Meneja wa SUMOTO SUMITOMO CORPORATION Ndg. Hasnein Gulamhussein (wa pili kushoto)  akimkabidhi msaada wa vifaaa vya umeme wa jua (Solar panel kits) kwa uongozi wa Zahanati ya Magoda ikiwa ni jitihada za kampuni hiyo kuboresha sekta ta afya vijijini. 
---
Hyasinta Kissima, Afisa Habari H/Mji Njombe.

Halmashauri ya Mji Njombe imepokea msaada wa vifaa 06 vya umeme jua (Solar Kits) kwa ajili ya vituo 06 vya afya ndani ya Halmashauri hiyo. Vifaa hivyo vitakavyosaida utoaji wa nishati ya Mwanga hususani wakati wa kutoa huduma kwa kina mama wakati wa kujifungua zimekabidhiwa katika zahanati ya Magoda Halmashauri ya Mji Njombe.

Bi Neema Lazaro yeye ni Mratibu wa program ya Tubadili lishe kutoka shirika la CUAMM ambaye yeye amesema kuwa mchakato wa kuzitafuta Zahanati ambazo hazina chanzo chochote cha umeme ulifanyika kwa kushirikisha ngazi ya Wilaya na Mkoa hatimaye kuweza kuzitambua Zahanati hizo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo vya umeme wa jua (Solar Kits) Meneja wa SUMITOMO CORPORATION Ndugu Hasnein Gulamhussein amesema kuwa Ofisi yake kwa kushirikiana na shirika la MADAKTARI PAMOJA NA AFRIKA (CUAMM) wamesukumwa kutoa vifaa hivyo ili kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za afya na kuzingatia vituo vya afya vyenye uhitaji zaidi na ambavyo havijafikiwa na umeme wa Gridi ya Taifa.

“Ni furaha yetu kuona kila Mtanzania anafikiwa na umeme popote alipo. Kwa kuzingatia umuhimu wa umeme kwenye vituo vya afya vijijini awamu hii tumeweka kipaumbele zaidi katika upatikanaji wa umeme nafuu kwenye zahanati hizi.”

Akitoa salam za shukrani kwa niaba ya Ofisi ya Mganga Mkuu na Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Njombe, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kibena Dkt Celine Nyoni amewaomba wafadhili mbalimbali kuendelea kuisaidi Sekta ya afya katika zahanati zilizopo maeneo ya vijijini ambazo hazijafikiwa na umeme wa gridi ya Taifa kwani zahanati hizo zimekua zinatoa huduma kwa kinamama wanaojifungua wakati wa usiku kwa kutumia vibatari, taa na tochi jambo ambalo limekua linahatarisha maisha ya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

“Tulikua kwenye shida kubwa kwa kina mama wanaojifungua kwa sababu tulikua tunatumia taa na wakati mwingine vibatari halivcdxambayo imekua ni changamoto kubwa kwetu. Lakini leo tumepata ufumbuzi wa mwanga kwa hiyo wakina mama watajifungua salama kabisa katika vituo hivyo vyote vilivyopatiwa msaada huu.”Alisema Dk Celina.

Anaendelea kusema “Halmashauri yetu inajumla ya Zahanati 58 zilizopo vijijini na kati ya Zahanati hizo zenye huduma ya Nishati ya umeme ni 32 tuu na leo tunaongeza idadi ya Zahanati zenye Solar kuwa 38.Hivyo bado tunaupungufu wa Zahanati 20 ambazo hazina huduma ya umeme. Hivyo wito wangu kwa wadau wote wenye mapenzi mema kuendelea kutusaidia kwa ajili ya Zahanati zilizosalia ili kuendelea kuboresha Sekta ya Afya hususani maeneo ya Vijijini.

Zahanati zilizopatiwa msaada wa vifaa hivyo vya Umeme jua (Solar Kits) katika Halmashauri ya Mji Njombe ni Zahanati ya Magoda, Idunda, Iboya, utengule, makanjaula na Lusitu. Mikoa itakayofaidika na Msaada wa vifaa hivyo vya umeme jua (Solar Kits) ni Njombe na Iringa na Jumla ya Zahanati 50 zinatarajiwa kupatiwa vifaa hivyo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: