Sunday, August 7, 2016

MANISPAA YA KINONDONI KUGAWANYWA ILI IPATIKANE MANISPAA YA UBUNGO

BARAZA la Madiwani Manispaa ya Kinondoni jana limekutana na kufanya kikao maalum cha kujadili na kupitia mapendekezo ya mgawanyo wa manispaa hiyo.

Kikao hicho kimekuja mara baada ya serikali kuu kuidhinisha kuwapo kwa wilaya tano katika jiji la Dar es Salaam badala ya tatu zilizokuwapo awali hivyo manispaa hiyo imegawanywa na kuwa wilaya mbili yaani wilaya ya Kinondoni na Ubungo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Mstahiki Meya wa manispaa hiyo, Boniface Jacob alisema kikao hicho cha baraza pia kitaangalia namna ya mgawanyo wa mali, rasilimali na madeni ya halmashauri katika wilaya hizo mbili.
Alisema kama mambo yatakwenda vizuri kwenye kikao hicho watafikia muafaka wa kugawanya vitu hivyo na kila mtu ataenda kivyake na kuanza kutekeleza majukumu yake kwa wananchi.

“Naomba kuwaambia madiwani kuwa wilaya zote ni muhimu kwani wakati watu wanatoa mapendekezo ya kuigawanya kinondoni waliangalia na kuzingatia vigezo vingi hivyo katika majadiliano yetu kusitokee na vitu ni kuvute tuweke masilahi ya wananchi mbele na ya kwetu nyuma, tukifanya hivyo tutafanikiwa.

“Lakini pia watu wa Ubungo wasimame vizuri na kutoa hoja na kuwashauri watu wa kinondoni mambo ya msingi ili tufikie muafaka mzuri na watu wa kinondoni wafanye vivyo hivyo, rai yangu kwa madiwani tujadili kwa kina na kwa utulivu ... sitegemei kikao kiwe cha migongano ,” alisema Meya Jacob.

Hata hivyo alisema baada ya majadiliano hayo kukamilika wataita vyombo mbalimbali vya habari na kutoa taarifa juu ya kile walichokubaliana kwa pamoja.

“Tukishamaliza kuangalia mapendekezo na majadiliano yetu tutawaita waandishi wa habari na kuwaambia nini tumejadili na kukubaliana na mipango ikoje ya kuanza kazi katika wilaya hizo,” alisema Meya Jacob.

Imeandikwa na Janet josiah.

Mwisho.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu