Wednesday, April 13, 2016

UCHUKUZI SC YATOKA SARE 1-1 NA AMADORY BOYS

TIMU ya soka ya Uchukuzi Sports Club mwishoni mwa wiki ilitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Amadori Boys ya Pugu Sekondari katika mchezo wa kirafiki uliofanyika jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Uchukuzi Sports Club inajiandaa kwa mashindano ya Mei Mosi yatakayoanza Aprili 16 mkoani Dodoma, ambapo mechi hiyo ni ya pili ya majaribio baada ya ile ya kwanza iliyofanyika hivi karibuni.

Katika mchezo huo, Uchukuzi SC ndio walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Isack Ibrahim katika dakika ya saba kabla ya Christian Moyo hajasawazisha mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Hatahivyo, Ibrahim alikosa magoli kadhaa ya wazi, baada ya walinzi wa Amadory Boys kumkaba baada ya kuona ni tishio langoni mwao.

Meneja wa Uchukuzi SC, Robert Damian aliyewahi kuichezea Simba ya Jijini Dar es Salaam, alisema kuwa mechi hizo za kirafiki zinawasaidia makocha wa timu yao kujua makosa ya wachezaji wao na kuyarekebisha kabla ya kwenda kwenye kituo cha mashindano, ili waweze kufanya vizuri.
Alitamba kuwa timu yao ya soka pamoja na nyingine za netiboli, kuvuta kamba, riadha, bao, drafti na vishale zitafanya vizuri katika mashindano hayo ya Mei Mosi kwani zimejiandaa vizuri, kwa kupata mechi kadhaa za kirafiki.

Aidha, timu ya netiboli ya Uchukuzi SC juzi ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Bandari Kurasini huku ikiwa na wachezaji wake wakongwe kama akina Matalena Mhagama, Subira Jumanne, Fanuna na wengineo, ambao wanaipa nguvu timu hiyo chini ya kocha wao mzoefu Judith Ilunda.

Timu ya Uchukuzi SC katika mashindano yaliyopita ya Mei Mosi yaliyofanyika jijini Mwanza, iliweza kutwaa makombe 13, kati ya hayo matano ni ya ubingwa katika michezo ya kuvuta kamba, baiskeli, bao, karata na riadha kwa upande wa wanawake na wanaume, wakati yaliyosalia ilishika nafasi ya pili na tatu.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu