Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar Dr. Ali Salim Ali alipofika kujitambulisha baada ya Tume hiyo kuwa chini ya Ofisi yake kufuatia mabadiliko ya Taasisi za Serikali uliofanywa hivi karibuni.
 Balozi Seif akikagua baadhi ya vitengo vya Ofisi ya Tume ya Ukimwi Zanzibar iliyopo Shangani Mjini Zanzibar akiwa katika ziara za kujitambulisha.
 Balozi Seif akizungumza na Watendji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar mara baada ya kuvitembelea vitengo mbali mbali vya Ofisi ya Tume hiyo Shangani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif akikagua baadhi ya vitengo vya Ofisi ya Tume ya Ukimwi Zanzibar iliyopo Shangani. Picha na OMPR,  ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika kwa Jamii kuwa na hadhari ya kuendelea kuelimishana katika kupiga vita vitendo hatarishi vinachochangia kuenea kwa maambukizo ya virusi vya Ukimwi hapa Nchini. 
Alisema mapambano dhidi ya vitendo hivyo yanahitaji nguvu za pamoja licha ya ugumu wa kazi hiyo ambayo wahusika wakuu ni miongoni mwa wananchi hasa vijana waliomo katika mitaa mbali mbali Mjini na Vijijini. 
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa Tume ya Ukimwi Zanzibar baada ya kufanya ziara fupi ya kujitambulisha kufuatia Tume hiyo kuwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kutokana na mabadiliko makubwa ya muundo wa Taasisi za Serikali uliofanywa hivi karibuni. 
Alisema utumiaji wa dawa za kulevywa, ukahaba pamoja na vitendo vya kujamiiana kwa kutumia jinsia moja ni miongoni mwa mambo matatu hatarishi yanayochangia kuenea kwa virusi vya ukimwi.

Balozi Seif alitahadharisha kwamba kuendelea kwa matumizi hayo ya vitendo hatari kunaweza kuigharimu Serikali kukosa nguvu kazi za watu hasa Vijana ambao ni asilimia kubwa ya Taifa.


Aliwahimiza watendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar kwa kushirikiana na taasisi za Kiraia waendelee kuongeza juhudi katika kutoa Elimu kwa umma kupitia vyombo mbali mbali vya Habari katika njia ya kupiga vita janga hilo. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameelezea faraja yake kuona hali ya ukimwi Zanzibar ipo chini ya asilimia 1% ikilinganishwa na mataifa mengine Duniani ikiwemo nchi za Afrika zilizopo katika Ukanda wa Jangwa la Sahara. 
Hata hivyo Balozi Seif alieleza kwamba bado jamii imetawaliwa na changamoto kubwa ya kutokuwa na tabia ya kupima afya zao jambo ambalo ni hatari katika kuyatambua maradhi yatakayokuwa yakimkabili mwanaadamu wakati wowote.

Katika kupiga vita maambulizi hayo Balozi Seif alishauri kuandaliwa kwa Sera itakayotengenezwa Sheria hapo baadaye ili kuchukuliwa hatua watu wanaoendeleza tabia ya kuambukiza wenzao virusi vya ukimwi kwa makusudi. 

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar Dr. Ali Salim Ali alisema watendaji wa Tume hiyo wamejipanga kuelekeza nguvu zao kwa vijana katika kutoa elimu ya mapambanao dhidi ya ukimwi ambao ndio waathirika wakuu wa maambukizo ya ukimwi hapa nchini.

Dr. Ali alisema utafiti umeonyesha wazi kwamba asilimia 12% ya vijana wenye umri kati ya miaka 12 hadi 16 ndio wanaokabiliwa na matatizo hayo kwa tabia yao ya kujiingiza katika matumizi ya kujidunga sindao.

 Alisema watu wasiopungua 200 huambukizwa viruzi vya ukimwi kila mwaka na hadi sasa inakadiriwa watu wapatao 400 wameshafariki dunia kutokana na maradhi hayo wakiwemo watoto wachanga wanaozaliwa wakiwa wameshaambukizwa virusi vya ukimwi.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Tume ya Ukimwi Zanzibar alieleza kwamba licha ya Zanzibar kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti ongezeko la maambukizi ya virusi vya ukimwi lakini utafiti mwengine unatarajiwa kufanywa ifikapo mwezi wa Nane mwaka huu kuangalia hali halisi ya maradhi hayo. 
Alisema katika kwenda sambamba na mpango Maalum wa Kimataifa wa kumaliza ukimwi kabisa ifikapo mwaka 2030 Umoja wa Afrika { AU }umeandaa mkakati kwa kuzishirikisha Nchi wanachama wa Umoja huo kuupeleka Umoja wa Mataifa New York kwa lengo la kuelezea hali halisi ya ukimwi Barani Afrika.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: