Monday, October 3, 2016

WAFADHILI WAFURAHISHWA NA UKAUSHAJI WA MBOGA MBOGA WA WANAWAKE MOROGORO


Mkurugenzi wa mawasiliano wa taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika, Anna Salado (kulia), akipakua mboga zilizopikwa kiasili na kuungwa kwa nazi wakati yeye na ujumbe wake walipotembelea mradi wa ukaushaji wa mboga na matunda wa wanawake wa Kata ya Mzinga mkoani Morogoro hivi karibuni. Kushoto ni Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Milikieli Mansweat Mahiku.

Mratibu wa mradi wa Green Voices kutoka taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika ya Hispania, Alicia Cebada, akiwa ameshikilia pakiti ya kisamvu kilichokaushwa na kufungashwa huku akiwapongeza wanawake wa kikundi cha Mzinga katika Kata ya Mzinga, Manispaa ya Morogoro
kwamba wamefanya kazi nzuri sana. Mwenye fulana nyeupe ni Bi. Esther Muffui, mshiriki kiongozi wa mradi huo.

SIYO tu mapishi ya asili ya kisamvu kikavu kilichoungwa kwa nazi, lakini mafanikio makubwa katika ukaushaji na usindikaji wa mboga na matunda katika mradi wa wanawake wa Kata ya
Mzinga, Manispaa ya Morogoro yamewavutia wahisani wa taasisi ya Women for Africa Foundation kutoka Hispania.

Hali hiyo imewafanya wanawake hao wawe katika nafasi kubwa zaidi ya kusonga mbele ikiwa wafadhili hao watatoa tena fedha katika awamu ya pili ya mradi wa Green Voices unaotekelezwa nchini Tanzania.

Akizungumza katika Kijiji cha Konga kwenye Kata hiyo, mratibu wa mradi huo kutoka Hispania, Bi. Alicia Cebada, alisema kwamba licha ya kuwa na muda mfupi tangu kuanza kwa mradi huo, lakini wanawake hao wamefanya mambo makubwa ambayo yanastahili kuungwa mkono.

“Hii teknolojia ya ukaushaji wa mboga na matunda ni rahisi na inafaa sana kwa uhifadhi wa chakula,
kinachotakiwa ni kwa wanawake hawa kuwezeshwa zaidi,” alisema Alicia ambaye aliongozana na Mkurugenzi wa habari wa taasisi hiyo, Anna Salado, na ofisa mwandamizi wa taasisi hiyo anayeshughulikia masuaa ya ubunifu, Bi Noellia pamoja na mratibu wa Green Voices Tanzania, Bi. Secelela Balisidya.

Alicia alisema kwamba, changamoto ndogo wanazokabiliana nazo wamezisikia, lakini akasema katu
zisiwakatishe tamaa kwa sababu inaonyesha dhahiri wanaweza kufanya mambo makubwa mbele ya safari.

Maofisa wa taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika kutoka Hispania wakiwa katika picha ya pamoja na wanakikundi wa Mzinga (wenye sare). Kulia ni mratibu wa mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya.

Mratibu wa mradi wa Green Voices kutoka Hispania, Alicia Cebada, akiuliza jambo kuhusu namna ya ukaushaji wa matunda.


Bi. Esther Muffui, mshiriki kiongozi wa kikundi cha Mzinga Women Group mjini Morogoro kinachotekeleza mradi wa Green Voices kwa ukaushaji wa mboga na matunda, akieleza jambo wakati ujumbe kutoka taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika ulipotembelea mradi huo hivi karibuni.

Matayarisho ya mboga mbichi kabla ya kuikausha.

Hapa sasa mboga inasambazwa tayari kwa kuwekwa kwenye kaushio.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu