Kikao cha Naibu Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jaffo na watendaji jijini Arusha, almanusura kivunjike mara baada ya Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Goodbless Lema kumtuhumu mkuu wa wilaya hiyo, Mrisho Gambo kwa kutumia madaraka yake vibaya na kutokuheshimu mipaka yake ya kazi.

Lema amedai kuwa kitendo cha DC kuandika barua Tamisemi na kutoa nakala Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza ongezeko la posho za madiwani kutoka Sh100,000 hadi Sh120,000 zilizopitishwa na kupata baraka za Ofisi ya Katibu Tawala, kinaonesha anafanya siasa zisizo na tija.

Pia alimtuhumu kuingilia utaratibu wa vibanda vya wafanyabiashara kupitia madalali jambo linalopingwa na baraza la madiwani linaloongozwa na Chadema.

Hata hivyo Gambo alisema yeye ni kiongozi mkuu wa wilaya na vyombo vyote viko chini yake na anawajibika kuingilia kati pale anapoona kuna changamoto zinazohitaji kupatiwa ufumbuzi.

Alisema hatasita kuchukua hatua zinapaswa kwani ameaminiwa na Rais, ndio maana ameendelea na wadhifa huo na haitaji kujifunza ukuu wa wilaya kwani amekuwa kwenye nafasi hiyo kwa miaka mitano sasa.

CHANZO: MWANANCHI
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: