Saturday, January 30, 2016

WAZIRI MKUU MAJALIWA KASSIM MAJALIWA KUSHIRIKI IBADA YA KUMUINGIZA KAZINI ASKOFU MKUU WA KANISA LA KIINJILI LA KILUTHELI TANZANIA (KKKT) MJINI MOSH


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makala akizungumza  na wanahabari ofisini kwake kuhusu ugeni wa Waziri mkuu ,Majaliwa Kassim Majaliwa mkoani Kilimanjaro.
Baadhi ya wanahabari wa mkoa wa Kilimanjaro wakimsikiliza Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Amosi Makala alipozungumza nao ofisini kwake.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda
ya Kaskazini.


WAZIRI mkuu, Majaliwa Kassimu Majaliwa, leo  anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ibada maalum ya kumuingiza kazini askofu mkuu wa kanisa la kiinjili la kiluteri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Frederick Shoo katika kanisa kuu la Moshi mjini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla,amesema waziri mkuu anatarajiwa kuwasili  mkoani Kilimanjaro kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ambapo atapokea taarifa ya mkoa kabla ya kufanya shughuli za kanisa.

Alisema waziri mkuu hataongozana na waziri yeyote wa serikali ya awamu ya tano bali wasaidizi wake na baada ya ziara hiyo maalum atarejea Dodoma kuendelea na shughuli za serikali.

Ibada hiyo maalumu itajumuisha viongozi mbalimbali wa serikali ndani na nje ya mkoa wa Kilimanjaro sanjari na viongozi wa madhehebu tofauti ya dini, wadau wa maendeleo, waumini na wananchi kwa ujumla.

Kutokana na ujio huo wa waziri mkuu, mkuu wa mkoa, aliwataka wananchi hususani katika wilaya za Hai na Moshi kujitokeza kwa wingi kumpokea kiongozi huyo ambaye pia atapokea changamoto mbalimbali zinazoukabili mkoa.

Kadhalika waziri mkuu anatarajiwa kutoa maelekezo ya serikali kulingana na changamoto zitakazojitokeza wakati anapewa taarifa ya mkoa.

Dk Shoo ambaye pia ni askofu wa dayosisi ya Kaskazini amechaguliwa kuongoza kanisa hilo kwa miaka minne na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na mtangulizi wake askofu Dk Alex Malasusa ambaye amemaliza muda wake wa uongozi.


Askofu Dk Shoo alichaguliwa mapema mwezi Agosti mwaka jana katika mkutano mkuu wa 19 wa kanisa hilo uliofanyika chuo kikuu cha Tumaini jijini Arusha baada ya kuwashinda wenzake wawili.

Uchaguzi wa nafasi hiyo  uliwashindanisha askofu Dk Stephen Munga wa dayosisi Kaskazini Mashariki na Askofu Charles Mjema
wa dayosisi ya Pare.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu