Wednesday, May 11, 2016

AFISA UTUMISHI MANISPAA YA ILALA ASIMAMISHWA KAZI

Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda, akizungumza na wakuu wa idara mbalimbali wa mkoa huo kuhusu kubainika kwa watumishi hewa wengine 39. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,Ally Hapi na Mkuu wa Wilaya ya Temeke,Sophia Mjema. Picha zote na Elisa Shunda
---
JUMLA ya watumishi hewa wengine 39 wamebainika katika Mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni wiki moja tangu Mkuu wa Mkoa wa huo, Paul Makonda, kuwasainisha mikataba wakuu wa idara zote kuhusiana na watumishi hao. 

Imeelezwa kuwa hadi sasa watumishi hewa 248 wamebainika mkoani hapa na kuisababibishia serikali hasara ya takriban Sh.bilioni 3.6. 

Akizungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwemo maofisa utumishi, wakuu wa idara, wakurugenzi na wakuu wa wilaya jana jijini hapa, Makonda alisema watumishi hao 39 wameisababishia serikali hasara ya Sh. milioni 724.

Kufuatia sakata hilo, Makonda alimwagiza mkurugenzi wa Ilala, Isaya Mngurumi, kumwandikia barua ya kumsimamisha kazi Ofisa Utumishi wa manispaa hiyo, Francis Kilawe, kutokana na kubainika watumishi hewa 11 ambao licha ya kutoonekana katika idara zao, waliendelea kulipwa mishahara.

Alisema ili taifa liweze kupiga hatua, kila mmoja kwa nafasi aliyonayo hana budi kufanya kazi kwa bidii kumsaidia Rais John Magufuli katika kuhakikisha kuwa maendeleo yanapatikana.

Hata hivyo, akizungumzia suala hilo baada ya mkutano huo kuisha, Mngurumi alisema atamuomba Makonda kutengua adhabu ya ofisa huyo kwani tangu alipowasili kikazi katika manispaa hiyo, haizidi miezi miwili.

“Ofisa huyo ametoka Ilemela na kuja hapa, kwa hiyo nitazungumza na mkuu wa mkoa ili amuondolee adhabu hiyo kwa sababu hana muda mrefu tangu awasili hapa,”alisema.

Makonda alisema amewapa muda wa wiki mbili kwa wakuu hao wa idara kuwasaka watumishi hewa na baada ya hapo, kazi hiyo itakuwa endelevu kwa kila aliyepewa dhamana ya kuisimamia ili kuokoa fedha zilizokuwa zikipotea.

“Haiwezekani mkuu wa idara akae bila ya kufahamu namna ya kuifanya kazi yake hadi alazimishwe au asimamiwe, nataka kuona kila mtu akitekeleza jukumu lake alilopewa kikamilifu,”alisema.

Mkuu huyo wa mkoa alisema serikali imetenga Sh.bilioni 40 kwa ajili ya maendeleo, hivyo bila ya kuwepo na kasi ya utendaji kazi, fedha hizo zinaweza kuliwa na wajanja na hatimaye lengo lisipatikane.

Makonda amewataka viongozi husika kuchukua hatua stahiki dhidi ya watumishi hao ili fedha zilizopotea zirejeshwe pamoja na kufunguliwa mashtaka kwa waliobainika.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu