Friday, November 27, 2015

DC AAGIZA MUUGUZI ALIYEKAMATWA KWA WIZI WA DAWA SHINYANGA ASIMAMISHWE KAZI MARA MOJA


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza katika kituo cha afya cha Kambarage mjini Shinyanga ambapo pamoja na mambo mengine amemwagiza mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga kumsimamisha kazi muuguzi Joseph Nkila anayetuhumiwa kuiba dawa za serikali pamoja na msimamizi wa kituo hicho Dkt Nassoro Yahya kwa uzembe unaosababisha mwanya wa upotevu wa dawa katika kituo hicho na kusababisha wananchi kuilalamikia serikali kwa kukosa dawa wakati mkoa wa Shinyanga hauna tatizo la dawa
Mfamasia/mtunza dawa wa kituo cha afya Kambarage Seleman Hamza akitoa maelezo namna anavyofanya kazi katika kituo hicho ambayo hata hivyo mkuu wa wilaya hakuridhika nayo na kumwagiza yeye na msimamizi wa kituo waandae maelezo ya kina ndani ya siku 5
Mmoja wa wasamaria wema waliomkamata muuguzi anayedaiwa kuiba dawa akisimulia jinsi wizi wa dawa unavyofanyika katika kituo hicho na jinsi walivyomkamata Joseph Nkila.
Mkuu wa wilaya Josephine Matiro akiwa katika kituo cha afya Kambarage,nyuma yake ni katibu tawala wa wilaya ya Shinyanga Boniface Chambi na kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Sande Deogratius
Dawa zikiwa katika chumba cha kuhifadhia dawa cha Kituo 
Mfamasia/mtunza dawa wa kituo cha afya Kambarage Seleman Hamza akizungumzia kuhusu tukio la wizi wa dawa katika kituo hicho na changamoto ya dawa katika kituo hicho ambapo alisisitiza kuwa kuna baadhi ya dawa hazipo katika kituo hicho
Dawa zikiwa katika chumba cha kuhifadhia dawa kituo cha afya Kambarage 
Dawa katika kituo cha afya Kambarage
Mkuu wa wilaya Josephine Matiro na katibu tawala wa wilaya ya Shinyanga Boniface Chambi wakiwa katika chumba cha kuhifadhia dawa
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akitoka kwenye kituo cha afya Kambarage
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akitoa maelekezo kwa kaimu mganga mkuu wa manispaa ya Shinyanga Dkt Mhana Raphael(mwenye suti),kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Sande Deogratius na mfamasia wa manispaa ya Shinyanga Emmanuel Zabron
Mkuu wa wilaya Josephine Matiro akimpa maelekezo kaimu mganga mkuu wa manispaa ya Shinyanga Dkt Mhana.
---
Hapa Kazi tu ndiyo Tunaweza Kusema!! Novemba 26,2015 asubuhi..Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro anafanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha afya cha Kambarage katika manispaa ya Shinyanga ili kujionea hali halisi ya huduma zinazoendelea katika kituo hicho.

Kubwa zaidi lililomfikisha hapo asubuhi asubuhi ni kuhusu sakata la muuguzi wa kituo hicho Joseph Nkina kukamatwa na wananchi akiwa na dawa za serikali ikiwemo kopo moja la dawa aina ya paracetamol na chupa mbili za dawa ya maji aina ya Erythromycin kinyume na utaratibu.

Baada ya kukutana na uongozi wa kituo hicho na wananchi waliofanikisha kukamatwa kwa muuguzi mkunga wa kituo hicho Joseph Nkila amemwagiza mkurugenzi wa manispaa hiyo kumsimamisha kazi muuguzi huyo kuanzia leo Novemba 26,2015, ili kupisha uchunguzi wa tukio hilo.

“Nimekuja hapa kuona uhalisia wa jambo hili,Kuna ushihidi wa wazi kabisa kuwa muuguzi huyu kweli kaiba dawa za serikali,mbaya zaidi akataka kudanganya kwa kuchukua stakabadhi kutoka kwenye duka la dawa za binadamu (pharmacy), nimekutana na msimamizi wa kituo cha afya Kambarage na mfamasia anayetunza dawa,na kinachoonekana hapa ni uzembe kwenye uongozi kwani dawa zinatoka bila kufuatiliwa kuwa dawa hizo zinafanya nini”,amefafanua Matiro.

“Nitamshangaa sana hakimu atayepindisha kesi hii kwani ushahidi uko wazi kabisa kutoka kwa wananchi kwamba amekuwa akijihusisha na wizi kwa muda mrefu na kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu katika kituo hiki cha afya,wananchi wananyimwa dawa,kumbe watu wachache tu wanacheza mchezo huu mchafu wa kuiba dawa”,ameeleza Matiro.

“Kila siku wananchi wanalalamika hakuna dawa,lakini tumeangalia stoo tumekuta dawa zipo za kutosha na Shinyanga hatuna tatizo la dawa,dawa moja tu ambayo ni Antibiotic ndiyo haipo,na tumeagiza iletwe”,alieleza Matiro.

“Cha kusikitisha msimamizi wa kituo hiki Dkt Nassoro Yahya anasema hakuna upotevu wa dawa,huyu naye hatakiwi kuwa hapa kazi imemshinda,nimemwagiza mkurugenzi pia amsimamishe kazi kwani haiwezekani dawa zitoke kwenye kituo bila yeye kufahamu”,amesema Matiro.

Katika hatua nyingine Matiro amewashukuru na kuwapongeza wananchi waliofanikisha kumkamata muuguzi huyo na kuahidi kuwapa zawadi kwa kazi nzuri waliyofanya akiwataka wananchi wengine kuendelea kuwafichua watumishi wasiofanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi zao

Mkuu huyo wa wilaya ametoa onyo kwa muuguzi aliyekamatwa, ndugu na marafiki kuacha kutoa vitisho kwa wananchi waliokamata dawa hizo na kufanikisha juhudi za kukamatwa kwa muuguzi huyo kinyume na hapo hatua kali za kisheria zitachukulia dhidi yao.

Na Kadama Malunde- Malunde1 blog 

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu