 waliofanya mitihani hiyo wamefaulu.

Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam leo, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dkt Charles Msonde amesema idadi ya watahiniwa waliofaulu ni sawa na asilimia 67.84, asilimia 10.85 zaidi ya ufaulu wa mwaka 2014 ambapo waliofaulu walikuwa asilimia 56.99.

Takwimu za matokeo hayo zinaonyesha, ufaulu katika masomo yote umepanda kwa asilimia kati ya 4.61 hadi 17.22 ikilinganishwa na mwaka 2014 huku watahiniwa wakifaulu zaidi somo la Kiswahili (77.20%) na kufaulu kwa kiwango cha chini katika somo la Kiingereza (48.56%).

Amesema kati ya watahiniwa wote waliofaulu 264, 130 ni wasichana ambao ni sawa na asilimia 64.60 ya wasichana wote 408, 900 waliotahiniwa huku wavulana wakiwa 253, 904 sawa na asilimia 71.58 ya wavulana 354, 706 waliotahiniwa.

Msondo amesema watahiniwa kumi bora wanatoka katika shule za Hazina iliyopo jijini Dar es Salaam, Mugini ya mkoani Mwanza na Twibhoki ya mkoani Mara huku wasichana 10 waliofanya vizuri wametoka shule za Mugini, Twibhoki na Little flower ya mkoani Mara.

Katika matokeo hayo, Waja Springs ya Geita imeongoza katika orodha ya shule kumi zilizofanya vizuri nchini, ikifuatiwa na Enyamai ya mkoani Mara katika nafasi ya pili, nafasi ya tatu inashikiliwa na shule ya msingi Twibhoki ya mkoani Mara.

Shule nyingine na nafasi ilizoshika kwenye mabano ni; Mugini ya Mwanza (4), Rocken Hill ya Shinyanga (5), Karume ya Kagera (6), Alliance ya Mwanza (7), Little Flower ya Mara (8), Palikas ya Shinyanga (9) na Mtakatifu Caroli ya Mwanza (10).

Kwa mujibu wa baraza hilo, shule ambazo hazikufanya vizuri katika matokeo hayo ni pamoja na Mwashigini ya Shinyanga, Mabambasi ya mkoani Simiyu, Mwangu iliyopo mkoani Lindi, Mohedagew ya mkoani Arusha na Kwale ya mkoani Pwani.

Zingine ni Njoro ya mkoani Arusha, Gomhungile ya mkoani Dodoma, Makole ya mkoani Tanga na Kitengu na Koloni za mkoani Morogoro.

Taarifa ya Necta inaonyesha kuwa mikoa 10 iliyofanya vizuri kwa ufaulu ni Katavi, Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Geita, Kagera, Tanga, Njombe na Iringa.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu