Monday, December 28, 2015

WATENDAJI NA WENYEVITI WA VIJIJI WAMETAKIWA KUACHANA NA IMANI POTOFU KUHUSU MATUMIZI YA VIRUTUBISHI

Mtaalamu wa Lishe kutoka Wizara ya Afya Ndg. Peter Kaswahili akiwaonesha Watendaji Mfuko wenye virutubishi ambavyo huongezwa kwenye unga wa mahindi kwenye mashine za kusagia
Ndugu Kaswahili akionesha nembo ya bidhaa ambazo zimeongezwa virutubishi kwenye mfuko wa unga wa mahindi.
Baadhi ya Watendaji na Wenyeviti wakiwa kwenye Picha ya Pamoja na Wataalamu wa Lishe.

Imeandaliwa Na,
Afisa Habari Halmashauri ya Mji Njombe.
---
Rai hiyo imetolewa katika mafunzo yaliyofanyika kwa wenyeviti na watendaji wa Vijiji kutoka Halmashauri ya Mji Njombe kwenye Mafunzo ya kuwajengea uelewa kuhusiana na Matumizi bora ya Virutubishi.

Akifungua mafunzo hayo Mtaalamu wa Lishe kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Ndg. Peter Kaswahili ameseme kuwa inasikitisha sana kuona baadhi ya viongozi wakiwa mstari wa mbele kupinga matumizi ya virutubishi kwa Wananchi wao licha ya elimu ya mara kwa mara ambayo imekuwa ikitolewa.

“Tumeitana Kama viongozi kwani tunashuhuda kuwa kuna baadhi ya maeneo wenyeviti au Watendaji wamekuwa Ni kikwazo, Watoa huduma vituoni wanahamasisha matumizi ya virutubishi lakini kiongozi katika jamii anaenda kumfuata na kusema kuwa hivi Virutubishi ni vya Freemason na mnataka kupunguza nguvu za kiume” Alisema ndugu Kaswahili.

Dhana hii ni potofu na si kweli kwani hamna tafiti iyoonesha kuwa matumizi ya virutubishi yamechangia kupunguza nguvu za kiume. Hivyo ni jukumu letu sisi kama Viongozi kuwaelimisha wananchi wetu na kuwahamasisha juu ya matumizi ya virutubishi kwenye vyakula.

Imeelezwa kuwa katika siku 1000 za kwanza, kwa maana siku ya kwanza tangu mimba inapotungwa mpaka mtoto kufikia umri wa miaka miwili matumizi ya virutubishi ni muhimu kwa mama mjamzito na kwa mtoto atakayezaliwa kwani itasaidia afya njema ya mama na mtoto virutubishi vitasaidia kuimarisha ukuaji wa akili (ubongo) kwa mtoto.

Akitolea ufafanuzi juu ya upatikanaji wa virutubishi ndugu Kaswahili amesema kuwa kuna virutubishi ambavyo huchanganywa kwenye uji wa mtoto na hupewa kwa mtoto mwenye umri wa kuanzia miezi sita na kuendelea na hupatikana katika vituo vya afya kwa shilingi mia moja kwa kila pakiti, na vingine hupatikana kwenye mashine za kusagia nafaka kama mahindi na huchanganywa pamoja kwenye unga kwa ujazo tofauti tofauti.

Nae Afisa Lishe kutoka Halmashauri ya Mji Njombe Bi. Bertha Nyigu amesema kuwa mpango huo haujafika kwa bahati mbaya kwenye vijiji hivyo, kwani kutokana na tafiti iliyofanyika mwaka jana kuhusiana na maswala ya afya na lishe imeonesha kuwa Mkoa wa Njombe umeongoza kwa asilimia 52 ya idadi ya watoto wenye tatizo la udumavu. Huku mikoa inayoongoza ikiwa ni Mkoa wa Njombe, Iringa na Mbeya.

Akitolea ufafanuzi wa hali ya lishe ilivyo katika Halmashauri ya Mji Njombe Afisa Lishe wa Halmashauri hiyo amesema kuwa kwa mwaka 2014 jumla ya watoto 45 walilazwa katika hospitali ya Kibena wakiwa na tatizo la Lishe na Watoto 11 kati yao walipoteza maisha ambayo ni sawa na asilimia (20.4), wakati kwa mwaka 2015 kuanzia mwezi January hadi November idadi ya watoto waliolazwa imeongezeka hadi kufikia 66 na kati yao 07 walipoteza maisha ambayo ni sawa na asilimia (10.6)

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO) linataka kutokuwepo kabisa na linapinga vikali vifo vya watoto vinavyosababishwa na matatizo ya utapiamlo na hata ikitokea iwe chini ya asilimia tano (5%).

Vilevile ameongeza kuwa tatizo la Uchafu wa mwili na mazingira unasababisha mlipuko wa magonjwa ya Kuhara na Kutapika naUchafu pekee unachangia asilimia 15% ya ongezeko wa tatizo la Utapiamlo.Hivyo amewataka viongozi hao kuendelea kutoa elimu ya afya ya mwili na kutunza mazingira kwa wananchi.

Baadhi ya Watendaji na Wenyeviti waliohudhuria mafunzo hayo wamefurahishwa na Elimu hiyo iliyotolewa na wamekiri kuhusika kwa namna moja au nyingine kuwa vikwazo juu ya program hiyo ya ugawaji wa Virutubishi kutokana na Ukosefu wa Elimu; lakini sasa Mafunzo hayo yamewasaidia kuwajengea uwezo kuhusiana na maswala ya Virutubishi na watakua Wahamasishaji wakubwa wa Matumizi ya Virutubishi kwa Wananchi Wao na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu