Tuesday, November 3, 2015

WATU SITA WAPOTEZA MAISHA MKOANI SINGIDA

RPC
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, ACP. Thobias Sedoyeka akiongea na waandishi wa habari Mkoani Singida alipokuwa akitoa taarifa za matukio ya mauaji ya watu sita Mkoani hapa.
SAM_0038
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mukhola, kata ya Mgori wakiwa katika safari ya kumtafuta mtu aliyewauwa wanawake wawili akiwemo mtalaka wake kwa kugombea mashamba.
Na Jumbe Ismailly, Singida.
WATU sita wamefariki dunia na mtu mmoja kujeruhiwa katika matukio manne tofauti yaliyotokea Mkoani Singida kati ya Okt,31 na Nov,01,mwaka huu.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Singida, ACP.Thobias Sedoyeka alifafanua kwamba matukio hayo yalitokea katika Vijiji vya Kintanula, wilayani Manyoni, kata ya Kindai, katika Manispaa ya Singida, Kijiji cha Kinyamwambo, kata ya Merya Singida vijijini na Kijiji cha Kamenyanga, wilayani Manyoni.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na ACP. Sedoyeka zimesema kuwa katika tukio la kwanza lililotokea okt,31,mwaka huu saa 2:30 usiku watu watano wasiofahamika wakiwa na mapanga walivamia nyumbani kwa Giganza Ntejo (61) na kumuua Hollo Hoye(57) kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali kichwani pamoja na kumjeruhi mwenye nyumba huyo.
Alibainisha kamanda huyo kwamba wakati Giganza akiwa amelala usiku na mwanamke huyo anayesadikiwa kuwa ni mke wake na kuanza kuwashambulia wote wawili na kisha kutokomea kusikojulikana.
Hata hivyo msemaji huyo wa jeshi alisema wakati wa purukashani waliovamiwa walikuwa wanapiga kelele za kuomba msaada ambapo majirani walifika na kukuta mwanamke huyo ameshafariki na mwanaume akiwa hoi kwa kujeruhiwa na ndipo waliwapeleka katika zahanati ya Kijiji na uchunguzi unaonyesha kuwa kifo cha marehemu kilitokana na kuvuja damu nyingi kutokana na jeraha alilolipata.
“Aidha uchunguzi wa awali wa polisi unaonyesha kuwa sababu za tukio hilo ni kisasi cha mapenzi baada ya mwanaume kuishi na mke huyo ilihali awali alikuwa ameolewa na mwanaume mwingine huko Kishapu, Mkoani Shinyanga”alisisitiza.
Katika tukio la pili lililotokea pia Okt, 31 saa mbili usiku kwenye mtaa wa Kibaoni, Manispaa ya Singida, Samweli Ezekieli (39) mkazi wa eneo hiloa nasadikiwa kuuawa na baba yake mzazi aitwaye Ezekieli Kiimu (60) kwa kupigwa na kukabwa shingoni.
Hata hivyo katika tukio la tatu lililotokea Nov,01,mwaka huu saa tisa alasiri katika Kijiji cha Kinyamwambo, kata ya Merya,wilaya ya Singida, Mustapha Saidi (47) mkazi wa Kijiji cha Kihunadi aliuawa na wananchi wenye hasira kali baada ya yeye kuwaua wanawake wawili kutokana na migogoro ya mashamba.
Kamanda huyo hata hivyo aliweka wazi kuwa katika tukio la nne lililotokea pia Nov,01,mwaka huu saa 12:00 jioni katika Kijiji cha Kamenyanga,wilayani Manyoni,mwendesha pikipiki Emmanueli Moses (43) mkazi wa Kijiji cha Samaria alifariki dunia baada ya kuanguka na pikipiki aliyokuwa akiiendesha.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu