Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Viongozi wa Vyama vya Siasa Tanzania (UWASATA), Cecilia Augustino akifafanua jambo wakati alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, kupinga maandamano ya UKUTA. Kulia ni Katibu wa umoja huo Mwajuma Naty na Makamu Mwenyekiti Zaitun Hokororo.

Hussein Makame - MAELEZO

Umoja wa  Wanawake Viongozi wa Vyama vya Siasa Tanzania (UWASATA), umepinga  maandamano yasiyo na ukomo yaliyotanganzwa na Chama cha Demokrasia na  Maendeleo (CHADEMA) kwa kuwa hayana tija kwa wananchi na Tifa kwa  ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam  leo, Mwenyekiti wa umoja huo Cecilia Augustino, alisema maandamano hayo  yanaashiria uvunjifu wa amani ambayo ni urithi wa Taifa la Tanzania.

Alisema wamefikisha tamko lao kwa Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji  Francis Mutungi na kumtaka msajili kutoacha chokochocko hizo ziendelee  kwani zitasababisha kutoweka kwa amani nchini.

“Sisi wanawake  viongozi wa vyama vya Siasa Tanzania tunapinga azimio la maandamano  yasiyo na kikomo yanayoandaliwa na chama cha Chadema, hakika maandamano  hayo hayana tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla” alisema Hokororo na  kuongeza:

“Mheshimiwa Msajili, chokochocko hizi zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa kisiasa zikiachwa tu bila ya kukemewa tunaamini  tunu yetu ya amani ambayo ni urithi wetu tulioachiwa na waasisi wetu  itatoweka” .Aliongeza kuwa hatma ya maandamano hayo ni kuingia kwenye  machafuko na hatimaye mauaji na mateso kwa wanawake, watoto na walemavu, mambo ambayo hawatakubali yatokee.

Alibainisha kuwa wanawake viongozi wa vyama vya siasa wanaamini kuwa siasa ni kushindana kwa hoja  na si uvunjifu wa sheria kwa njia ya maandamano yasiyo na tija kwa  wananchi na Taifa.

Aliliomba Baraza la Vyama vya Siasa kuhakikisha  linawajibika katika kulinda demokrasia, amani na ustawi wa jamii nzima  ya Watanzania. Katika hatua nyingine, umoja huo unaojumuisha wanawake  viongozi wa vyama 22 vya siasa nchini, umeomba kufanya kongamano la  amani lenye lengo la kuhamasisha amani na utulivu nchini.

Hivyo, Hokororo aliwaomba viongozi wakuu wa nchi kuanzia Rais wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, wadau wa amani na  mashirika binafsi kushirikiana na umoja huo kufanikisha kongamano hilo.

“Hakika tunaumia wanasiasa wanapokuwa chanzo cha migogoro na vurugu kwa  Taifa letu.Hivyo tunamuomba Rais wetu tunajua ni msikivu aweze kuona  namna nzuri ya kutafuta suluhu ya mgogoro huu wa kisiasa” alisema  Mwenyekiti Cecilia Hokororo.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji  Francis Mutungi, tayari ameitisha Baraza la Vyama vya Siasa Agost 31,  mwaka huu ili kutoa fursa kwa pande vyama husika kukaa meza moja na  kujadili tofauti zilizopo na kuzipatia ufumbuzi.

Naye Makamu  Mwenyekiti wa umoja huo Ziada Athumani alisema wanaunga mkono hatua hiyo kwani ndio njia muwafaka ya pande husika ili kufikia muwafaka kwa njia  ya amani.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, wanawake  viongozi wa vyama vya siasa waliwakilishwa na wenzao kutoka vyama vya  Demokrasi Makini, ADA TADEA na Chama cha Umoja wa Demokrasi ya Vyama  Vingi (UMD).
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: