Tuesday, March 8, 2016

MAALIM SEIF SHARIF HAMAD AZUNGUMZIA HALI YA AFYA YAKE

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na waandishi wa habari katika hospitali ya Hindu Mandal Jijini Dar es Salaam kuelezea maendeleo ya afya yake. Amesema anaendelea vyema baada ya jana kuugua ghafla na kulazwa katika hospitali hiyo. Amewashukuru wananchi ndani na nje ya nchi kwa kuonesha mapenzi na mashirikiano makubwa. Anatarajiwa kutoka hospitalini hapo leo jioni (Picha na Salmin Said, OMKR)
---
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amezungumza na waandishi wa habari katika hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam, na kusema kuwa hali ya afya yake inaendelea vizuri.

Maalim Seif ametoa taarifa hiyo kufuatia kuugua ghafla jana asubuhi na kukimbizwa katika hospitali hiyo, ambapo alilazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Daktari wa Maalim Seif aliyeambatana naye akiwa Dar es Salaam Dkt Omar Mohd Suleiman amesema tatizo kubwa lililomkabili kiongozi huyo ni machofu aliyokuwa nayo baada ya kutokea safarini nchini India Ijumaa iliyopita.

Amesema alilazimika kulazwa hospitali hapo ili kupata uangalizi wa karibu na kupumzika, na kwamba afya yake inaendelea vizuri na anatarajiwa kutolewa hospitalini hapo leo jioni.

Maalim Seif aliugua ghafla jana asubuhi akiwa safarini kuelekea Dar es Salaam, hali iliyopelekea kukimbizwa hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu