Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini Mhe, Hussein Bashe.
Meneja wa huduma kwa jamii wa Airtel Bi Hawa Bayumi.
Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini Mhe, Hussein Bashe (kushoto) akibadilishana mkataba wa thamani ya shilingi milioni 20 na Meneja wa huduma kwa jamii wa Airtel Bi Hawa Bayumi (kulia) mara baada ya kusaini mkataba huo Nzega na kushudiwa na mkuu wa wilaya wa Nzega Mh, Godfrey Ngupula. mkataba huo unaunganisha Airtel FURSA na asasi iliyoundwa kimikakati na Mbunge huyo ya Nzega Urban Trust Fund kwa lengo la kumaliza tatizo la umasikini wa kipato katika jimbo la Nzega Mjini, Programu hii itawawezesha vijana wajasiriamali waishio katika ya kata 10 zilizoko ndani ya Jimbo la Nzega Mjini mkoani Tabora kupata mikopo yenye riba nafuu itakayosaidia kutatua changamoto za ajira kwa vijana.
Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini Mhe, Hussein Bashe (kushoto) akisaini mkataba na Meneja wa huduma kwa jamii wa Airtel Bi Hawa Bayumi (kulia) huku mkuu wa wilaya wa Nzega Mh, Godfrey Ngupula akishudia, Airtel FURSA imefanya makubaliano hayo ili kushirikiana na asasi iliyoundwa kimikakati na Mbunge huyo ya Nzega Urban Trust Fund ili kumaliza tatizo la umasikini wa kipato katika jimbo la Nzega Mjini leo, Programu hii itawawezesha vijana wajasiriamali waishio katika ya kata 10 zilizoko ndani ya Jimbo la Nzega Mjini mkoani Tabora kupata mikopo yenye riba nafuu itakayosaidia kutatua changamoto za ajira kwa vijana.
---
Airtel Tanzania kupitia mpango wake wa Airtel FURSA “Tunakuwezesha” kwa kushirikiana na Nzega Urban Trust Fund asasi iliyoundwa kimkakati na Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini Mhe. Hussein Bashe ili kumaliza tatizo la umasikini wa kipato Jimbo la Nzega Mjini leo imezindua programu maalumu ya kuwezesha vijana iliyopewa jina la WanaNzengo Airtel FURSA. Programu hii itawawezesha vijana wajasiriamali waishio katika ya kata 10 zilizoko ndani ya Jimbo la Nzega Mjini mkoani Tabora kupata mikopo yenye riba nafuu itakayosaidia kutatua changamoto za ajira kwa vijana.

Programu hii iliyozinduliwa na Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini Mhe. Hussein Bashe, itawawezesha zaidi ya wajasiriamali 350 kunufaika na mikopo kupitia huduma ya Airtel Money. Mikopo hii itatolewa kwa kikundi kilichoundwa na vijana watano ambao watapewa mtaji kati ya shilingi Shs.100,000 hadi 1,000,000 kulingana na mahitaji yao.

Sambamba na mikopo ya WanaNzengo Airtel FURSA vikundi vya wajasirilamali vitapewa mafunzo ya ujasiriamali ikiwa ni pamoja na namna ya kuendesha vikundi pamoja na jinsi ya kutafuta soko, kusimamia mahesabu na nyenzo muhimu zitakazowapatia mafanikio katika biashara zao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo, Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini Mhe. Hussein Bashe aliupongeza uongozi wa Airtel Tanzania kwa kuanzisha utaratibu wa kuwawezesha vijana hapa nchini kwa kutoa mitaji ya kibiashara ili kuinua maisha zao. Katika hotuba yake alisema “programu hii itawasaidia vijana wa jimbo la Nzega mjini kujikwamua kiuchumi na hatimae kubadilisha maisha yao. Nawahimiza vijana kujiunga na vikundi vya ujasiriamali kuepusha wimbi la ukosefu wa ajira nchini na kuacha tabia ya kushiriki katika vitendo viovu ambavyo vinahatarisha maisha yenu na usalama wa taifa kwa ujumla. Programu hii imedhamiria kuwasaidia, kuwajenga na kuwainua vijana wa hapa Nzega Mjini wanawake kwa wanaume, hivyo nawahimiza kuitumia fursa hii kwa manufaa yenu na jamii kwa ujumla”. Alisema Bashe

“Ninawapongeza Airtel kwa kuona vyema kuungana nasi katika kutekeleza juhudi zetu za kuhakikisha tunainua uchumi mdogomdogo na kuwawezesha wajasiriamali kuwa na mitaji tena isiyo na riba kubwa na yenye masharti nafuu kabisa itakayowasaidia kukuza kipato chao. Tumejipanga kuhakikisha kiasi hiki cha shilingi millioni 20 kilichotolewa na Airtel kinatumika vyema ili kuweza kuwafikia wajasiriamali wengi zaidi, pesa hizi zitazunguka mikononi mwa wajasiriamali na hivyo tunahimiza vikundi vitakavyokopa viweze kurejesha mikopo yao kwa wakati bila usumbufu ili wengi waweze kufaidika na programu hii” Alisistiza Mhe. Bashe.

kwa upande wake Meneja huduma kwa Jamii wa Airtel, Hawa Bayumi alisema “tunaelewa changamoto nyingi ambazo vijana wamekuwa wakikutana nazo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ajira na hata pale wanapotaka kujiajiri huwa hawana mtaji wa kuanzisha biashara. Nchini Tanzania, vijana wapatao 1,000,000 kila mwaka wanakosa ajira na hii ni changamoto kubwa sana. Tunaamini ushirikiano huu kati ya Airtel FURSA na Nzega Trust Fund kutachochea ujasiriamali na kuwawezesha vijana wetu kuanzisha biashara na kujiajiri hapa Nzega Mjini.

Mpaka sasa Airtel FURSA “Tunakuwezesha” imewawezesha vijana zaidi ya 5,000 kwa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali na vitendea kazi kote nchini. Tunaahidi kuendeleza falsafa hii tukitambua vijana ndio chachu ya maendeleo katika jamii yoyote na pia nawahimiza vijana wa Nzega Mjini kuchangamkia fursa hii sasa” alisema Bayumi.

Ili kupata mkopo kikundi kitatakiwa kuwakilisha fomu yao ya maombi ikiambatanishwa na barua ya udhamini wa ukaazi kutoka Serikali ya Mtaa wanakoishi ikionesha anuani yao ya makazi pamoja na wazo la biashara ambalo litajadiliwa na kupitishwa na jopo la wataalamu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: