Monday, November 7, 2016

DC KINONDONI AHITIMISHA AWAMU YA KWANZA YA ZIARA YAKE MSASANI

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Salum Hapi leo amehitimisha awamu ya kwanza ya ziara yake ambapo amefanya jumla ya mikutano 24, ikiwemo 10 ya hadhara na 14 ya ndani ikijumuisha kamati za maendeleo za kata na mazungumzo na wazee.

Katika awamu hiyo ya kwanza Mh. Hapi ametembelea wastani wa mitaa 50 ambako amekagua miradi mbalimbali kama shule, masoko, maji, zahanati, barabara, madaraja, maeneo ya wazi na vikundi vya ulinzi shirikishi.

Akihitimisha awamu ya kwanza ya ziara yake Hapi amewataka watendaji wote wa Serikali za Mitaa Kinondoni kutumia mashine za kieletroniki kwenye shughuli zote za ukusanyaji wa mapato na michango ya wananchi ikiwemo matumizi yake.

Akizungumza katika kata ya Msasani Mkuu wa wilaya ya Kinondoni ameelezea kuwa timu yake ya ziara inapumzika kwa muda ili kujipa muda na nafasi ya kufanya tathimini ya ziara, kuandaa taarifa ya changamoto, maagizo na maelekezo mbalimbali ili kuyawekea mpango wa utekelezaji na kufatilia utekelezaji wake.

DC Hapi ameeleza kuwa matumizi ya mashine hizo za EFD yataisadia uwekaji wa kumbukumbu vizuri, kudhibiti ubadhirifu na kuwezesha serikali kupata taarifa hizo kwa usahihi.

Mh. Hapi amesisitiza kuwa ni vyema zoezi hilo likaanza maramoja kwani kata zote zimepatiwa mashine hizo za EFDS na viongozi hao watambue kuwa fedha wanazokusanya kwa wananchi kwa ajili ya usafi na ulinzi shirikishi ni za wananchi na hivyo inabidi zitumiwe kama walivyokubaliana kwenye mikutano mikuu ya mitaa na sio vinginevyo.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya huyo amezindua magari mawili ya taka aina ya trekta kwa ajili ya uzoaji taka, ambayo yametolewa na Meya wa manispaa ya Kinondoni Mstahiki Benjamin Sitta.

Aidha DC Hapi ameahidi kuwashughulikia watendaji wote wasioendana na kasi ya Rais Magufuli na kupiga marufuku uzembe, rushwa na ukandamizaji.

Mkuu wa wilaya ameshiriki kikao cha maendeleo ya kata (WADC), kupokea taarifa ya maendeleo ya kata, kuzungumza na wazee wa kata hiyo pamoja na kufanya mkutano wa hadhara kusikiliza kero mbali mbali zinazowakabili wananchi wa kata hiyo.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu