Friday, June 10, 2016

NAIBU WAZIRI AKUTANA NA UJUMBE WA UNDP

 Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mh. Luhaga Mpina akimkaribisha Bi. Awa Dabo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa. Mazungumzo baina yao yamefanyika leo Mtaa wa Luthuli, jijini Dar es Salaam.
 Ujumbe kutoka Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, kutoka kushoto ni Bw. Nehemia Murusuri, Bi. Getrude Lyatuu na Bi. Awa Dabo, walipomtembelea Naibu Waziri Mh. Luhaga Mpina hii leo.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mh. Luhaga Mpina akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa na Wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais mara baada ya mazungumzo baina yao.
---
Na Lulu Mussa

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mh. Luhaga Mpina hii leo amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Awa Dabo pamoja na ujumbe aliombatana nao, Ofisini kwake Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao ujumbe huo umeonyesha nia ya kufanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Makamu wa Rais hususan katika nyanja ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ikiwa ni pamoja na kupambana na mabadiliko ya Tabianchi na nishati mbadala.

Awali Naibu Waziri Mpina aliwafahamisha kuwa Ofisi yake imeandaa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa kupanda miti nchi nzima na kuwataka wadau wa maendeleo kuwaunga mkono. "Tunaendelea na jitihada za kupanda Miti mingi iwezekanavyo na katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kazi hiyo" alisisitiza Naibu Waziri Mpina.

Aidha, Naibu Waziri Mpina ametoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kuunga mkono kampeni hii kubwa ya upandaji miti nchi nzima na kusisitiza kuwa uhai wa viumbe vyote unategema Mazingira hivyo ni vema kuyahifadhi na kuyalinda kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Mheshimiwa Mpina pia amesema Ofisi yake kwa sasa inafanya marekebisho ya Sera ya Mazingira na kujenga uwezo kwa watendaji wa ngazi zote juu ya kusimamia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na kuelimisha Umma juu ya kampeni ya Usafi ya kila mwisho mwa mwezi.

kwa upande wake Bi. Dabo amesema kuwa shirika lake limeweka vipaumbele vya kutekeleza ndani ya miaka mitano ambavyo vinaendana na Mpango wa Maendeleo wa Taifa, sambamba na kusaidia vikundi mbalimbali katika ngazi za vijiji juu ya kutunza vyanzo vya maji na kuhifadhi mazingira.

Bi Dabo ameahidi kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais katika jitihada za kukabiliana na changamoto za Mabadiliko ya Tabianchi.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu