Sunday, November 8, 2015

IKULU KUTAMU KWA NKURUNZIZA, KAGAME, KABILA BILA KUJUA MWISHO WA KIVULI CHAO

Kuna sura inayokinzana katika eneo la Afrika Mashariki na lile la Kati. Kuna wakati wanasiasa wanabisha kwenye eneo hilo. Pia, bado kuna mwangwi unaosukuma juu ya kile kinachoitwa ‘mabadiliko ya nyakati’.

Wote wanaozunguka eneo hilo wanavuta subira kujua hatma yake. Hata hivyo, kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda ni kama vile tayari amechochea gia. Anajiandaa kukoleza moto gari lake ili asonge mbele zaidi.

Inawezekana wakati huu anawatupia macho wenzake. Anaendelea kuwakodolea tena anawasimanga moyoni. Lakini bila shaka anaamini iko siku watafaulu na hatimaye kufuata mkondo wa kisiasa zake.
Wenzake wanaendelea kupingana kuanzia kwenye vikao vya Bunge hadi majukwaa ya wazi ya kisiasa.

Pia, wanaendelea kutumia mifumo ‘dhaifu’ ya kisheria kuendelea kupenyeza ushawishi wao. Wana kiu kubwa tena wanaendelea kuwajaza hamasa wananchi ili waendelea kusalia madarakani.
Mengi yanaendelea kujitokeza barani Afrika. Mathalani, Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), bado haamini kama atafaulu.

Jaribio lake la awali kulishawishi Bunge kubadilisha Katiba ili awanie muhula mwingine wa tatu wa uongozi lilizua mzozo mkubwa na hata kusababisha ‘vurumai na kujitokeza harufu ya kutoweka kwa amani’.

Jaribio hilo sasa ameliweka kando huku akiendelea kupima kina cha maji kwa kijiti.

Wale wanaomjua wanasema kuwa Rais Kabila anachanga upya karata zake. Wanasema huenda akaibuka ‘kivingine’.

Wanasisitiza kuwa Rais Kabila bado hajakata tamaa tena anasukumwa na kile kilichojitokeza kwa Rais Kagame. Rais Kagame ameidhinishwa na Bunge kuendelea kuwania madaraka kwa muhula mwingine wa miaka saba.

Pia, kuna wale wanaamini kuwa, Rais Kabika inawezekana yupo kwenye tafakuli kubwa.

Wanaamini kuwa huenda kiongozi huyo akabadilisha mchezo na kuwashinda wapinzani wake kwa kutumia ‘mkakati mgumu’ uliotumiwa na Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi.

Licha ya kuwa mazingira ya kisiasa kwa nchi hizo mbili yanabeba sura mbili zinazotofautiana lakini siasa hupenda kuazima matukio. Siasa ni harakati ya kuhodhi madaraka. Daima siasa ni mchezo wa kuwinda dola. Inavyoonekana Rais Kabila shauku yake kubwa ni kufuata mkondo wa jirani yake Rais Kagame.

Rais Kagame amefunguliwa mlango kuendelea kusalia madarakani. Bunge limeidhinisha marekebisho ya Katiba na hivyo kumpa fungua wa kuendelea kukalia kiti cha ‘enzi’ kwa utawala wa Rwanda.
Wenyewe Rwanda wanamsifu wakisema ni kiongozi aliyebeba ‘mkono wa chuma’.
Rais Pierre Nkurunziza amejitwalia funguo. Amewapiga chenga wapinzani wake na kuendelea kushikilia ufunguo wa kusalia madarakani. Licha ya kuandamwa na shinikizo kutoka nyumbani hadi katika duru za kimataifa, Rais Nkurunziza hakusita kuendelea na mkakati wake. Aliusuka mpango na kisha kuutekeleza na sasa anaushikilia.
Analaumiwa na kushutumiwa na wengi. Anakosolewa tena anabanwa na wakubwa wa magharibi.
Hata hivyo, amepuuza hayo yote na kuendelea na kile kinachotajwa na wengi ‘ umwamba wa baadhi ya viongozi wa Afrika kusalia madarakani kwa kupindisha katiba zao’.
Tayari ameanza kuonja kile wengi wanakiita joto la jiwe. Mkoloni wake wa zamani, Ubelgiji ilikuwa nchi ya kwanza kuuadhibu utawala wake.
Ubelgiji imesitisha baadhi ya misaada ya maendeleo huku ukionya kuchukua hatua zaidi katika siku za karibuni iwapo ukandamizaji kwa makundi ya wapinzani utaendelea.
Marekani imefuata mkondo. Rais Barack Obama ametangaza kuing’oa Burundi kutoka kwenye mikataba yake ya kibiashara ya AGOA inayoyawezesha mataifa ya Afrika kuingiza bidhaa zao katika soko la nchi hiyo bila ya kulipa kodi.
Mpango huo uliasisiwa wakati wa utawala wa Rais Bill Clinton anayetajwa ndiye aliyefufua upya uhusiano wa karibu baina ya mataifa ya Afrika na Marekani.
Rais Obama ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa mstari wa mbele kuwakosoa viongozi wa Afrika wanaong’ang’ania kubakia madarakani, alisema amechukua hatua hiyo baada ya kushuhudia kushuka kwa viwango vya demokrasia katika taifa hilo.
Jinamizi la utamu wa madarakani bado linaendelea kuzunguka. Rais Kagame amefaulu kunyosha mstari tena kwa wananchi wake.
Hata hivyo, wapinzani wake wanalalamika kwa kile wanadai kuandamwa na vitisho na wakati mwingine kuwa hatarini kuuawa.
Ingawa amefaulu kushika ufunguo wa kuendelea kusalia Ikulu kwa mkono wa umma, lakini kivuli cha mwisho wake bado kinatawaliwa na chenga. Wengi wanaona kuwa, Rais Kagame ‘amejitengenezea’ maadui wengi kuliko ilivyotarajiwa.
Hali kama hiyo inaanza kulinyemelea taifa la Congo Brazzaville ambako Rais Denis Sassou Nguesso ambaye wakati fulani alipewa sifa kubwa kutokana mchango wake wa kusaidia kutatua migogoro ya Afrika. Inaelezwa kuwa kwa sasa kiongozi huyo anageuka kinyonga.
Ameanzisha mkakati wa kubadilisha Katiba ya nchi hiyo ili awanie urais katika muhula mwingine wa tatu.
Hata hivyo anakabiliwa na upinzani mkali, lakini mwenyewe anasisitiza kuwa lazima ajenda yake ipate uungwaji mkono.
Japokuwa kila mwanasiasa huja na mwonekano wake, lakini kwa walio wengi wanahisi kuwa viongozi hao wanajaribu kucheza kwenye utelezi mkali huku wakiwa wamevalia suruali yenye msumari pembeni.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu