1. Mfanye ahisi kuwa yuko salama; acha kuwa mbabe na mgomvi!

2. Unapoingia nyumbaniToa salamu kwa upendo. Salamu humfukuza shetani nyumbani kwako!

3. Mke ni mfano wa chombo laini ni lazima kukitunza. Kumbuka kuwa kuna mambo mazuri utakayoyapata kwake,

4. Unapomshauri jambo, basi kaa naye faragha na katika mazingira yenye utulivu. Usifanye hivyo hadharani, kwa maana hiyo ni sawa na kumkashifu.

5. Kuwa mkarimu kwa mkeo- humfanya azidi kuwa na hisia ya upendo na kuendelea kuhisi kuwa anapendwa.

6. Mpishe kwenye kiti chako. Hilo litaupoza moyo wake.

7. Epuka ghadhabu na hasira. Kaa na wudhu muda wote. unapokuwa na hasira kaa chini, kama ulikuwa umekaa basi lala

8. Jitahidi kuonekana maridadi na unukie vyema kwa ajili ya mkeo. Huimarisha MAHABA!

9. Usiwe mgumu. Hilo litakuangusha. Kuwa mgumu na mkali haitakufanya kuwa mume bora.

10. Msikilize mkeo – KUWA MSIKILIZAJI MZURI.

11. Kubali kusifiwa na kubembelezwa, kataa mabishano na majibizano. Mabishano ni kama sumu katika ndoa. Mtu mmoja mwema aliwahi kusema: “Mwenyezi Mungu akiwapendelea watu shari huwaacha wabishane.”

12. Tuwaite wake zetu kwa majina mazuri kabisa, jina lolote ambalo mke anapenda kulisikia.

13. Mshangaze kwa mambo yenye kumvutia. Kama anapenda kitu fulani, mshtukize kwa kumletea kitu hicho bila yeye mwenye kutarajia. Itastawisha mahaba moyoni mwake.

14. Udhibiti ulimi wako! hivyo tazama unachoongea na namna unavyoongea!

15. Sisi sote tuna mapungufu. Yakubali mapungufu yake na Mungu ataweka baraka katika ndoa yenu.

16. Mwambie kuwa unamthamini. Muoneshe kuwa unamthamini na kutambua uwepo wake katika maisha yako.

17. Mhamasishe kuendeleza uhusiano mzuri na ndugu na wazazi wake.

18. Zungumza naye mada anayoipenda.

19. Mkiwa mbele ya ndugu zake msifu. Waambie kuwa ni mtu mzuri sana, na kwamba ni mtu mwema na unamshukuru Mungu kwa kumfanya kuwa mwenza wako.

20. Peaneni zawadi, mtazidi kupendana. Zawadi huongeza mahaba.

21. Achana na mambo yale yale ya kila siku angalau kwa muda fulani, mshangaze na kitu tofauti kabisa, hilo litaondosha kutu katika mahaba yenu na kuling’arisha penzi lenu.

22. kuwadhania vizuri wenzetu. Msimdhanie vibaya mkeo.

23. Yapuuze baadhi ya makosa yake…. Jifanye kuwa hujayaona. Usiyaingize akilini mwako.

24. Ongeza matone ya subira yako, hususan anapokuwa mjamzito au akiwa katika siku zake.

25. Tarajia na heshimu wivu wake.

26. Kuwa mnyenyekevu. Iwapo kazi yako ni nzuri, heshimu kwamba anawatunza watoto, anakuhudumia, anaihudumia nyumba yako unapokuwa haupo, nguvu yake ndio nguvu yako, na mafanikio yake ndio mafanikio yako.

27. Usiwafanye marafiki kuwa bora zaidi ya mkeo.

28. Msaidie mkeo kazi za nyumbani.

29. Msaidie kuwaheshimu wazazi wako, huwezi kumlazimisha kuwapenda, lakini unaweza kumsaidia kuwapenda hatua kwa hatua.

30. Muoneshe kuwa yeye ni mke bora, ni mke wa mfano.

31. Mkumbuke mkeo katika dua zako. Itaongeza mahaba na ulinzi wa ndoa yenu.

32. Yaache yaliyopita. Hayana msaada tena kwako zaidi ya kukuongezea maumivu na utungu. Muachia Mungu.

33. Usijaribu kuonesha kwamba unamfanyia hisani pindi unapofanya kitu, kama vile kununua chakula cha nyumbani, kwa sababu wewe sio mtoa riziki bali ni mfikishaji wa hiyo riziki. Pia ni njia ya kuwa mnyenyekevu na kuonesha shukrani kwa Mungu.

34. Shetani ndiye adui yako, sio mkeo. Wakati fulani mke na mume wanapozungumza shetani huingilia kati na kuchochea ugomvi, hivyo shetani ndiye adui wa kweli. Haitoshi tu kumchukia shetani, bali unatakiwa kumuona kama adui kama Mungu anavyoagiza. Shetani anapenda talaka. Kila siku anakutana na jeshi lake la maibilisi na kuwauliza kazi walizofanya, baadhi husema kuwa wamemshawishi mtu fulani kuiba au kunywa pombe na kadhalika. Yule anayesema kuwa amemfanya mtu fulani amtaliki mkewe husifiwa kuwa amefanya kazi bora kabisa.

35. Mlishe chakula kwa mikono yako. Ni jambo lenye baraka. Chakula hicho hakiishii tumboni tu, bali huenda moja kwa moja moyoni mwake. Huongeza mahaba na kuhurumiana baina yenu.

36. Mlinde mkeo dhidi ya shari za shetani na wanadamu. Yeye ni kama lulu ghali ambayo inatakiwa kulindwa dhidi ya hasadi za iblisi na shetani.

37. Muoneshe tabasamu lako. Tabasamu mbele yake. Kumbuka: TABASAMU NI SADAKA.

38. Matatizo na changamoto ndogo ndogo zinaweza kuwa tatizo kubwa. Kama una mambo madogo ambayo hayapendi nawe ukaendelea kuyarudiarudia, yatatengeneza ukuta mkubwa kati yenu. Usiyapuuze, yanaweza kuja kuwa makubwa.

39. Epuka kuwa mkali.

40. Heshimu fikra zake, muoneshe kwamba unapenda fikra na mawazo yake.

41. Msaidie kufikia mafanikio yake, kwa maana mafanikio yake ndio mafanikio yako.

42. Heshimu uhusiano wa ndoa na mipaka yake. Wakati fulani anaweza kuwa hajisikii vizuri; basi heshimu na uthamini hisia zake.

43. Msaidie katika utunzaji wa watoto. Baadhi ya wanaume hudhani kuwa jambo hilo linapunguza uanaume wao, lakini ukweli ni kwamba linakufanya uzidi kuheshimika, hususan mbele ya za Mungu.

44. Tumia tunu za ulimi na mazungumzo matamu. Mwambie anaonekana mrembo, maridhawa na maridadi. Tumia sanaa ya ulimi kuliboresha penzi lako.

45. Keti ushirikiane chakula na mkeo.

46. Mjulishe kuwa unasafiri. Usimshtukize, kwa maana hilo ni kinyume na Usitaarabu. Mwambie tarehe na muda utakaorudi kutoka safarini.

47. Usiondoke nyumbani pindi matatizo yanapoibuka.

48. Nyumba ina siri na faragha zake. Ukizipeleka siri hizi kwa marafiki na jamaa zako utakuwa unaweka shimo hatari sana katika ndoa yako. Siri ya nyumba hubaki nyumbani.

49. Hamasishaneni kufanya ibada; kwa mfano mnaweza kwenda kanisani au msikitini pamoja.

50. Zitambue na uzijue haki zake, sio tu kuziandika bali kuziingiza ndani ya moyo na akili yako.

51. Kuishini na wake zenu kwa wema’ Katika nyakati za raha na nyakati za shida ishi naye kwa wema na mahaba.

52. wakati wa mahusiano ya kimapenzi tunapaswa kuonesha heshima na kuwajali wake zetu.

53. Unapokuwa na khitilafu na mkeo usimwambie kila mtu. Ni kama kuliacha wazi jeraha lako, hivyo kuwa mwangalifu kwa wale unaowaelezea matatizo na khitilafu zenu.

54. Muoneshe mkeo kuwa unajali sana afya yake. Afya njema ya mkeo ni faida kwako na uzima wake ndio uzima wako. Kujali afya yake humuonesha kuwa unampenda kwa dhati.

55. Usidhani kuwa siku zote utakuwa sahihi. Hata uwe mwema kiasi gani lazima utakuwa na mapungufu. Ondokana na maradhi ya dhana hiyo.

56. Mhusishe katika matatizo, furaha na huzuni zako.

57. Mhurumie kwa udhaifu wake. Mhurumie wakati wote.

58. Kumbuka kuwa wewe ndo nguvu yake, wewe ndiye mtu anayemuegemea wakati wa tabu na dhiki.

59. Mkubali kama alivyo. Maandiko yanasema kuwa wanawake wameumbwa kutokana na ubavu uliopinda. Ukijaribu kuunyoosha utauvunja. unaweza usiipende tabia yake moja lakini utaipenda tabia yake nyingine, hivyo mkubali kama alivyo.

60. Daima uwe na nia njema kwa mke wako. Muda wote Mungu anaiona nia na moyo wako. Miongoni mwa ishara Zake ni kuwa amekuumbieni wake kutokana nanyi ili mpate kwao utulivu, na ameweka baina yenu mapenzi na kuhurumiana. Hakika katika hayo kuna ishara kwa wenye kutafakari.

NIWATAKIE SIKU NJEMA.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: