Sunday, August 21, 2016

HERI KUTAFUTA KUPENDA KULIKO KUPENDWA

Iko mithali maarufu isemayo; MPENDE AKUPENDAYE! Mithali hii inadai KUPENDWA KWANZA na sio KUPENDA KWANZA. Huu ni ushahidi wengi
Wetu tunatafuta kupendwa kwanza badala kupenda wengine.

Lakini kwa mchaji Mungu, Biblia imeamuru kupenda wengine kwanza badala ya kutafuta kupendwa na wengine kwanza. Ndiyo maana Yesu aliweka bayana akisema: “…nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” (MK.12:30-31)

Hapa tafsiri ya “kupenda” maana yake ni “kujitoa mhanga” kwa ajili ya Mungu na wengine”! kupenda ni "kumtanguliza Mungu" kwanza na "kuwatanguliza wengine".

Kujitoa mhanga ni "kuumia kwa ajili ya Mungu na wengine", ili kumfurahisha Mungu na wengine.

KWANINI MUNGU AMETUAMURU KUMPENDA YEYE NA WENGINE KWANZA?

Mungu anatutaka sisi tufanane naye kitabia. Ni tabia ya Mungu kutafuta kupenda kuliko kupendwa. Tangu binadamu alipoanguka dhambini, ni Mungu aliyetangulia kuchinja dhabihu ya kwanza kwa ajili ya msamaha wa dhambi, na akamfunika na ngozi ya mnyama aliyemchinja. (MW.3:21)

Hata mpango wa ukombozi wa binadamu ulipofika ni Mungu aliyetangulia kuupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe pekee (YH.3:16). Ndiyo maana mtume Yohana ameandika akisema: “ Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza.” (1 YH.4:19)

HATARI YA KUJIPENDA KWANZA

Ukitafuta kupendwa wewe kwanza tayari utajikuta unachochea ubinafsi (uchoyo na ubahili) badala ya kusaidia wengine! Na dhambi kuu kuliko zote ni UBINAFSI.

Ndiyo maana ubinafsi unapotawala katika jamii unatafsiriwa kimaandiko kuwa ni nyakati za hatari: “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha…..” (2 TIM.3:1-2)

Unaona rafiki? Hizi zinaitwa nyakati za hatari. Hatari ipi? Ni hatari sana kujitanguliza sisi wenyewe badala ya Mungu na wengine. Ni hatari sana "kuabudu" fedha badala ya Mungu na kutumikia wengine.

Hii inaitwa hatari kwa sababu katika “kujipenda” kunapofusha macho na kupoteza kanuni ya ushirika na Mungu na wengine.

FAIDA ZA KUTAFUTA KUPENDA BADALA YA KUPENDWA

Ikiwa tutafaulu zoezi la kutekeleza amri ya kumpenda Mungu na wengine kwanza, tayari tutakuwa tunatii amri iliyo kuu. Na utii ni bora kuliko kuliko dhabihu.

Aidha, kutanguliza kupenda ndio msingi wa sisi kupendwa na Mungu na wengine. Ukitanguliza kupenda kwanza mrejesho wake ni wewe kupendwa pia. Lakini ukijipenda mwenyewe mrejesho wa kupendwa utabaki kitendawili kwetu.

Hebu tuanze hivi sasa baada ya kusoma makala hii. Ubarikiwe.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu