Monday, November 28, 2016

UZINDUZI WA SIKU 16 ZA MAADHIMISHO YA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA MKOA WA SHINYANGA

Hapa ni katika barabara ya Shinyanga - Tabora, maandamano ya wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia mkoa wa Shinyanga ambao ni Jeshi la polisi, Agape, ICS, PACESH, Rafiki, Red cross,ofisi ya mkurugenzi manispaa ya Shinyanga na wadau mbalimbali wakati wa uzinduzi wa siku 16 za maadhimisho ya kupinga ukatili wa kijinsia duniani mkoa wa Shinyanga.---

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo wenye kauli mbiu ya ‘Funguka sema hapana kwa ukatili wa kijinsia,elimu salama kwa wote’ alikuwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro aliyemwakilisha mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack.

Takwimu zinaonesha kuwa tatizo la ndoa za utotoni kwa mkoa wa Shinyanga ni 59% ikifuatiwa na Tabora 58% na Mara 55%.

Pia kwa wastani takribani watoto wawili kati ya watano nchini Tanzania wanaolewa chini ya umri wa miaka 18 na kwa mwaka 2010 pekee 37% ya wanawake wenye umri kati ya 20-24 walikuwa wameolewa au walikuwa katika mahusiano ya kimapenzi kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Kwa mujibu wa utafiti wa UNFPA katika wilaya ya Kahama na Kishapu unaonesha kuwa zaidi ya watoto 500 wa kike katika mkoa wa Shinyanga huacha shule kwa sababu ya mimba za utotoni kila mwaka.

Kwa mujibu wa taarifa ya UNFPA (2013) asimilia 45 ya wanawake wenye umri wa miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili katika mkoa wa Shinyanga na Mwanza kwa kipindi cha mwaka 2010 pekee na 25% ya wanawake mkoani Shinyanga wamefanyiwa ukatili wa kingono.

Mwandishi wetu Kadama Malunde,alikuwepo kwenye uzinduzi wa siku 16 za maadhimisho ya kupinga ukatili wa kijinsia mkoa wa Shinyanga leo Novemba 26, 2016.
Siku 16 za harakati dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia ni kampeni ya kimataifa iliyoanzishwa na taasisi ya kimataifa ya wanawake katika uongozi ‘Women Global Leadership Institute’iliyoanzishwa mwaka 1991 nchini marekani kwa nia ya kuamsha ari ya kuzuia na kupambana na ukatili dhidi ya wanawake kwa kuzingatia haja ya kuleta usawa wa kijinsia.
Wanafunzi wakiwa wamebeba mabango.
Kampeni hiyo ilianzishwa ikiwa ni matokeo ya mauaji ya wanawake yaliyotokea 1960 Mirabele nchini Dominica wakiwa katika harakati za kupinga utawala wa kidikteta wa rais wan chi hiyo Raphael Truijilo na kuhitimishwa tarehe 10 Desemba ambayo ni siku ya kimataifa ya tamko la haki za binadamu ikiwa ni ishara ya kuhusisha ukatili dhidi ya wanawake na haki za binadamu kwani ukatili huu ni uvunjwaji wa haki za binadamu.
Meza kuu wakiongozwa na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro aliyemwakilisha mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack wakipokea maamandamano hayo.
Meza kuu wakishikana mkono na mwanamke aliyetoa ushuhuda namna alivyofanyiwa unyanyasaji wa kijinsia na mme wake. Wa kwanza kushoto ni mkurugenzi wa shirika la Agape Aids Control Programme, John Myola.
Afisa kutoka shirika la ICS Shadia Nurdin akisoma risala ya wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia ambapo alisema changamoto wanazokabiliana nazo ni pamoja na sheria kinzani,sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ambayo inaruhusu mtoto kuolewa chini ya miaka 18. Changamoto zingine alizitaja kuwa ni mila potofu ikiwa ni pamoja na kuenzi ngoma za wakato wa mavuno mathalani ukango,uswezi, bukwilima, samba na nyinginezo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro akizungumza katika uzinduzi huo ambapo alisema jeshi la polisi lina majukumu ya kusimamia sheria na mikataba ya kimataifa ambayo inahusiana na masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia na watoto lakini hawawezi kusimamia peke yao bali wanahitaji ushirikiano na taasisi zingine na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha kuwa ukatili unamalizika katika jamii.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro aliwataka wananchi wote kuwa mstari wa mbele kupinga ukatili wa kijinsia na watoto.

Mgeni rasmi Josephine Matiro akizungumza wakati wa uzinduzi wa siku 16 za maadhimisho ya kupinga ukatili wa kijinsia duniani mkoa wa Shinyanga ambapo aliwataka akina mama katika jamii kupaza sauti badala ya kunyamaza kimya na kuogopa kutoa ushahidi mahakamani pindi wanapotendewa ukatili katika familia zao huku akiwaasa kukaa karibu na watoto wao ili watoto hao waweze kuwasimulia kama wanatendewa vitendo vya kikatili.

Matiro aliwaomba viongozi wa madhehebu ya dini mkoani Shinyanga kufungua makanisa na misikiti maeneo ya vijijini ili watu wawe na hofu ya mungu waache kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Mkuu wa dawati la jinsia na watoto mkoa wa Shinyanga Pili Misungwi alisema suala ukatili wa kijinsia ni tatizo kubwa katika jamii hivyo dawati lake linaendelea na jitihada za kuwatafuta, kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria watu wote wanaojihusisha na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Misungwi alisema siku 16 za harakati dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia ni kampeni ya kimataifa iliyoanzishwa kwa lengo nia ya kuamsha ari ya kuzuia na kupambana na ukatili dhidi ya wanawake kwa kuzingatia haja ya kuleta usawa wa kijinsia.Alisema katika siku hizo 16 wataendelea kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia na hata baada ya siku hizo 16,wataendelea na utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi na kuwashughulikia watu wote wanaojihusisha na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu