Thursday, October 8, 2015

NIMRI KUFANYA KONGAMANO LA SAYANSI LA 29 KUANZIA OKTOBA 13-15, 2015

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI), Dk. Mwele Malecela akiongea na waandishi wa habari leo ofisini kwake kuwaelezea juu ya kongamano la Sayansi la 29 kuanzia Oktoba 13-15, 2015 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam. Pembeni yake ni Meneja Raslimali Watu, Bupe Ndelwa.
Waandishi wa habari wakifuatilia mkutano huo.
 ---
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu inapenda kutoa taarifa kuwa itafanya Kongamano lake la Sayansi la 29 kuanzia Oktoba 13-15, 2015 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam. Madhumuni ya Kongamano hili ni kuwakutanisha Watafiti, Watunga Sera, Watoa Maamuzi, Watoa huduma za afya, Wananchi na Wadau wengine wa Tafiti za Afya kutoka ndani na nje ya Tanzania ili kuwasilisha na kujadili matokeo ya tafiti mbalimbali kulingana na mada kuu ya Kongamano.

Ufunguzi rasmi wa Kongamano hilo utafanyika siku ya Jumanne tarehe 13 Oktoba 2015 saa 3.00 asubuhi. Mgeni rasmi katika ufunguzi huo tunategemea atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Pamoja na hotuba ya ufunguzi, mgeni rasmi atazindua maadhimisho ya miaka 35 ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu na Kumbukumbu za miaka 120 za utafiti wa afya Tanzania. Katika sherehe za ufunguzi, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu itamtunukia Mgeni Rasmi zawadi kwa ajili ya mchango wake mkubwa katika kukuza na kuthamini utafiti nchini Tanzania.

Mhesimiwa Mgeni Rasmi atatembelea Banda la Maonyesho ya utafiti ambako kumbukumbuza za kihistoria za utafiti wa afya tangu mwaka 1895 zitaoneshwa.

Zaidi ya washiriki 300 kutoka Tanzania na nchi mbalimbali duniani, zikiwemo Uganda, Cameroon, Kenya, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, India, Japan, Denmark, Switzerland, Uingereza, Kanada, na Marekani wamethibitisha kushiriki katika Kongamano hilo. Jumla ya mada 177 zitawasilishwa.

Mada kuu ya Kongamano ni: Uimarishaji wa afya na hali bora ya maisha kupitia tafiti zenye ubunifu: mpango wa kukabiiliana na kasi ya ongezeko la mseto wa magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza Barani Afrika. Katika Kongamano hili, mada mbalimbali zinazohusu magonjwa, athari za mazingira na vianishi vya kijamii, na mifumo ya utoaji huduma za afya zitawasilishwa, kujadiliwa na kutolewa mapendekezo ya hatua za kuchukua.

Mada zitakazojadiliwa zitalenga maeneo yafuatayo:

1. Tafiti za Magonjwa na Tiba
a) Kupambana na janga la magonjwa mseto ya kuambukiza na yasiyoambukiza katika nchi kusini mwa Jangwa la Sahara katika kipindi cha baada ya 2015
b) Tafiti na mikakati ya kudhibiti magonjwa ya kuambukia kusini mwa Jangwa la Afrika baada ya 2015
c) Shughuli za kiuchumi na milipuko ya magojwa mapya
d) Changamoto za upatikanaji wa chakula, lishe na magojwa yanayohusiana na maji
2. Mifumo ya Huduma za Afya
a) Afya kwa wote: uimarishaji wa mifumo ya huduma za afya na sera
b) Ekolojia ya Afya na Afya Moja: Mkakati mtambuka wa kudhibiti magonjwa
c) Matumizi ya tehema katika huduma za afya

3. Visababishi vya maradhi katika jamii
a) Afya ya mama na mtoto katika nchi kusini mwa Jangwa la Sahara
b) Matumizi ya matokeo ya tafiti katika kukabiliana na visababishi vya maradhi katika jamii
c) Shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabia nchi

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu