Wednesday, December 9, 2015

MADIWANI WA HALMASHAURI YA MJI NJOMBE WAPATIWA MAFUNZO YA UONGOZI BORA

Mtaalamu Kutoka Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Anton Palangyo akizungumza na Waheshimiwa Madiwani (hawapo pichani) kuhusiana na maswala ya Maadili ya Viongozi.Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Njombe Ngd Gualbert Mbujilo akifuatiwa na Afisa Serikali za Mtaa Mkoa wa Njombe.
Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Mji Njombe wakiwa kwenye Mafunzo ya Uongozi kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe.
---
Madiwani wa Halmashauri ya Mji Njombe wamepatiwa mafunzo juu ya maswala ya Uongozi Bora na Kupiga vita vitendo vya Rushwa pindi wanapokuwa kwenye majukumu yao ya Uongozi.

Akifungua Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe, Mtaalamu kutoka TAKUKURU Ndugu Charles Nakembetwa alianza kwa kuwaeleza maana nzima ya Uongozi, kwamba Uongozi ni kujua Dhamana, Dira na Mustakabali wa jamii na baada ya Kujua Dira ni jukumu la Kiongozi kukaa mbele na kuiongoza jamii.

Akizungumza katika Mafunzo hayo, Mtaalamu huyo alisema kuwa Viongozi wengi wanageuza maana ya uongozi na kuona kama uongozi ni kutumikiwa, kuabudiwa na ndio maana matukio ya kuomba rushwa yanaripotiwa mara kwa mara.

‘Viongozi wengi hawawatembelei watu kwenye Maeneo yao na kuishi kwa kuwa mfano wa jamii wanayoiongoza. Wengi wamekuwa ni Wabaguzi na Wamekosa uwajibikaji kitu ambacho ni kinyume na dhana nzima ya Uongozi.’’Alisema Ndugu Charles Nakembetwa.

Vile vile amewasisitiza Madiwani hao kuwa TAKUKURU ni chombo cha Kuelimisha na Kuhamasisha Viongozi kushiriki kikamilifu juu ya upambanaji wa maswala ya rushwa, na wasisite kuripoti taarifa zozote zile zinazohusiana na maswala ya rushwa ndani ya Halmashauri.

Nae Mtaalamu Kutoka Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Ndg. Anton Palangyo amewataka Madiwani hao wafuate maadili ya Uongozi na kutambua kama watakayokuwa wanafanya ni sahihi au sio Sahihi, na pindi wanapogundua kuwa sio sahihi wajisahihishe ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Baadhi wa Madiwani waliohudhuria mafunzo hayo wamesema kuwa, Mafunzo hayo yamewajengea uwezo na kuwaongezea ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kazi.

Mafunzo hayo yameendeshwa na Mtaalamu kutoka TAKUKURU, Mtaalamu kutoka Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Afisa Serikali za Mitaa Mkoa wa Njombe, Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Njombe, na Mwanasheria wa Halmashauri ya Mji Njombe.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu