Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF),Godfrey Simbeye (katikati) akizungumza kwenye Mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, kuhusu mafunzo yatakayo tolewa kwa wajasiriamali wadogo na wakati kupitia tovuti ya taasisi hiyo. Meneja mradi wa TPSF Celestine Mkama (kushoto) wa mwisho kulia Mtaalamu wa ujasiriamali na maendeleo ya kiuchumi, Haji Dachi.
Meneja Mradi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Celestine Mkama (kushoto) ) akizungumza kwenye Mkutano na waandishi wa habari Dar es salaam, kuhusu mafunzo yatakayotolewa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kupitia tovuti ya taasisi hiyo. Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Godfrey Simbeye na Mtaalamu wa ujasiriamali na maendeleo ya kiuchumi, Haji Dachi.
Mtaalamu wa ujasiriamali na maendeleo ya kiuchumi, Haji Dachi (kulia) akizungumza na waandishi wa habari Dar es salaam, namna wajasirimali wadogo na wakati watakavyo weza kunufaika na mafunzo yatakayotolewa na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) kupitia tovuti ya Taasisi hiyo . kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Godfrey Simbeye.
---
Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa kushirikiana na Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT) itaendesha mafunzo maalum kwa wajasiriamali nchi nzima kuhusu namna ya kunufaika na tovuti mpya ya habari kwa wajasiriamali.

Akiongea kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Mkurugenzi Mkuu wa TPSF, Godfrey Simbeye amesema taasisi hiyo imeanzisha vipindi vya redio katika vituo mbalimbali vya redio za kitaifa na vituo vidogo vya redio za jamii katika mikoa ya Dodoma, Geita, Kigoma na Mbeya. Vipindi hivyo vya redio vitaenda sambamba na warsha za mafunzo zitakazowahusisha wajasiriamali na wadau mbalimbali katika mikoa hiyo.

“Kampeni hii imelenga kuongeza uelewa wa wajasiriamali juu ya tovuti hiyo ambayo ina mifumo ya mafunzo kwa wajasiriamali, namna ya kuanzisha na kukuza biashara, upatikanaji wa mitaji, mbinu sahihi za kuendesha biashara, namna ya kutafuta na kuuza bidhaa katika masoko, vilevile kampeni itatoa jukwaa la majadiliano kuhusu mada mbalimbali zinazowahusu wajasiriamali wadogo nchini.” alisema Simbeye.

Mafunzo yatatolewa nchi nzima na wataalamu waliobobea katika biashara na ujasiriamali kwa kipindi cha miezi nane ili kuwajengea uwezo wajasiriamali waweze kunufaika ipasavyo na tovuti hiyo iliyozinduliwa mapema mwaka huu na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage mapema mwaka huu. Tovuti hiyo inayopatikana kupitia www.entrepreneurs.or.tz, www.wajasiriamalitz.or.tz au kwa kupiga namba *148*99*06# ni kituo maalum chenye taarifa zote sahihi zinazomtosheleza mjasiriamali kuendesha biashara kwa mafanikio.

“Huduma hii imetolewa ili kuwasaidia wajasiriamali ili waweze kupata nyenzo muhimu za kuendesha biashara, vyanzo vya fedha, kuingia kwenye masoko ya hapa nchini na kimataifa, na taarifa nyingi za kuweza kumsaidia mtu anayetaka kuanzisha biashara na kuwawezesha wale ambao tayari wanafanya biashara kujiongezea ujuzi na uzoefu,” alisema Simbeye.

Meneja Mradi wa Tovuti hiyo, Celestine Mkama alisema “Tumeona umuhimu wa kuendesha kampeni ya kuongeza uelewa wa tangu wakati tunatengeneza mfumo huu wa habari. Tunatarajia kupitia kampeni hii kuweza kuwafikia wajasiriamali moja kwa moja kupitia vipindi vya redio na warsha na kuweza kutatua matatizo yao kwa kuwapatia ujuzi”. Hivi sasa kuna wajasiriamali zaidi ya milioni tatu nchini na tunajua kwamba ujuzi hafifu ni kikwazo kikubwa katika ukuaji wa biashara ndogo ndogo ambazo ni muhimu sana katika ukuaji uchumi,” alisema Mkama.

“Tunataka kuhamasisha matumizi ya tovuti hii na kutoa mafunzo wakati huo huo. Tunaamini jambo hili litawajengea uwezo na kuwapa wajasiriamali ujuzi muhimu wa kuendesha biashara endelevu.”
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: