Thursday, October 8, 2015

MEFMI YAFANYA MAJADILIANO NA MAGAVANA WA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI NA KUSINI

Dr. Servacius Likwelile Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa serikali wa kwanza kushoto akiwa katika picha ya pamoja na Magavana wa Mashariki na Kusini mwa Afrika baada ya mkutano wa MEFMI (Picha na Eva Valerian, Peru – Lima).
---
Katika kipindi hiki cha mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa, kumekuwa na mikutano mbalimbali inaendelea hapa nchini Peru.

Mikutano hiyo inaendeshwa na Taasisi mbalimbali zenye utaalamu wa kiuchumi na kifedha. Akizungumza na waandishi wa habari, katibu Mkuu Wizara ya fedha Dr. Servacius Likwelile alisema “MEFMI ni chombo kikubwa kwa Afrika Mashariki na Kusini katika kutoa mafunzo ya usimamizi wa mambo ya uchumi kwa watendaji wa nchi wanachama.”

 Aliendelea kusema kuwa katika siku hizi mbili wamekutana na chombo hicho kwa madhumuni ya kuzungumzia maendeleo ambayo yanatokana na rasilimali kama vile gesi na madinii na kutoa mapendekezo ya namna gani Afrika inaweza kusimamia rasilimali hizo.

Akitoa ufafanuzi katika majadiliano hayo Dr. Likwelile alisema” Tanzania kuna rasilimali nyingi kama vile gesi ambayo imegunduliwa Mtwara na kusisitiza kuwa kuna nchi mbalimbali barani Afrika ambazo zina dhahabu ya kutosha ambayo inaweza kuinua uchumi wa Afrika kama kutakuwa na utaratibu mzuri wa kuzitumia.

“Lengo kuu la mkutano wa MEMFI ni kuzungumzia shughuli zinazofanywa na MEMFI ili kuwezesha kupanga namna ya kuboresha uwezo na kuendesha shughuli zetu katika kuinua uchumi wa Afrika kwani tutahitaji fedha nyingi kwa ajili ya kuwekeza kwenye miundombinu lakini lazima tuhakikishe kwamba tunafanya hivyo ili kuhakikisha uchumi wetu unakuwa imara na kunakuwa na utaratibu wa kuweka akiba kwa ajili ya vizazi vijavyo, hili ni suala la msingi sana” alisistiza Likwelile.

Likwelile aliongeza kuwa “Vizazi vingi vinatumia rasilimali zote bila kuangalia utaratibu wawakati ujao kuwa utakuwaje, hivyo katika kikao hiki tumekubaliana kuanzisha mfuko ambo ni kwa ajili ya kuwekeza kwa ajili ya matumizi ya baadae (Sovereign Wealth Fund). 

Masharti ya mfuko huoyatakuwa ni kama ifuatavyo: 
(i) Mfuko huo lazima uweze kuzalisha ajira, 
(ii) Mfuko huo lazima uwe na misingi imara ya kusimamia uendeshaji wa shughuli zake,
(iii) Mfuko lazima uwe na chombo imara kinacho kisimamia mfuko huo. 
(iv) Lazima kuwe na utaratibu ambao unasema mfuko huu utafanya nini na hautafanya nini.

La msingi kuwe na mfumo wa kisheria lakini tuangalie rasilimali watu ili kuweza kuhifadhi mfuko huo. Na namna gani miundombinu itawezakusaidia kuimarisha uchumi ili uweze kutambuliwa.”
Naye Gavana wa Benki kuu ya Tanzania Prof. Benno Ndulu alisema kuwa,ni muhimu kujua mapato yetu yatokanayo na upatikanaji wa madini kwani tunaweza kuyatumia vizuri katika kuhakikisha tunatengeneza miundombinu, kuongeza uwezo wa kuzalisha na baada ya hapo nchi iweze kuendelea kupiga hatua hata kama madini yatakuwa yamekwisha.

Waziri wa Fedha ni Gavana katika mikutano hii, akifuatiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dr. Servacius Likwelile ambaye ni Gavana msaidizi kwa upande wa Benki ya Dunia (WB), aidha Gavana wa Benki kuu Prof. Benno Ndulu ni Gavana msaidizi kwa upande wa Shirika la Fedha la Kimataifa(IMF).

Hali ya hewa mjini hapa ni baridi, rasharasha na manyunyu ya hapa na pale hasa nyakati za asubuhi.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu