Monday, December 28, 2015

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO

download (14)
Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo inapenda kuujulisha Umma kwamba kumekuwapo na upotoshwaji unaondelea katika mitandao ya kijamii hususan facebook, Instagram na WhatsApp ambapo sehemu ya upotoshaji huo imenukuliwa kama ifuatavyo “Wizara imetoa tamko kuwa kuanzia januari 2016 mavazi yote yasiyo stahiki ambayo hayaendani na mila na desturi zetu Wizara yangu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitafumbia macho mavazi hayo.

HAYARUHUSIWI KUVALIWA SEHEMU ZIFUATAZO
  1. Kwenye masoko makubwa
  2. Hospitali kubwa(Private or Public)
  3. Maofisini na Vyuoni
  4. Mijini kwenye mikusanyiko ya watu wengi
Hatua kali za kisheria zitachukuliwa endapo kwa wale ambao watavaa mavazi haya ikiambatana na faini ya sh. 100,000/=” mwisho wa kunukuu.
Tunachukua fursa hii kukanusha vikali taarifa hizo kuwa siyo za kweli na kwamba mhusika amefanya uhalifu wa kimtandao kwa kuaanda taarifa yake ya uongo na kuibandika katika uso wa Tovuti ya Wizara yenye anuani: www.habari.go.tz kwa lengo la kuipotosha jamii.
Kufuatia uharifu huo Serikali inatoa onyo kali na haitawavumilia wale wote wanaokiuka misingi ya sheria ya mtandao ya mwaka 2015 ambayo inakataza kusambaza taarifa za uongo na haitasita kuwafikisha katika vyombo vya sheria wale wote watakaobainika kufanya uharifu huo.
Pamoja na upotoshaji huo wa makusudi napenda pia kutumia wasaa huu kuwakumbusha watumishi wa umma na jamii yote kwa ujumla kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma inao Waraka wa Utumishi wa Umma Na. 3 wa mwaka 2007 kuhusu mavazi kwa watumishi wa Umma. Waraka huo umeainisha mavazi ambayo hayafai kuvaliwa katika ofisi za umma kwa wanawake na wanaume; aidha umeelekeza aina za mitindo ya nywele isiyofaa pamoja na aina za viatu visivyofaa.
Mifano ya mavazi yasiyokubalika kwa watumishi wa umma wanawake ni kama vile nguo zinazobana, nguo fupi ambazo zinaacha magoti wazi, nguo ambazo zinaacha sehemu ya mwili wazi kama vile kitovu na kifua, nguo ambazo zina picha, michoro, na maandishi ambayo hayaendani na shughuli za Serikali, kaptura aina yoyote ile kama vile pedo na pensi, nguo zinazoonyesha maungo ya mwili (transparent), suruali za ‘Jeans’, na nguo zingine zote zenye kukinzana na maadili ya utumishi wa umma na jamii kwa ujumla.
Aidha, kwa upande wa wanaume mavazi yasiyokubalika ni pamoja na nguo ambazo ni za kazi maalum kama vile michezo (hizi zivaliwe wakati wa shughuli hiyo tu), nguo ambazo zina michoro, maandishi na picha ambazo haziendani na shughuli za Serikali, nguo zinazobana, kaptura ya aina yoyote, suruali yoyote inayoachwa bila kupindwa, suruali za “Jeans” na Fulana “T-shirts” (Hizi zivaliwe tu wakati wa shughuli maalum inayotambulika), Kikoi au msuli, nguo zenye maandishi ya chama chochote cha siasa na yenye kuonyesha ushabiki wa kitu fulani.
Pamoja na kuwepo kwa miongozo ya mavazi yanayostahili kwa watumishi wa umma, tafsiri ya mavazi ya heshima hutegemea mila na desturi ya jamii husika.

​Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,​
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu