Friday, July 1, 2016

WAKUU WAPYA WA WILAYA MKOA WA PWANI WAAPISHWA LEO

MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo kushoto akimkabidhi zana za kufanyia kazi mkuu wa wilaya ya Kibiti Gulamu Kifu, baada ya kumwapisha kwenye hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya ofisi ya mkuu huyo wa mkoa.
Mkuu mpya wa wilaya ya Kibaha Asumpter Mshama kulia akiapa mbele ya mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo kushoto wakati wa hafla iliyofanyika mjini Kibaha ya kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya za mkoa huo ambao waliteuliwa hivi karibuni na Rais Dk John Magufuli
Mkuu mpya wa wilaya Rufiji Juma Njwayo kulia akiapa mbele ya mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo wakati wakiapishwa wakuu wa wilaya za mkoa huo kwenye viwanja vya ofisi ya mkuu wa mkoa huo iliyopo mjini Kibaha.

Na John Gagarini, Kibaha.

MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewataka wakuu wapya wa wilaya wlioteuliwa na Rais Dk John Magufuli mkoani humo kuinua pato la wananchi wa mkoa huo kutoka milioni 1.2 kwa mwaka hadi milioni 3 kwa mwaka.

Ameyasema hayo leo mjini Kibaha wakati akiwaapisha wakuu hao wa wilaya wapya na kusema kuwa pato la mwananchi wa mkoa wa Pwani liko chini sana licha ya kuwa na fursa mbalimbali za kipato.

Ndikilo amesema kuwa kutoakana na pato hilo la wananchi kuwa dogo kiasi hicho hata mchango wa mkoa kwa Pato la Taifa ni dogo sana la asilimia 1.8 jambo ambalo linapaswa kuwekewa mkakati wa kupandisha pato hilo ili liwe na mchango mkubwa kwa mwananchi na Taifa kwa ujumla.

“Nawapongezeni kwa kuchaguliwa kwenye nafasi hizi na mkoa tayari umeandaa mpango kazi wake kwa ajili ya kuinua pato la mwananchi hivyo mnapaswa kuweka vipaumbele ambavyo vitasaidia kuinua uchumi wa wananchi wa wilaya unayoongoza,” alisema Ndikilo.

Amesema kuwa hakuna sababu ya mkoa kuendelea kuwa na pato dogo huku kukiwa na vyanzo vingi vya mapato ikiwa ni pamoja na rasilimali mbalimbali kama vile uvuvi, kilimo, korosho, maliasili ikiwa ni pamoja na mbuga za wanyama na madini mbalimbali.

“Mfano ni majumba mengi yanayojengwa Dar es Salaam kokoto na mawe yanatoka mkoa wa Pwani hivyo hakuna sababu ya kuwa maskini tuna zao la korosho ambapo kwa msimu uliopita wakulima waliuza korosho zenye tahamani ya shilingi bilioni 18,” alisema Ndikilo.

Amewataka wahakikisha wanawajibika na kutowalea watumishi ambao ni kikwazo na wenye urasimu wa kuwahudumia wananchi ambao hufika ngazi ya mkoa kulalamika ili hali ngazi za chini kuna watendaji ambao wangeweza kutatua matatizo hayo.

“Changamoto ni nyingi ikiwa ni pamoja na suala la ulinzi na usalama, wahamiaji haramu, matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi nisingependa mambo haya yatokee tena hakikisheni mnatimiza wajibu wenu na kuwaondolea kero wananchi,” alisema Ndikilo.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga alisema kuwa moja ya changamoto ambazo atakabiliana nazo ni pamoja na wahamiaji haramu kw akudhibiti bandari 19 ambazo zimekuwa ni njia ya wahamiaji hao haramu.

Naye Asumpter Mshama amesema kuwa moja ya mambo atayapaa kipaumbele ni kuhakikisha fedha kwa makundi ya vijana na akinamama asilimia 10 zinatoka ili wananchi waweze kujenga uchumi wao na ule wa Taifa.

Wakuu wapya walioapishwa jana ni pamoja na Shaibu Nunduma wilaya ya Mafia, Filberto Sanga Mkuranga, Gulamu Kifu wilaya ya Kibiti, Asumpter Mshama wilaya ya Kibaha, Juma Njwayo wilaya ya Rufiji na Majid Mwanga wilaya ya Bagamoyo huku Happyness William hakuweza kuapishwa kutokana na dharura.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu