Tuesday, January 5, 2016

WANASIASA WAKWAMISHA SHUGHULI ZA URAGHABISHI WILAYA YA SHINYANGA VIJIJINI

Mchungaji wa kanisa la Umoja wa Makanisa ya Ubatizo  Lucas Machibya akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani ) kuhusu baadhi ya shughuli za uraghabishi katika kijiji cha Pandagichiza
---
Na Krantz Mwantepele, Shinyanga.

Si mara nyingi viongozi wa kidini hujihusisha moja kwa moja na harakati za kisiasa ila wamekuwa mstari wa mbele kukemea matendo yanayofanywa na wanasiasa. Hawafanyi hivyo kwa bahati mbaya ila kutokana na nafasi yao katika jamii, hususani kuwaongoza waumini wao kwenda mbinguni.

Hata hivyo, hii haimaanishi hakuna kabisa viongozi wa dini waioamua kujiingiza katika harakati za siasa ili kuleta maendeleo ya watu kwa haraka na ufanisi. Mchungaji Lucas Machibya ni mmoja kati ya viongozi wachache wa dini wanaoingia katika siasa.

Huyu ni mchungaji wa kanisa la Umoja wa Makanisa ya Ubatizo lililopo katika kijiji
cha Pandagichiza chenye wakazi wanaokadiriwa 2,481, idadi kubwa ikiwa ni ya wanawake wanaokadiriwa kufikia 1,476. Hiki ni moja ya vijiji vilivyopo wilaya ya Shinyanga Vijijini, jimbo la Solwa.

Machibya ni mmoja wa wachungaji waraghbishi toka mkoa wa Shinyanga ambao uraghbishi wao umepelekea wananchi kumchagua kuwa mwenyekiti wa kijiji. Kujibainisha kwake kama mtu mwenye uwezo wa kusimamia anachokiamini na kushawishi wananchi kutambua majukumu na haki zao na jinsi ya kuzidai vimekuwa nguzo yake kubwa ya kukubalika. 


Kama walivyo wananchi wengi wa kijiji chake, yeye ni mkulima mdogo ambaye pia ni mwanachama wa Mtandao wa Wakulima Wadogo Tanzania (MVIWATA). Kupitia mwaliko wa mkulima mwenzake, Elizabeth Edward, Machibya amefanikiwa kupata maarifa ya uraghbishi na jinsi ya kufanya uraghbishi; uwezo wa kuwashawishi na kuwahusisha ama kuwachokoza watu ili waweze kujitambua na kutojiona wao ni wa jamii ya chini. Sifa iliyomfanya aalikwe kwenye mafunzo ya uraghbishi ni uwezo wake wa kuhoji mambo mbalimbali pasipo kukata tamaa kama anavyosema mwenyewe:


“Mimi ni mtu wa kuhoji vitu na si mtu wa kuridhika ama kukaa kimya n’napoona kuna jambo sijalielewa. Kwa kweli yale mafunzo yalinifanya kujiona mtu tofauti sana nikijilinganisha na nilivyokuwa awali. Nilijihisi tayari nimekuwa mtaalamu wa masuala ya uwajibikaji na utawala bora.”

Kwa kuwa wao ni wakulima, walianza uraghbishi wao kwa kutaka kujua nini kinaendelea kuhusu bei ya pamba. mchungaji Machibya anaeleza ilivyokuwa:


“Kule tulifundishwa jinsi ya kuuliza maswali. Na cha kwanza tulichotaka kujua ni kwa nini bei ya zao letu la pamba imeshuka sana. Hili tuliliuliza sisi sote, mimi na waraghbishi wengine.”

Hawakuishia hapo tu bali wakaanza pia kufuatilia mapato na matumizi ya fedha za kijiji toka kwa viongozi wao. Walifanya hivyo kwa kuwatembelea ofisini na kuomba kupatiwa taarifa hizo na pia walitaka kufanyika mikutano ya hadhara. Baada ya harakati hizo kushika kasi, iliwabidi waongeze watu wengine zaidi kwa kuwatembelea majumbani kwao na kuwaraghbisha.

“Mchungaji aliomba kunitembelea nyumbani na alipofika alinipatia elimu. Kimsingi, alitaka nijitambue kwa kujua wajibu na haki zangu. Alinitaka nisiogope kuuliza maswali kwenye mikutano kwa kuwa tuna uhuru wa kufanya hivyo. Nikajua kuwa nina wajibu kuuliza na kujua mapato ya fedha za kijiji na na matumizi yake kuwa hiyo ni haki yangu,” anaeleza Bw. Daudi Denis toka kijiji cha Pandagichiza.
Baadhi ya waraghabishi wa kijiji cha Pandagichiza wakiwa na waandishi wa habari za mtandaoni katika moja ya jengo la jiko  la shule ya msingi Pandagichiza ambalo limetoakana na juhudi zao za uraghabishi 
Kufanikisha haya yote kumewajengea uaminifu mkubwa sana waraghbishi na baadhi yao wamekuwa wakishirikishwa katika vikao muhimu vya maendeleo na serikali yao ya kijiji. Baadhi yao wametokea kuaminika zaidi na jamii kiasi cha kuombwa wagombee nyadhifa mbalimbali za uongozi wa serikali na ndani ya vyama vya siasa kama ilivyokuwa kwa mchungaji Machibya.

Hivyo basi, waraghbishi wengi wanaojihusisha na siasa wamejikuta wakinasa katika mtego huu wa migogoro ya kimaslahi kati ya shughuli zao za uraghbishi na zile za kisiasa kwa kuchukiwa na baadhi ya watu wanaotofautiana kimlengo wa kisiasa na kuonekana wasaliti na watu wasiokuwa na misimamo.

Wakati mwingine wanachukiwa ikidhaniwa kuhoji kwao mara kwa mara ni njia ya kujitafutia mtaji wa kisiasa na si kuwatumikia wananchi na kuibua maovu kwa maslahi ya jamii nzima na kwamba uraghbishi unawanufaisha wao binafsi na vyama vyao tu.
Uraghbishi ulimuingiza mchungaji Machibya kwenye mgogoro mkubwa na walinzi wa jadi, Sungusungu. Katika maeneo mengi ya Kanda ya Ziwa walinzi hawa wamekuwa na nguvu kubwa na wakati mwingine wanaweza kutoa adhabu kali kwa yeyote anayebainika kutenda kosa. 

Tofauti hiyo na Sungusungu ilisababisha yeye na waraghbishi wengine sita kukamatwa na kutozwa faini ya shilingi laki tano na elfu sitini (560,000/=) kwa mpigo kwa kisingizio cha kuvuruga amani katika kijiji hicho. Hii ni kwa sababu tu walikuwa wanauliza maswali kuhusu mapato yanayotokana na faini na michango mingine toka kwa wanakijiji. 

Vitisho na maonyo ya uongozi viliwapunguza kasi baadhi ya waraghbishi na kuingiwa hofu kiwa wangefikishwa pabaya zaidi ya hapo. Ila mchungaji Machibya hakuishia hapo bali aliendelea na shughuli hizo kama kawaida. Baadaye aliteuliwa kuwa katibu wa mtandao wa waraghbishi na huko ndiko alikojizolea uaminifu na umaarufu zaidi baada ya kuanza kujihusisha na kuhoji mambo makubwa ya kiutawala na utendaji kijijini hapo. 

Hiyo ilimwongezea hamasa ya kuendelea kuwatumikia watu kwa kuongeza juhudi katika shughuli za uraghbishaji na kufikia hatua ya kuombwa na wananchi kugombea wadhifa kichama (siasa) na uongozi katika serikali ya kijiji.

Na mwaka 2014 wakati wa mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa ukiendele, ndipo yeye alijikita kwa dhati kuomba nafasi ya kugombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kufanikiwa kuteuliwa kugombea. Akielezea ilivyokuwa, mchungaji Machibya anasema:

“Wapinzani wangu walipojua kwamba mimi ndio nimepitishwa waliamua kujitoa katika vyama vyao na kuniunga mkono. Hii kwa sababu hawakuona sababu ya kupingana nami kwa kuwa wanafahamu uwezo na umakini wangu kiutendaji na kiuwajibikaji.”

Matokeo ya harakati hizo ni kwamba Mchungaji Machibya alichaguliwa kwa kishindo kuwa mwenyekiti wa kijiji na baadaye alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa wenyeviti wa wilaya nzima. Sanjari na nafasi mwenyekiti wa kijiji, aliendelea pia kushika nyadhifa nyingine ikiwamo kuwa mraghbishi kiongozi na mchungaji.
Hizi ni nyadhifa nyingi zinazoambatana na majukumu mengi kwa mchungaji Machibya hivyo kujikuta kwenye mazingira magumu sana ya kutumikia nyadhifa zote. Lakini pia alipata upinzani mkali sana kutoka kwa viongozi wengine na hata wakati mwingine kushindwa kusimamia kwa pamoja majukumu yote.

Huku ni mraghbishi na huku ni mwenyekiti wa kijiji. Hii haikuwa changamoto ndogo kwake. Akifafanua hilo, mchungaji Machibya anasema: “Kwa sababu nilikuwa kiongozi wa waragbishi ilikuwa ni kama nayajua maswali kabla ya mtihani na wenzangu walikuwa wanashindwa kuhoji vizuri kwa kuwa mie ni kiongozi wao. Ndipo nikaamua kujitoa uongozi na kuwa mraghbishi wa kawaida, lakini sikuishia hapo nikajivua na majukumu ya uchungaji wa kanisa japo ni shughuli niliyoipenda sana na kuwa mzee wa kanisa kawaida.”

Kwa haraka haraka, unaweza kusema shughuli ya kuhoji mwenzio inafanana na kuhojiwa wewe binafsi. Mwanzoni alipata ugumu kidogo kwa sababu kila mwananchi alikuwa anategemea mabadiliko ya haraka wakati vitu vingine vilikuwa kimfumo zaidi. Hiyo ilimfanya achelewe kutoa majibu ya haraka. Na ili asiangukie kwenye dimbwi la lawama, alihakikisha anakuwa muwazi kwa wananchi na viongozi wake wa karibu katika kila jambo.
Kuna mbinu kadhaa alizotumia ikiwa ni pamoja na kuteua viongozi wa halmashauli ya kijiji wanaoendana na falsafa yake ya uwazi na uwajibikaji na pia aliendelea kuwatumia waragbishi wenzake katika kuibua mambo pale alipohisi yanakwama. Mchungaji Machibya anafahamu kwamba yeye kama kiongozi ana wajibu wa kuwa na uelewa wa mambo mbalimbali ikiwemo sheria na sera za nchi. Kwa kuelewa hilo, alipoanza kutafuta fursa za mafunzo ya uongozi na kukutana na mashirika mbalimbali yaliomwezesha kupata elimu. 

Hakuishia hapo bali aliendelea kujenga mizizi ya waraghbishi wengi zaidi na mpaka sasa amefanikiwa kuwajengea uwezo wenyeviti wenzake 40 kati ya 126 wa wilaya nzima, na bado anaendelea kutafuta maarifa mengine ili awape wenzake.

Kwa nafasi yake, anatafuta wadau na mashirika yenye ujuzi huo ili awezeshe wenyeviti wote kupata mafunzo kwani wengi wao wanatawala wananchi kimazoea tu. Hawana ufahamu wa namna nzuri ya kutekeleza majukumu yao.
Kwa misingi hiyo, mchungaji Machibya ameamua kutumia uraghbishi kama nyenzo ya kumuongezea ufanisi katika majukumu yake na si kutengeneza uadui na waragbishi kama ilivyo kwa viongozi wengi wa vyama na serikali. Kwa mfano huu, tunapata picha halisi ni kwa namna gani uragbishi ukichukuliwa kwa mtazamo chanya unakuwa nyenzo muhimu ya kuongeza chachu ya utawala bora katika serikali zetu za mitaa, kijiji na taifa kwa ujumla. Na kwa sasa, anapambana na mambo makuu matano ikiwa ni pamoja na mradi wa maji utakaomwezesha kukusanya kiasi cha shilingi 500,000.

Pamoja na mapato mengine yanayokusanywa na Sungusungu pamoja na kuhamasisha kusomeshwaji kwa wingi kwa watoto wa kike. Na tayari hatua za makusudi za kuhakikisha kwamba malengo ya kuongeza mapato na hivyo kulipia watoto wa kike kuhudhuria shuleni zimeshachukuliwa.

Hii ikiwa ni pamoja kupunguza adhabu kali za viboko, kuunda upya uongozi wa Sungusungu. Kwa upande wa mapato, wameweka mikakati ya wazi ya kuhakikisha mapato yanayopatikana yanasomwa mbele ya wananchi. Kwa upande wa shule, kila mzazi na jamii nzima imeandaliwa mikakati ya makusudi kuwawajibisha wale wote wanaoshindwa kuwapeleka watoto wa kike. Waraghbishi wamekuwa chachu kubwa katika uvumbuaji wa taarifa pamoja na uelimishaji pia.

Jambo la kwanza kwa kiongozi yeyote anayetaka mafanikio katika uongozi wake ni kutanguliza maslahi ya wananchi kwanza kabla ya maslahi binafsi au ya chama chake. Kinyume na hivyo anaweza kutia doa hata huo uraghbishi wake. Utu wa mtu hupimwa kwa matendo yake na hata mtazamo wa watu anaowaongoza.

Viongozi wengi wanatumia uraghbishi kama nyenzo ya kujijengea umaarufu wakati wenyewe ni kama hulka ama tabia ya mtu kupenda haki na mambo yakiwa yanasonga. Kwa hiyo unaweza kukuta waraghbishi wengi sana kama matendo yako yatalenga kukomboa watu na si maslahi binafsi.

Jambo lingine ambalo alisisitiza ni kwamba hawa viongozi wawe na utamaduni wa kutafuta maarifa na si kusubiri fursa za kuletewa tu na wahisani. Kiongozi bora ni lazima aendane na mabadiliko ya kila siku na si kuongoza watu kwa mazoea. Binadamu wanabadilika kila siku, hivyo kuna umuhimu wa kuonesha tofauti kati ya kiongozi mraghbishi na wa kawaida. Hiyo itaibua mwamko mkubwa wa viongozi wengi kuwa waraghbishi.
Kiongozi asiyejua sheria na sera za nchi ni sawa na kipofu. Siri ya elimu na ufahamu ipo kwenye maandishi, mafunzoni na kwenye semina elekezi kwani bila kufanya hivyo utauchukia uraghbishi.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu