Taarifa zinasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju amewasilisha waraka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam akitaka kushikiliwa na kuzuiwa kwa mali zote za mtuhumiwa wa madawa ya kulevya, aliyejulikana kwa jina la Muharami Abdallah, maarufu kwa jina la Chonji na mkewe, Mwalibora Nyanguri kuhamisha umiliki, kupangisha au kuombea mikopo.

Maombi hayo dhidi ya Muharami na mkewe yaliwasilishwa kwa hati ya dharura mahakamani hapo Septemba 13, mwaka huu mbele ya Jaji Wilfred Dyansobela.

Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali ameiomba Mahakama hiyo imzuie Muharami, mawakala wake au mtu mwingine yeyote kwa niaba yake, kuhamisha umiliki wa mali, kupangisha nyumba au kuombea mikopo (ili serikali ifuatilie uhalali wa upatikanaji wa mali hizo).

Mahakama hiyo imetakiwa kutoa zuio hilo kwa nyumba sita za mtuhumishi zilizopo maeneo ya Magomeni, Tandale Ziota na Mbezi Juu jijini Dar es Salaam.

Nyumba hizo ni namba 95280 iliyopo Kiwanja Namba 43 Kitalu O, Namba 90292 iliyopo Kiwanja Namba 66 Kitalu P, nyumba iliyopo Kiwanja Namba 68 Kitalu X, nyumba yenye Mita ya Luku Namba 43001304757 na nyumba nyingine yenye Mita ya Luku Namba 04215118664.

Mali nyingine zilizowekewa zuio na kuwa chini ya serikali ni gari aina ya Mitsubishi Canter yenye namba za usajili T 376 BYY, Toyota Verossa yenye namba za usajili T 326 BXF na mali nyingine zote zenye jina au umiliki wa Kampuni ya Mumask Investment ambayo ipo chini ya mtuhumiwa huyo.

Katika maombi hayo, AG amemwomba Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na Ofisa Mtendaji wa Mtaa (husika) wasipitishe uhamishaji wa umiliki wa nyumba hizo na mahakama imwamuru Msajili wa Ardhi kutambua kwamba nyumba hizo zimewekewa pingamizi.

Maombi hayo kwa mara ya kwanza yalitajwa katika mahakama hiyo Novemba 12, mwaka huu ambapo mahakama iliamuru wadaiwa kuwasilisha hati kinzani Novemba 26 (leo) na AG atajibu Desemba 3, mwaka huu na maombi yatasikilizwa Desemba 4, mwaka huu.

Mtuhumiwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 50 ya mwaka 2014 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar ambapo anatuhumiwa kujihusisha na biashara haramu ya kusafirisha madawa ya kulevya yenye thamani ya shilingi 227, 374,500. Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi, Janet Kaluyenda.

Hata hivyo, katika Mahakama ya Kisutu kesi hiyo ilitajwa jana Novemba 25. Mtuhumiwa huyo anapelekwa mahakamani akitokea katika Gereza la Keko jijini Dar.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa akilifungua bunge mjini Dodoma, hivi karibuni, Rais John Pombe Magufuli, alikaririwa akisema amedhamiria kupambana na biashara haramu ya madawa ya kulevya ambapo alisema atashughulika zaidi na wauzaji badala ya watumiaji.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: