Monday, June 20, 2016

SERIKALI INAHUJUMU MAMEYA WA DAR ES SALAAM - MEYA WA MANISPAA YA KINONDONI, BONIFACE JACOB

Habari za mchana huu ndugu waandishi wa habari na wananchi wote ndani ya Manispaa ya Kinondoni, awali ya yote nimshukuru mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia pumzi na uhai mpaka leo hii, alikadhalika niwe miongoni mwa wengi tunaowatakia heri ndugu zetu Waislamu, katika mwezi huu Mtukufu wa tiba, mwenyezi Mungu awajalie heri na kuzisikia funga ziwe zenye Baraka kwao na jamii kwa ujumla.

Baada ya kutoa utangulizi huo, ndugu zangu waandishi wa habari na wananchi wa Kinondoni, sio kawaida yangu kuongea habari zinazohusu Serikali Kuu, kwa kuwa ninaamini kuwa Maendeleo ya Wananchi wa Mkoa huu wa Dar es salaam na Wilaya ya Kinondoni, hayawezi kuletwa kwa ubinafsi wa viongozi, bali ushirikiano mwema ya sisi tuliopewa dhamana ya kuziongoza Halmashauri kutoka vyama vinavyounda UKAWA, na CCM wanaounda Serikali Kuu. Jambo hili hufanya tuwe kimya na wavumilivu mara nyingi sana, ingawa bado kuna mahusiano ya kutia shaka kila kukicha.

Ila leo ndugu zetu waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla, tumeamua kuandika na kufikisha ujumbe huu kwenu, ili mjue yalipofikia kama viongozi na Serikali Kuu na mabaya yanayoendelea na ya kusikitisha sana.

Na kusema huku, tutafanya viongozi wakuu wa nchi kama walikuwa hawajui wajue au walitoa baraka hizi, basi sawa watusikie masikitiko yetu haya, kwa kuwa tulikuwa na imani nao sana na bado tutaendelea kuwa na imani nao kama Serikali juu ya kutatua changamoto na matatizo ya Wananchi.

Hali ya kimahusiano kati ya Mameya wanaotokana na UKAWA na Serikali Kuu si mazuri hata kidogo, viongozi tumeamua tuhabarishe umma wa Watanzania kuwa kuna hujuma za waziwazi zinazofanywa na wenzetu juu ya shughuli za Mameya wa Kinondoni, Ilala na Jiji la Dar es salaam.

Si mara ya kwanza hii kwa sisi Mameya kuhisi kuhujumiwa na baadhi ya viongozi serikalini ambao kimsingi, sisi tuliamini uchaguzi umeshapita na kwamba kila mmoja wetu atampa mwenzake heshima inayostahili juu ya ajenda za Maendeleo, ndiyo maana kama nilivyo sema hapo awali, tumekuwa kimya juu ya vikwazo vidogo vidogo ambavyo tulihisi ni hujuma lakini tukaamua kuwa kimya na wavumilivu lakini tunatambua kuwa ipo mikakati ovu mingi dhidi yetu, ya kutukwamisha tusifanikiwe kuleta Maendeleo ndani ya Mkoa wetu na Wilaya zetu, hata tulipo amua kuvumilia uchokozi wa wawaziwazi wa kejeli za kutishia kunyang'anya Mameya magari na vinginevyo, kutoka kwa mtu tunaye muheshimu kama Waziri wa TAMISEMI ofisi ya Rais, akidai wakurugenzi watupore magari tena mbele ya vyombo vya habari.

Ila sasa hujuma zimefika mahali pabaya kiasi kwamba kutukwamisha kupata misaada ya Maendeleo kutoka kwa nchi rafiki na Halmashauri zilizopo Dar es salaam.

Binafsi Manispaa ya Kinondoni nilishawahi kunyimwa ruhusa nisisafiri kwenda nchini Afrika ya Kusini nilipokuwa nimealikwa na wahisani waliotaka kunifadhili kutengeneza mto Mlalakuwa, uliokuwa utengenezwe kingo zake kuanzia Goba,Makongo juu mpaka Kata ya Kawe kuelekea baharini, wafadhili hao ni ICLEI-local government sustainability, mradi ambao ulikuwa unafanyika nchi nyingi za Afrika.

Mbali nakuwa wafadhili walikubali kulipia usafiri,malazi na gharama zote za kongamano lililokuwa lifanyike huko Afrika Kusini, nchi zote zilifika katika kongamano la CIP AIRR, lakini uwakilishi wetu ulikosekana kwa kisingizio cha ruhusa kutopatikana, madhara yake Manispaa ya Kinondoni ikaondolewa kwenye programu ya kufadhiliwa huku nchi kama Ghana,Kenya,Zambia na nyinginezo zikifadhiliwa. Baada ya mkutano kuisha nchini Afrika Kusini, Katibu Mkuu kiongozi akaniandikia kibali cha kusafiri, baada ya kongamano kuisha na kukosa kiasi cha tshs Bilioni 1.3.

Kubwa lilofanya kuwatarifu nyinyi na umma juu ya hujuma hizi ni kitendo cha juzi alfajiri. Tukiwa tayari uwanja wa ndege kuanza safari ya mualiko wa kwenda nchini uturuki, ulio andaliwa na kufadhiliwa na ubalozi wa uturuki nchini Tanzania kwa ajili ya kukamilisha maongezi yaliyokwisha anza hapa Dar es salaam juu ya kusaidia kutatua chngamoto za ajira za vijana kwa miradi endelevu; ikiwemo mpango wa ujenzi wa chuo cha ufundi stadi kwa udhamini wa ubalozi wa uturuki,kupitia wafadhili wake.

Ubalozi wa Uturuki ulikuwa umedhamini safari ya Mameya kwenda Uturuki kukutana na wadau na wafadhili wa miradi mbalimbali ikiwemo ikiwemo Chuo Cha Ufundi ndani ya Manispaa ya Kinondoni, Ubalozi huo ulikuwa umeshatoa kibali cha kusafiri (Visa) na kugharamia fedha za usafiri, malazi, chakula na gharama zingine zote, ambapo matayarisho tu yali gharimu kiasi cha dola za kimarekani 42,000/=,sawa na shillingi millioni 88,kwa mameya wote wanne na mtendaji mmoja mmoja kutoka kila Halmashauri.

Safari pamoja na mkutano vilitakiwa kuanza tarehe 16 june mpaka 19 june 2016,huku wafadhili na wadau wetu wa maendeleo wakiandaa mialiko na wawekezaji na wafadhili kutoka sehemu mbali mbali za uturuki,kuja makao makuu ya nchi hiyo,jiji la instanbul ulitarajiwa lakini Serikali imevunja Safari hiyo.

Kwa kufanya hivi Serikali imezikosesha Manispaa zetu fursa za Maendeleo ikiwemo Chuo hicho cha ufundi.

Msimamo wetu kwenye hili suala ni kutaka kujua:

• Je huo ndio msimamo rasmi wa viongozi wote wa serikali,?

• Tungependa kusikia Tamko kutoka kwa Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kama maagizo haya ya kubana fedha na matumizi ya serikali yanahusianaje na safari za kufadhiliwa na nchi wahisani?

• Je hakuna namna ya kushirikiana na nchi rafiki kutupatia miradi ya Maendeleo?

Mwisho nimalizie kwa kusema sisi bado tuna imani ya kwamba hujuma hizi Mheshimiwa Rais hazifahamu ila isipokuwa baadhi ya viongozi wa serkali wanajaribu kuweka tafsiri tofauti ya sera ya kuzuia matumizi mabaya ya fedha kwenye safari za nje ya nchi.

Pamoja na kutumia vibaya agizo la Mheshimiwa Rais kuruhusu vibali vya viongozi katika mamlaka mbalimbali za serikali, Sisi tuna amini kuwa agizo la kuomba kibali maalumu ikulu halituhusu sisi (kama viongozi tusio watendaji), wala kutumia bajeti za serikali au halmashauri zetu kwenda kuonana na wadau wamaendeleo.

IMETOLEWA NA MSTAHIKI MEYA WA MANISPAA YA KINONDONI.
BONIFACE JACOB.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu