Saturday, August 6, 2016

GELINE AWAHIMIZA WATANZANIA KUJUA HAKI ZAO

Geline Fuko (kushoto) akipokea maua kutoka kwa wafanyakazi wenzake wa LHRC kama ishara ya pongezi mara baada ya kutua katika uwanya wa ndege wa kimataifa wa Mwl. Julius Kambarage Nyerere akitokea Marekani alikokuwa akihudhuria mafunzo ya vijana wa kiafrika yaliyoandaliwa na Raisi Obama. Geline alipata heshima ya wazo lake la kuanzishwa kwa Kanzidata ya Katiba chini ya LHRC kutambuliwa na Raisi Obama.
---
Shangwe zilitawala wakati mtanzania Geline Fuko alipowasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl. Julius Kambarage Nyerere majira ya saa nne usiku Agosti 5, 2016 akitokea nchini Marekani alikohudhuria mafunzo ya viongozi vijana kutoka bara la Afrika. Wafanyakazi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ambao ni wafanyakazi wenza wa Geline, familia ya Geline, ndugu na marafiki walitoa mapokezi ya kishujaa kwa mwanaharakati huyo aliyetajwa kuwa mfano wa kuigwa na Raisi Obama.

Akizungumza na wanahabari, Geline alisema amefarijika na hakutarajia kama wazo lake la kuanzishwa kwa Kanzidata ya Katiba litakuwa wazo kubwa ambalo litakubalika mpaka na Raisi Obama. Hata hivyo Geline amesema amefurahishwa na program hiyo ya Mandela Washington Fellowship kwani imewawezesha washiriki kujifunza mambo mengi na kupata uono mpana zaidi wa kufanya mambo.

Geline aliwahimiza watanzania kutembelea Kanzidata hiyo iliyopo mtandaoni (http://katiba.humanrights.or.tz/) ili kuweza kuijua katiba yao na kuweza kujua haki zao kama watanzania. Mwisho alishukuru kwa mapokezi makubwa ambayo pia hakuyatarajia.

Akitoa neno la shukurani kwa Geline kwa niaba ya LHRC, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala-LHRC Ezekiel Masanja amempongeza Geline kwa kuitoa kimasomaso LHRC na Tanzania kwa ujumla.

Geline Fuko amepata kutambulika baada ya Raisi Obama kumtaja kama mfano wa kuigwa wa wanaharakati wa haki za binadamu wakati akizungumza Jumatano Agosti 3, 2016 katika kilele cha mpango wake wa kuwawezesha vijana wa kiafrika unaojulikana kama Mandela Washington Fellowship. Raisi Obama alimsifu mwanasheria huyo kutoka LHRC ambaye ni moja ya vijana 1000 waliokuwa jijini Washington kwa lengo la kujengewa uwezo ili kuweza kusaidia Maendeleo katika Nyanja zote za maisha katika nchi zao. Raisi Obamaalisifu juhudi za Geline za kuibua wazo la kuanzisha kwa mara ya kwanza Kanzidata ya Katiba nchini Tanzania na kutekeleza wazo hilo chini ya LHRC.

Raisi Obama alikaririwa akisema “Marekani itaendelea kushikakamana na wanaharakati kama Geline Fuko kutoka Tanzania. Geline ni mwanasheria na mwanaharakati wa haki za binadamu ambaye amefanikisha kuanzishwa kwa Kanzidata ya Katiba ya kwanza na ya pekee nchini Tanzania inayowawezesha watanzania kusoma Katiba kupitia simu zao za mkononi”.

Programu ya Mandela Washington Fellowship yenye lengo la kuwawezesha vijana wa Kiafrika katika Nyanja za kiuchumi, kisiasa, kiteknolojia na kijamii ilianzishwa na Raisi Obama mwaka 2014. Programu hii hujumuisha vijana elfu moja (1000) kutoka nchi mbalimbali za Afrika ambao hugaramiwa na serikali ya Marekani kwenda jijini Washington kwa lengo la kujengewa uwezo zaidi.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilianzisha Kanzidata ya Katiba mwaka mmoja uliopita mnamo Julai 15, 2015. Kupitia tovuti maalumu (http://katiba.humanrights.or.tz/) na simu za mkononi, watanzania wanaweza kusoma Katiba katika Kanzidata hiyo.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu