NA RAISA SAIDI, BUMBULI.

SERIKALI ya Tanzania imevunja rasmi mkataba na mwekezaji wakiwanda cha kuzalisha Chai cha Mponde kilichopo wilayani Bumbuli Mkoani Tanga na kuamuru kitwaliwe na kianze kazi mara moja.

Akizungumza katika mkutano uliowajumuisha wadau wazao la chai, Msajili wa Hazina Laurence Mafuru amesema kuwa kwa mamlaka aliyopewa amevunja rasmi mkataba huo kwasababu Mwekezaji aliyekuwepo kashindwa kutekeleza makubaliano yaliyoweka .
 Mafuru alisema kuwa wamefikia uwamuzi huo kutokana na kujiridhisha pamoja na kupitia mikataba walioingia na mwekezaji huyo ndipo serikali imeamua ikirudishe kiwanda hicho mikononi mwa Wizara ya Viwanda na Biashara ili utaratibu mpya wa uendeshwaji wa kiwanda uanze huku Bodi ya Chai Tanzania ukiendelea kukisimamia mpaka hapo serikali itakapotafuta mwekezaji mwingine.

Mei mwaka 2013, wakulima wa chai waliitisha mkutano na kumwalika Mbunge wa Jimbo la Bumbuli Januari Makamba na kueleza kutokuwa na imani na mwekezaji na Chama cha Wakulima wa Chai cha Usambara (UTEGA) na kuamua kukifunga kiwanda licha ya Mbunge kuwasihi wasichukue uamuzi huo wa hasira.

Tangu wakati huo jitihada nyingi zimefanyika zikiongozwa na Mheshimiwa Makamba kuhakikisha kwamba kiwanda kinafunguliwa na wakulima wanauza chai yao.

‘’Tuliteseka kwa muda mrefu na leo Serikali imefanya uamuzi wa kukirudisha kiwanda mikononi mwetu, Tunaishukuru Serikali kwa kutusaidia sisi wananchi tulioteseka kwa muda mrefu ,” Alisema Challes Ngovi ambaye ni mkulima wa chai Mponde.

Hata hivyo Mafuru alibainisha kuwa ucheleweshaji wa kukifungua kiwanda hicho ulitokana na utaratibu uliokuwa ukifanywa na Serikali na baada ya kujiridhisha ndipo ikaamua kumuandikia rasmi barua Mwenyekiti wa Utega inayoonyesha kuvunjwa kwa mkataba huo na kuamuru kiwanda kirudi Serikalini.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bumbuli January Makamba alisema kwamba kazi waliyomtuma wananchi ya kukirudisha kiwanda mikononi mwao imekamilika ingawa imechukua muda mrefu.

Makamba ambaye pia ni Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughuliokia Mazingira na Muungano alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Magufuli kwa kuingilia kati mgogoro huo ambao umedumu kwa zaidi miaka mitatu na hatimae kuumaliza.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Umoja wa Wakulima wa Chai Usambara UTEGAWilliam Shelukindo aliilaumu serikali kutoka na uamuzi wake wa kukitaifisha kiwanda hicho bila ya kutoa nafasi kwa mwekezaji kuweza kujitetea kwani ni ameshindwa kuzalisha.

“Serikali katika hili imeshindwa kutupa nafasi ya kujitetea ili kuweza kujua sababu za kushindwa kuzalisha ,lakini kwa sasa hatuna cha kufanya zaidi ya kutekeleza matakwa yao”alisema Shelukindo.

Ambapo Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mwantumu Mahiza alisema kuwa siku 90 za kupeleka malalamiko na utetezi kwa seriklai zilishatangazwaa na kumalizika kilichobaki ni utekelezaji wa kanuni na taratibu za serikali kukichukuwa kiwanda na kuanza uzalishaji.

“Niwaombe wananchi hakikisheni mnazalisha zao hilo kwa wingi ili kiwanda kiweze kufanyakazi na kuboresha uchumi wa kila mmoja wenu,wilaya,mkoa na taifa kwa ujumla kwani Bumbuli mnategemea zao la chai kwa kiasi kikubwa.

Wakati huo huo,Wananchi waishio maeneo mbalimbali katika Jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Tanga wamempongeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira kwa hatua ya kuwasaidia kuishawishi serikali kukipatia ufumbuzi mgogoro wa kiwanda cha chai cha Mponde.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi, mmoja ya wakulima hao,Swahiba Mbili alisema kuwa kufunguliwa utawasaidia wananchi ambao walikuwa na changamoto ya mazao yao kuharibika shambani kupata soko la uhakika ambalo linaweza kuwainua kimaisha.

Swahiba alisema kuwa wao kama wakulima pamoja na kuishukuru serikali kutwaa kiwanda lakini wanamshukuru Januari Makamba kwa sababu hakuweza kuwa mbali nao kwenye kipindi chote wakati kiwanda hicho kimefungwa na kuaidi kumpa ushirikiano katika kipindi cha kuwatumikia wananchi hao.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: