MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imewafikisha mahakamani watu wanne, wakiwemo ndugu, kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uongo.

Taarifa hizo wanadaiwa kuzitoa kwa lengo la kuupotosha umma katika kipindi cha uchaguzi ulimalizika Oktoba 25, mwaka huu, kupitia mtandao wa Whatsapp na kundi la kijamii liitwalo Soka.

Watuhumiwa hao, Leila Sinare (36), Godfrey Soka (45), Deo Soka (40) na Monica Soka (32), wakazi wa Dar es Salaam, walifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Leila na wenzake walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Cyprian Mkeha na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali Wankyo Simon akishirikiana na Wakili wa Serikali Mkuu kutoka TCRA, Johannes Kalungura.

Simon alidai shitaka la kwanza linamkabili Leila peke yake, ambapo anadaiwa tarehe tofauti kati ya Oktoba 20 na 30, mwaka huu, sehemu isiyojulikana jijini Dar es Salaam, alisambaza taarifa za uongo kwa njia ya sauti kupitia mtandao wa Whatsapp.

Alidai mshitakiwa huyo alisambaza ujumbe usemao: “Ndugu zangu wa kigango cha siasa, hakuna kutakiana uchaguzi mwema wala nini. Nchi yetu inaingia kwenye machafuko muda wowote kuanzia sasa hivi ni kama tulivyoambiwa kwamba nchi itageuka kuwa nchi ya vita ni kweli imeingia kwenye vita.

“Maboksi yenye kura feki yamekamatwa Jimbo la Vunjo yamekamatwa maboksi matatu, tumekamata maboksi matatu feki Moshi Mjini, maboksi sita Ilemela, maboksi 12 Hanang.”

“Kwa kifupi uchaguzi umeshavurugika na Tanga nasikia magari yamesimama sehemu makamanda zetu bado wanaendelea kufuatilia lakini inasemekana ni maboksi ya kura na mpaka sasa hivi hali siyo nzuri CCM wameingiza kura nyingi feki, na niseme kutokana na hali halisi ambayo ipo hatuponi,” ujumbe ulidai.

Uliendelea kudai kuwa: “Hatuponi kwa sababu Mwanza vijana vimeshaanza kuuawa, wameshakufa vijana wanne, watano mpaka sasa hali hiyo inaendelea. CCM jamani tunaomba mtuachie nchi kwa amani, kweli ingelipaswa kutuua angalau kwa sumu mkabaki wenyewe, msitutese msitutese.”

Simon alidai ujumbe huo ulikuwa na lengo la kuupotosha umma kipindi cha uchaguzi mkuu mwaka huu.

Godfrey, Deo na Monica, wanadaiwa katika kipindi hicho jijini Dar es Salaam, waliusambaza ujumbe huo wa njia ya sauti kupitia kundi la mawasiliano liitwalo Soka.

Washitakiwa hao walikana shitaka hilo, ambapo Simon alidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.

Hakimu Mkeha alitoa masharti ya dhamana kwa kuwataka kila mshitakiwa kutia saini dhamana ya sh. milioni tano na kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika atakayetia saini dhamana ya kiasi hicho.

Washitakiwa hao waliweza kutimiza masharti hayo ya dhamana, hivyo kuachiwa kwa dhamana hadi Desemba 3, mwaka huu, kesi itakapotajwa.

Akizungumza nje ya mahakama, Kalungura alitoa onyo kwa watu wanaotumia mitandao vibaya kwa kusema kwamba TCRA iko macho hivyo wanaofanya hayo watafikishwa mahakamani.

Alitoa rai kwa wananchi kwamba wasisambaze taarifa wasizo na uhakiki nao na bila ya kuwa na chanzo chake.

Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Charles Kenyela, alitoa onyo kali kwa mtu yoyote atakayesambaza habari za uongo na za uzushi.

Kenyela alitoa wito kwa wazazi kuendelea kuwasihi vijana wao waache kujiingiza katika makundi na kutoa habari zisizo sahihi kwa kuwa mwisho wa siku wataishia kukamatwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: