Wednesday, August 10, 2016

MAONI YA MSOMAJI; BARUA YANGU KWA WATANZANIA WANAOUNGA MKONO UKUTA

KWENU Watanzania wenzangu ambao kwa pamoja tunaitakia mema nchi yetu. Salamu zangu zimfikie kila mmoja wetu ambaye kikatiba ananeemeka na matunda yanayotokana na Tanzania yetu.

Binafsi mimi ndugu yenu, Erick Evarist ni mzima wa afya. Namshukuru Mungu naendelea vizuri na majukumu yangu ya kila siku. Mimi kazi yangu ni uandishi wa habari na kupitia gazeti hili, nimekuwa nikiwaandikia Watanzania wenzangu ambao ni mashuhuri.

Toafauti na mazoea yangu ya kila siku, leo nimewakumbuka Watanzania wote kwa ujumla wao ili niweze kuwafikishia kile kilichopo moyoni mwangu.

Ndugu zangu, madhumuni ya barua hii ni kutaka kuwakumbusha Watanzania kuhusu suala zima la Septemba 1. Hakika kila mmoja anajua kwamba, viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, wametangaza msimamo wao waliouita Ukuta.

Wakiapa kupambana na serikali kwa kile walichodai imepoka demokrasia. Japo viongozi hao sijawasikia wakinyambua vizuri hoja zao za msingi lakini miongoni mwa mambo ambayo wanayatetea, ni suala la kuuiwa kufanya maandamano na mikutano ya kisiasa.

Pia kwa upande mwingine hoja yao iumeegemea kwenye Bunge lililopita, bunge la 10. Wanasema, Naibu Spika, Tulia Ackson hakuwatendea haki, alikibeba zaidi chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuwanyima nafasi ya kuzungumza wapinzani.

Ndugu zangu, wakati natafakari hoja hizo, nipata shaka kama kweli hoja hizo zinanitosheleza mimi kuingia barabarani kuandamana. Napata shaka maana kuna vitu vinachanganywa, katika hoja ya mikutano, ufafanuzi umeshatolewa mara kwa mara.

Serikali imesema haijazuia mikutano badala yake wamezuia maandamano yasiyokuwa na tija. Kwamba kiongozi wa chama fulani, anao uwezo wa kufanya mikutano katika eneo lake, akazungumza nao katika suala zima la kuleta maendeleo.

Mwenyekiti serikali za mtaa, Diwani, mbunge anaweza kufanya hivyo kwa muda wake na watu wake. Tunachotaka kuandamana faida yake ni nini? Tukiandamana ndiyo mambo uhuru wa demokrasia utapatikana?

Rais ameshasema tusiandamane maana yeye ndiye mwenye dhamana na nchi kwa sasa. Ndiye amiri jeshi mkuu, ambaye jeshi la polisi na majeshi mengine yote yako chini yake. amesema maandamano hayo ni haramu. Kwa maana nyingine hayana baraka za jeshi la polisi.

Kuingia mtaani bila kibali ina maana ni kuvunja sheria za nchi. Hilo ndugu zangu si jambo jema. Ni ishara kwamba tunataka kuipoteza amani pasipo kuwa na hoja. Wanaotetea maandamano labda huenda wana malengo yao, tofauti na suala la kupokwa kwa demokrasia.

Kwani kila mbunge akifanya mikutano yake, akaelezwa kile ambacho viongozi wake wa kitaifa wamedhamiria katika kuleta maendeleo kitaharibika nini? Hoja ya kwamba rais anajipa nafasi ya kuwakushukuru Watanzania kwa kumpigia kura mbona liko wazi, yeye si ndiyo mshindi?

Wapinzani wanataka kushukuru Watanzania kwa lipi? Tuache aliyeshinda ashukuru na apate muda wa kutekeleza ahadi alizowaahidi wananchi kuliko kumpinga.

Hoja ya kwamba wapinzani walibanwa bungeni, naiona kwa sasa si wakati wake. Wangepambana kwa hoja bungeni kuliko vile walivyokuwa wanatoka.

Mimi ni ndugu yenu;
Erick Evarist.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu