Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob akiongea na wakazi wa Kata ya Kunduchi Mtaa wa Mji mpya na Mecco katika viwanja vya Mecco jijini Dar es Salaam ambapo amewaambia kuwa maeneo yao hayatauzwa hivyo kuwataka wananchi waendeleze maeneo yao kujenga nyumba za kisasa na serikali nayo kujenga majengo ya huduma muhimu kama vile Zahanati, shule na masoko.
Mbunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee akiongea machache.
 Wananchi wakiwa wamewapokea viongozi hao wakati wakitembelea maeneo yao.
---
HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni imemaliza mgogoro wa ardhi kwa kuwaondoa hofu wakazi wa Kata ya Kunduchi Mtaa wa Mji mpya na Mecco kuwa eneo lao halitauzwa wala kugaiwa mwekezaji yoyote atakayekuja kuwekeza.

Eneo hilo ambalo lina kaya zaidi ya 1000 limekuwa na mgogoro kwa muda mrefu huku wananchi wakidaiwa kubomolewa na kuondolewa katika maeneo yao wakiambiwa kuwa linahitajika kwaajili ya uwekezaji.

Leo 13/8/2016 katika viwanja vya Mecco Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob aliwaambia wakazi wa Kata ya Kunduchi, maeneo ya mitaa ya Mji mpya na Mecco kuwa hayatauzwa hivyo kuwataka wananchi waendeleze maeneo yao kujenga nyumba za kisasa na serikali nayo kujenga majengo ya huduma muhimu kama vile Zahanati, shule na masoko.

Meya Jacob alisema kwa haraka sana manispaa itapeleka wataalam wake wa ardhi na mipango miji kupima eneo hilo ili liwe maalum kwa ajili ya makazi ya watu.

"Sisi kama Manispaa tunawaambia kuwa eneo hili alitauzwa wala hatuna muwekezaji ambaye atakuja kuwekeza hapa hivyo nawaomba mlale usingizi mzuri jengeni nyumba za maana za kuishi na wale ambao wana viwanja uzeni bila wasiwasi," alisema.

Meya Jacob alisema maamuzi ya kuwaondoa hofu wananchi hao haja yafanya peke yake bali ni vikao vya kikatiba vya baraza la madiwani na kikao cha fedha na uongozi ambavyo viliamua kuruhusu ardhi hiyo imilikiwe na wananchi.

Aidha alisema maamuzi hayo yamefikiwa baada manispaa kama serikali kutaka kumaliza mgogoro huo uliochukua miaka mingi kwa wananchi kwenda kuishitaki.

"Baada ya wananchi kuishitaki manispaa, kesi mbili ambazo zilikuwa hazitaki kumalizana ...tuliona tuzungumze na wanasheria ambao walikuwa wakisimamia kesi hiyo Kituo cha haki za binadamu (LHRC) na Kampuni ya Nyumba Bora ili kumaliza mgogoro huo"

Hata hivyo Meya Jacob aliwataka wananchi hao kutomsikiliza yeyote atayetaka kuuibua mgogoro huo hasa madalali ambao alidai ndiyo walikuwa vinara wa kuuchochea mgogoro huo kwa kuwachochea wanasheria, kuwapeleka wawekezaji na kuchangisha fedha.

"Sasa tunafungua ukurasa mpya, wana mecco na mji mpya endelelezeni nyumba na sisi manispaa tujenge miundombinu ya maendeleo ... yoyote atakayewaletea maneno mwiteni dalali na kumripoti kwetu" alisema

Na katika hatua nyingine, Meya Jacob alisema atawachukulia hatua watendaji wa kata na mitaa hiyo ambao hawakufika katika kikao hicho cha jana.

"Mtendaji wa kata ya Kunduchi na mitaa hii nitawachukuliwa hatua za kukosa nidhamu....kwanini hawakufika katika kikao hiki wakati walitakiwa kuwepo?

Ujumbe wa kikao hiki ni munimu sana lakini hawakufika ... hawa nawamudu, nitawaondoa hapa."

Mapema akimkaribisha Meya Jacob, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee lengo la kikao hicho ni kumaliza mgogoro wa ardhi hiyo ya Mecco na Mji Mpya ambalo limekuwa na uchochezi wa watu tofauti wenye maslahi yao.

"Ndugu zangu wananchi, mstahiki Meya ... nadhani sasa mara baada ya kikao hiki, kwa pamoja tutaweza weza kufanya maendeleo na manispaa kurudisha huduma za msingi ambazo zimekatwa kwasababu ya mgogoro huu" alisema Mdee

Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa kamati ya mipango miji Mustafa Muro alisema kuwa, makubaliano ya wananchi na serikalj yatawezesha manispaa hiyo kuupanga mji huo kwa namna ilivyojiandaa.

Imeandikwa na Janet Josiah.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: