Tuesday, November 17, 2015

MATIBABU YA BURE KWA WAKAZI WA KEREGE

 Klabu ya Rotary ya Dar es Salaam Oyster Bay, kwa mara nyingine tena, imeandaa kambi ya matibabu ya bure. Kambi hiyo ilifanyika siku ya Jumapili Novemba 15, 2015 ambapo zaidi ya wahudumu 50 wa afya walipima na kutibu magonjwa kwa wakazi zaidi ya elfu moja Kerege wilayani Bagamoyo.
Kambi hiyo ilifunguliwa saa mbili asubuhi na kuisha saa kumi jioni ambapo wakina mama wajawazito na wazee walipewa kipaumbele cha kuhudumiwa haraka. Wataalamu wa afya walifanya vipimo vya magonjwa mbalimbali kama vile malaria, upungufu wa damu, kisukari na shinikizo la damu. Vipimo vyote na matibabu vilitolewa bure na ilipobidi, wagonjwa walipewa rufaa kwenda hospitali kwa matibabu zaidi.
Kambi hiyo pia ilitoa matibabu ya ngozi, meno na upimaji wa macho na kutoa miwani za bure kwa wenye matatizo ya macho. Upimaji wa saratani ya kizazi na saratani ya matiti pia ulifanyika pamoja na upimaji wa hiari wa VVU, ushauri nasaha na elimu juu ya suala la UKIMWI. Kama ilivyofanyika miaka iliyopita, elimu ya kinga dhidi ya malaria pamoja na vyandarua vya bure vilitolewa.

Wakina mama wajawazito walipewa ushauri pamoja na vifaa vya kujifungulia. Wataalamu wa afya pia walitoa ushauri kuhusu mitindo ya maisha kama vile lishe na umuhimu wa kufanya mazoezi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Leena Kapadia, Mratibu za Kambi hiyo alisema, “Lengo la kambi hiii ni kutoa huduma za msingi kwa watu ambao kwa kawaida hawapati matibabu kwa urahisi. Kambi hii inaweza kuwa ndio wakati wa pekee ambao wanakijiji hawa wanapata fursa ya kumuona daktari, tunahisi kuwa tuna wajibu wa kuwapatia matibabu ya magonjwa yanayowasumbua na kuwapa rufaa ya kwenda hospitali inapobidi.”

Kambi ya Matibabu ilidhaminiwa na Diamond Trust Bank na Rotary Club of Seattle 4 na iliandaliwa kwa kushirikiana na Shree Hindu Mandal Hospital, Vital Supplies, Kidz Care Tanzania, Elite Dental Clinic, Whitedent, Sayona, Ultimate Security, The Living room furniture na VClick Concepts.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu