Friday, August 26, 2016

WATANZANIA TUPAZE SAUTI KUKATAA MAANDAMANO YA SEPTEMBA MOSI – CHEYO

Mwenyekiti wa UDP Mh. John Cheyo akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo
pichani) kwenye ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO mapema leo jijini Dar, akiwaomba viongozi wa chama cha CHADEMA, Kusitisha maandamano yao waliyoyapa jina la UKUTA, wanayotarajia kuyafanya Septemba Mosi nchi nzima, Mhe. Cheyo amekiomba chama hicho kutofanya maandamano hayo kwa lazima na badala yake watumie njia ilio sahihi ambayo ni ya mazungumzo ya mezani na kuendelea kuitunza amani ya nchi iliopo, pia amewaomba Watanzania kupaza sauti zao kuyakataa maandamano hayo yanayoweza kuharibu amani na utulivu wa nchi yetu.Pichani kulia ni Kaimu Katibu MKuu wa chama hicho Mhe. Goodluck Ole Medeye.

"Ukitaka kufanya maandamano,vyombo vya usalama vikikukatalia, basi usitumie  nguvu,jaribu kutafauta njia nyingine ambayo itakuwa ya amani zaidi kuliko kulazimisha,jambo ukililazimisha bila kufuata taratibu na sheria za nchi, matokeo yake hayatakuwa mazuri, yataleta machafuko na kutia doa  amani ya nchi yetu ambayo tumekuwa tukijivunia,hivyo nawasihii ndugu  zangu wa CHADEMA bado kuna njia nzuri za kufuata na kufikia muafaka wa  jambo hilo bila kusumbua amani ya nchi yetu iliopo kwa sasa" alisema Mhe. Cheyo.
Mhe. Cheyo akisitiza jambo wakati alipokuwa akijiabu maswali mbalimbali ya  waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo wa kukitaka chama cha  CHADEMA kusitisha maandamano yake, kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara  ya Habari MAELEZO,Vicent Tinganya.PICHA NA MICHUZI JR.

Na Lilian Lundo - MAELEZO, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Chama cha UDP John Cheyo amewataka Watanzania kupaza sauti na  kukataa maandamano ya Septemba Mosi mwaka huu ambayo yameandaliwa na  Chama cha Demokrasia (CHADEMA).

Cheyo ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu msimamo wake juu ya maandamano hayo.

“Watanzania wenzangu jambo la kuwaacha watoto wetu kwenda kupambana na Polisi si  jambo zuri, wote tupaze sauti zetu na kusema hapana kwa maandamano ya  Septemba Mosi,” alisisitiza Cheyo.

Alisema kuwa, ziko njia mbalimbali ambazo Chadema wanaweza kuzitumia kutatua  migogoro, kama vile meza ya mazungumzo na kuachana na maandamano ambayo  yanachochea vurugu na hata kutishia amani ya nchi.

Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linapotoa katazo la maandamano ni lazima utii  uwepo, kwani Polisi wapo kwa mujibu wa Sheria na Katiba. Ikiwa Chama  hicho hakikuridhika na katazo hilo basi wanatakiwa kuonana na Waziri anayehusika na Jeshi la Polisi.

Akifafanua zaidi alisema kuwa Rais Magufuli amekuwa akichukua hatua za makusudi za kutatua matatizo mbalimbali kama vile kupambana na ufisadi, ambapo  viongozi wengi wa Serikali wamesimamishwa kazi au kufukuzwa kutokana na  kujihusisha na masuala ya rushwa.

Mwenyekiti huyo wa UDP amewataka watanzania kumuunga mkono Mhe. Rais Magufuli ili  aweze kutimiza ndoto zake na yale ambayo ameyaahidi kwa ajili ya nchi ya Tanzania.

Aidha Cheyo aliwasifu viongozi wa Dini ambao walikaa na Viongozi wa Umoja wa  Katiba ya Wananchi (UKAWA) na kukubali kurudi bungeni bila pingamizi  lolote. Amewataka viongozi hao wa dini kuendelea kuzungumzia suala la  amani kwa Watanzania na Viongozi wa kiasa ili kudumisha amani ya nchi.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu