Sunday, August 21, 2016

MARIE STOPES TANZANIA: TUMEOKOA MIMBA 870,000 ZISITOLEWE (ABORTION)


Na Veronica Romwald, Dar es Salaam.

HUDUMA ya mbalimbali za afya ya uzazi zinazotolewa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Maria Stope zimewezesha kuokolewa kwa mimba 870,000 zilizokuwa zitolewe (abortion).

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano wa Taasisi hiyo, Symphrose Makungu alisema takwimu hizo ni za mwaka jana pekee.

Alisema zimekusanya kutoka katika vituo vyake zaidi ya 30 vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini.

“Taasisi yetu ilianzishwa mwaka 1989, tunatoa huduma ya afya ya uzazi na ushauri juu ya uzazi wa mpango, kwa mwaka jana pekee kupitia elimu tunazotoa kwa wananchi wanaokuja kwenye vituo vyetu imesaidia kuokoa mimba 870,000,” alisema.

Alisema mimba hizo zilikuwa zitolewe na wahusika waliokuwa wamezibeba kutokana na sababu mbalimbali ambazo nyingi kati ya hizo hazina msingi wowote.

“Tunapokea watu wengi kwenye vituo vyetu, miongoni mwao wapo wasichana wadogo ambao walipata ujauzito bila ya kutarajia hapa naongelea juu ya mimba za utotoni.

“Mabinti hao tunapozungumza nao wengi wao wamekata tamaa ya maisha kwanini wamepatwa na hali hiyo wakati wakiwa wadogo na wanahitaji kuendelea na masomo yao,” alisema.

Alisema hata hivyo baada ya kupewa ushauri nasaha walikubaliana na hali waliyonayo na kujifungua watoto wao salama.

“Mbali na hilo, kwa mwaka huo huo tumefanikiwa kuepusha mimba 330,000 zisizokuwa za kutarajiwa, tumeokoa vifo vya kina mama vipatavyo 5,000 na vya watoto 6,400,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Afya wa taasisi hiyo, Dk. Joseph Komwihangiro alisema mwaka jana walihudumia zaidi ya wanawake 500,000 ambapo asilimia 12 kati yao walikuwa ni wasichana wenye umri mdogo.

“Ipo haja ya kuanza kutoa elimu ya afya ya uzazi katika shule za msingi na sekondari kama ambavyo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anavyopendekeza,” alisema.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu