Tuesday, January 19, 2016

RAIS DKT JOHN POMBE MAGUFULI AKUTANA NA BALOZI WA ISRAEL NCHINI IKULU LEO

Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akipeana mikono na Balozi wa Israeli nchini Mhe Yahel Vilan alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo January 19, 2016
Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiongea na Balozi wa Israeli nchini Mhe Yahel Vilan alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo January 19, 2016.
---
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemhakikishia Waziri Mkuu wa Israel kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari kushirikiana na kuimarisha zaidi mahusiano kati ya Tanzania na Israel katika nyanja mbalimbali ili kuleta manufaa kwa pande zote.

Rais Magufuli amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Israel hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Nairobi - Kenya Mheshimiwa Yahel Vilan, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

"Natambua mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na Israel, mahusiano haya ni muhimu sana kwa ustawi wa nchi zetu mbili, nataka mahusiano haya yaimarishwe zaidi " Alisema Dkt. Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli ameahidi kuwa Tanzania itahakikisha inaanzisha ubalozi wake nchini Israel haraka iwezekanavyo.

Kwa upande wake Balozi wa Israel hapa nchini Mheshimiwa Yahel Vilan pamoja na kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na uongozi wake katika kipindi kifupi cha miezi miwili tangu aingie madarakani amemhakikishia kuwa Israel itaendelea kushirikiana na Tanzania na ipo tayari kuimarisha zaidi mahusiano.

Balozi Vilan ametaja baadhi ya maeneo ya ushirikiano kiuchumi kuwa ni pamoja na Kilimo, Maji, Ufugaji wa Nyuki na Sayansi na Teknolojia huku akibainisha kuwa Israel imewaalika Jumuiya ya wafanyabiashara wa Tanzania kushiriki katika Kongamano la biashara kati ya Tanzania na Israel litakalofanyika Mjini Tel Aviv nchini Israel, mwezi Septemba mwaka huu.

Balozi Vilan pia ameahidi kufikisha ujumbe wa Rais Magufuli kwa Waziri Mkuu wa Israel Mheshimiwa Benjamin Netanyahu na pia ameahidi kuanzisha ofisi ya kutoa huduma ya visa hapa nchini haraka iwezekanavyo.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU. 
Dar es salaam.
19 Januari, 2016

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu