Wednesday, December 16, 2015

BEI YA MENO YA TEMBO YAANGUKA NCHINI CHINA

Pamoja na kupanda kwa bei za pembe za ndovu kuanzia mwaka 2010 kufikia mwaka 2014, thamani ya meno ya tembo imeshuka kwa kiasi kubwa nchini China jambo ambalo ni habari njema kwa Tanzania katika harakati zake kukomesha ujangili wa pembe za ndovu.

Taarifa mpya ya utafiti uliofanywa na watafiti Esmond Martin na Lucy Vigne wa shirika la Save the Elephants na kutolewa wiki hii imeainisha kwamba bei za meno ya tembo ghafi nchini China zimeshuka kwa zaidi ya nusu katika kipindi cha miezi 18 iliyopita kutoka dola za Marekani 2,100 kwa kilo moja hadi kufikia dola 1,100.

Katika utafiti wao uliofanya katika majiji nane nchini, watafiti hao wamegundua kwamba mahitaji ya meno ya tembo na bidhaa zitokanazo na pembe za ndovu yanaendelea kushuka kwa kasi kubwa kuliko ilivyowahi kutokea. Viwanda vinavyotengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na pembe za ndovu vimeripoti kuwepo na uhaba wa pembe za ndovu na vibali vinavyotolewa na serikali kuwaruhusu wafanyabiashara kuuza pembe za ndovu kihalali vimecheleweshwa.

Matokeo ya utafiti huu mpya yanaenda sanjari na ongezeko kubwa la uelewa wa watu nchini China ambapo sasa sehemu kubwa ya jamii inaelewa madhara ya tatizo la ujangili kwa tembo wa Afrika na uelewa huu umeongezeka maradufu kati ya mwaka 2012 na 2014 kwa mujibu wa taarifa ya Wildaid, Save the Elephants na African Wildlife Foundation. Wakati hali hii ikijitokeza, serikali ya China imepiga hatua kubwa katika kudhibiti soko la pembe za ndovu tangu mwezi Septemba ambapo Rais wa nchi hiyo Xi Jinping alitangaza kwamba China na Marekani zitashirikiana kukomesha biashara ya pembe za ndovu.

Akizungumza kuhusu utafiti huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Wildaid, Peter Knights amesema: “Kuanguka kwa bei ya pembe za ndovu nchini China ni habari nzuri tuliyotaka kusikia japo bado kuna kazi kubwa hii ni hatua muhimu sana katika kukomesha janga la ujangili. Kupigwa marufuku biashara hii nchini China na Marekani vitatoa shinikizo kwa Hong Kong, Thailand na Japan nazo kupiga marufuku biashara hii. Pia hii itazipa moyo nchi za Kenya na Tanzania kuendelea kupambana na ujangili.”

Tangu mwaka 2012, mashirika ya WildAid, Save the Elephants na African Wildlife Foundation yaliungana kufanya kazi ya uhamasishaji juu ya ujangili nchini China kwa kuwatumia watu maarufu nchini humo kama Yao Ming mcheza mpira wa kikapu NBA zamani na muigizaji Li Bingbing ambao kupitia matangazo mbalimbali wamekuwa wakihamasisha jamii kuacha kununua, kugawa au kupokea pembe za ndovu kama zawadi.

Mashirika makubwa ya habari nchini China ya CCTV na Xinhua nayo yametoa msaada mkubwa katika jitihada hizi kwa kutoa matangazo yenye thamani ya dola za Marekani milioni 42 bure ambapo matangazo hayo yamewafikia mamilioni ya wananchi wa China. Vilevile jitihada hizi pia zimesaidiwa na Mwanamfalme wa Uingereza Prince William ambaye alitoa hotuba ya kihistoria mwezi Oktoba na kuwaomba wananchi wa China kukataa kabisa biashara ya pembe za ndovu.

Akizungumza kuhusu anguko hilo la bei ya meno ya tembo Balozi wa WildAid Jacqueline Mengi amesema: "Upunguaji wa mahitaji ya pembe za ndovu huko nchini China ni ishara kwamba jitihada za Wildaid pamoja na serikali za nchi tofauti zinaendelea kuzaa matunda. Mwaka jana tulizindua kampeni maalum ya kuongeza ufahamu na kuielimisha jamii kuhusu tatizo la ujangili linaloikabili Tanzania. Kwa matokeo ya utafiti huu ni dhahiri kwamba mwamko wa kulinda tembo wetu umeongezeka.”

Mashirika ya WildAid, African Wildlife Foundation na Save the Elephants yamekuwa yakiipa shinikizo kubwa Hong Kong nchi inayodaiwa kuwa kituo kikubwa cha biashara hiyo duniani. Baada ya mashirika hayo hivi karibuni kutoa filamu iliyochukuliwa kwa siri ikionyesha jinsi ambavyo Hong Kong imeshindwa kudhibiti biashara hiyo haramu, maafisa wa serikali hiyo wameonyesha dalili za kuwa tayari kukomesha biashara hiyo jambo ambalo linaungwa mkono na Baraza a Sheria la Hong Kong.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu