Tuesday, August 30, 2016

AKINAMAMA WAJAWAZITO WAJIFUNGUA KWA TOCHI ZA SIMU MONDULI - ARUSHA

Na Woinde Shizza, Arusha.

Wajawazito katika zahanati ya kijiji cha Selela kata ya Selela wilaya ya Monduli mkoani Arusha wamelazimika kujifungua kwa kutumia tochi za simu pamoja na taa ya chemli kutokana na kukosekana kwa huduma ya umeme kwa takribani mwezi mmoja na wiki mbili.

Kinamama wa kijiji hicho tumaini shirima na mwasiti hemedy wameeleza kuwa wamekua wakiwapeleka wajawazito kwenye zahanati hiyo kwa ajili ya kujifungua na kushuhudia wauguzi wakitumia tochi za simu kutoa huduma kwa wajawazito jambo ambalo linawafedhesha hivyo wameiomba serikali isaidie upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme ili waweze kupata huduma bora.

“Tunapata shida hata tunapowapeleka Wajawazito zahanati hakuna umeme wauguzi wanatumia tochi za simu, juzi tulimpeleka mwenzetu akajifungue tuliona hilo likijitokeza kwa sababu umeme hakuna”

Mganga wa zahanati hiyo Michael Msalu alisema kuwa nyakati za usiku wanalazimika kutumia tochi jambo ambalo linaweza kuathiri afya ya mama mjamzito na mtoto, vile vile wameshindwa kufanya baadhi ya vipimo maabara kutokana na kukosa huduma ya umeme .
 
Msalu anaeleza kuwa si jambo zuri kiafya kushika simu huku unamhudumia mama mjamzito unaweza kusababisha maambukizi kwani huduma hiyo inahitaji uangalifu mkubwa ili kulinda afya ya mama na mtoto pamoja na mtoa huduma.

Diwani wa kata ya Selela, Cathbert Meena amesema kuwa licha ya zahanati hiyo shughuli za kiuchumi na kijamii zimesimama katika kata hiyo ikiwemo biashara, mashine za kusaga nafaka kwa muda wa mwezi mmoja na wiki mbili baada ya transfoma iliyowekwa na Tanesco kupata hitilafu baada ya kuwasiliana na mamlaka hiyo imekua ikitupiana mpira kati ya Rea katika maboresho hayo.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mkoa wa Arusha Tanesco ambaye ni Mhandisi Mkuu Donasian Shamba amekiri kuwepo kwa tatizo hilo ambalo linasababishwa na masuala ya kitaalamu yanayopelelekea transfoma kuungua mara kwa mara hivyo wametuma timu ya wataalamu na mapema wiki hii watarekebisha tatizo hilo ili wananchi wapate huduma.

Wakazi wa Selela wamelazimika kusimamisha shughuli zao za uchumi zinazotegemea nishati ya umeme hivyo wanaiomba serikali ichukue hatua ili waweze kurudi katika shughuli za uzalishaji zinazowaingizia kipato.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu