Sunday, April 3, 2016

RAIS DKT. MAGUFULI ACHANGIA SHILINGI MILIONI 10 UPANUZI WA KANISA CHATO

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
NEMBO YA TAIFA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa Mchango wa Shilingi Milioni 10 kwa Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato Mkoani Geita kwa ajili kuchagia upanuzi wa kanisa hilo.

Fedha hizo zimekabidhiwa na Kaimu Mnikulu Bw. Ngusa Samike katika misa ya pili ya ibada ya Jumapili ya pili ya Pasaka, iliyofanyika kanisani hapo leo tarehe 03 April, 2016.

Kabla ya misa hiyo ya pili Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli wakiwa pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Mheshimiwa Raila Amoro Odinga na Mkewe Mama Ida Odinga, walisali misa ya kwanza ambapo Rais Magufuli aliahidi kuchangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya upanuzi wa kanisa hilo ambao unaendelea.

Katika Misa hiyo Paroko wa Parokia ya Chato, Padre Henry Mulinganisa alieleza kuwa kanisa hilo linatarajia kuadhimisha miaka 50 ya tangu kuanzishwa kwake baadaye mwaka huu, na kwamba maadhimisho hayo yanakwenda sambamba na upanuzi wa kanisa ambao unachangiwa na waumini wenyewe.

Padre Mulinganisa amemshukuru Rais Magufuli kwa mchango huo, na amemuahidi kuwa utatumika vizuri ili uendeleze upanuzi wa kanisa hilo pamoja na michango ya waumini wengine.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Chato
03 April, 2016

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu