Wednesday, September 28, 2016

SERIKALI YAFUTA HATI 3 ENEO LA MAKABURI KINYEREZI


Jonas Kamaleki, MAELEZO

Wakazi wa Kinyerezi Sokoni, Dar es Salaam wameipongeza Serikali ya awamu ya Tano kwa kufuta hati tatu zilizokuwazimetolewa katika eneo la makaburi liliouzwa kinyume cha sheria.

Pongezi hizo zimetolewa leo kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi baada ya kumwagiza kamishna wa ardhi Kanda ya Dar es Salaam kufuta hati hizo mara moja na kulirejesha eneo la makaburi kwa wananchi.

Akiongea kwa niaba ya wakazi wa Kinyerezi, Mwanasheria, Mwinjuma Mzee amesema kuwa Wanakinyerezi wanamshukuru sana Mhe. Waziri kwa kurejesha eneo la makaburi kwa wakazi hao.
“Mhe. Waziri na msafara wake wote tunawashukuru kwa kumaliza mgogogoro huu ambao umedumu kwa muda mrefu na tumemwomba Waziri ashughulikie na maeneo mengine yanayohusu huduma za jamii kama zahanati na shule,” alisema Mzee.

Naye mkazi wa Kinyerezi, Bi. Maimuna Forogo ameelezea furaha yake kwa kumshukuru sana Mhe waziri kwa hatua aliyoichukua ya kubatilisha hati za umiliki wa makaburi.

“Mimi namnshukuru sana Mhe. Waziri na Serikali ya awamu ya Tano kwa ujumla kwa kutujali sisi wananchi, mimi kwenye makaburi haya nilimzika babu yangu sasa wanataka nimpeleke wapi kwanza ni mifupa mitupu,”alisema Maimuna.

Kwa upande wake, Mhe. Lukuvi amesema ameamua kubatilisha hati tatu za viwanja zilizotolewa na watumishi wasiowaaminifu wa Serikali ili eneo hilo liendelee kutumika kwa ajili ya maziko.

“Nimemuagiza kamishna anitafutie wahusika ambao walishiriki katika kumilikisha eneo la makaburi kwa watu ili wachukuliwe hatua za kinidhamu, watu hawa inabidi wafukuzwe kazi kwani kitendo cha kumilikisha eneo la kuzika hakivumiliki,”alisema Waziri Lukuvi.

Ameongeza kuwa watu ambao wanadiriki kuuza makaburi ambayo yametumiwa tangu mwaka 1962 na kwa sasa yapo zaidi ya 500, ni watu ambao hawana hata hofu ya Mungu hivyo kufukuzwa ni halali yao.

Mhe. Lukuvi ametoa wito kwa viongozi wenzake wanapofanya shughuli za mipangomiji nchini kutenga sehemu za huduma za jamii ikiwemo mahali pa kuzikia kwani kila mtu atakufa na anahitaji kuzikwa.  

“Serikali ya awamu ya Tano tumeamua kurekebisha pote palipokuwa pamepinda ili wananchi wapate haki zao,”alisema Lukuvi.

Aidha amewataka waliokuwa wamemilikishwa wafike wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili wampe Waziri uzoefu wanaoutumia kununua maeneo ya huduma za jamii ikiwemo maeneo ya makaburi ili imsaidie kujua jinsi mtandao ulivyo.
Hati tatu zilizofutwa ni 213, 215 na 217 Kitalu B, Kinyereze, Kata ya Segera jijini Dar es Salaam.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu