Wednesday, November 18, 2015

WATU WAWILI WASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA TUHUMA ZA KUTAKA KUSAFIRISHA KOBE HAI 201

Jeshi la Polisi Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), limewakamata watu wawili kwa tuhuma za kutaka kusafirisha kobe hai 201 wenye thamani ya Sh30.4 milioni waliokuwa kwenye soksi kwenda Kaula Lumpa, Malaysia.

Kamanda wa Polisi JNIA, Martin Otieno aliwataja waliokamatwa kuwa ni mkazi wa Kariakoo, David Muungi (36) na mkazi wa Kidongo Chekundu Zanzibar, Mohamed Suleiman Mohamed (43).

Otieno alisema kobe hao aina ya Indian Star, waliwekwa watatu hadi sita ndani ya soksi na kisha kwenye pampasi kubwa ndani ya mabegi matano.

Alisema ufungaji huo ulifanyika ili kwenye mashine ya ukaguzi isijulikane kilichomo ndani ya mabegi hayo.

Kamanda Otieno alisema mizigo hiyo ilipofika katika eneo la uchambuzi juzi saa 4.30 usiku, kikosi kazi kiliyatilia shaka mabegi hayo yaliyokuwa yakisafirishwa kwenda chini Malaysia kupitia Dubai kuwa huenda yakawa na nyara za Serikali.

Otieno alisema juhudi zilifanyika ili kuwatambua wamiliki wa mabegi hayo na walikamatwa na baadaye kufikishwa Kituo cha Polisi cha Uwanja huo kwa ajili ya upekuzi.
“Watuhumiwa hawa walikamatwa katika eneo la ukaguzi wa mwisho wa abiria na kupelekwa kwenye eneo la uchambuzi wa mizigo na waliyatambua mabegi yao,” alisema Otieno.

Watuhumiwa hao walipohojiwa na polisi walidai kobe hao waliwatoa Visiwa vya Comoro na Ushelisheli lakini polisi wanahisi hawakutoka huko, bali mwambao wa Pwani.

“Tulipoendelea kuwahoji walidai wanampelekea mteja wao anayeishi Kaula Lumpa ambaye jina lake hatuwezi kulitaja kutokana na upelelezi unaoendelea,” alisema Otieno.

Februari 27, mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar, polisi walikamata kobe wadogo 250 wakitaka kusafirishwa kwa njia ya magendo kwenda Malaysia.

Juni 24, kwenye Uwanja wa JNIA polisi pia walimkamata raia wa Kuwait, Hussein Mansoor akiwa na kobe 173 aliokuwa akiwasafirisha kuelekea nchini kwake.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu